1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa vyama wasaini kiapo cha utiifu kwa Kabila

Iddi Ssessanga
21 Februari 2019

Rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila ambaye alikabidhi madaraka kwa Felix Tshisekedi, amewasainisha viongozi wa muungano wake wa FCC kiapo cha utiifu kwake. Muungano wa Kabila wa FCC ndiyo wenye viti vingi zaidi bungeni.

https://p.dw.com/p/3DnNL
Kongo Joseph Kabila, Präsident
Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Kabila wa Common Front For Congo FCC, unasalia kuwa wenye nguvu zaidi bungeni, baada ya kupata wingi mkubwa wa viti katika uchaguzi wa Desemba 30, ambao pia ulimpa ushindi wa urais kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi.

Karibu mwezi mmoja baada ya makabidhiano ya mdaraka, rais mstafu Joseph Kabila aliwakusanya viongozi wa vyama 18 vinavyounda muungano wake kwenye shamba lake lililopo Kingakati, karibu na Kinshasa, ilisema FCC katika taarifa.

Iliongeza kwamba aliwafanya wasaini waraka wa dhamiri wenye nukta muhimu saba. Juu ya orodha: "Tunasisitiza uaminifu wetu na utiifu wetu kwa Mh. Joseph Kabila Kabange, rais wa heshima wa Jamhuri."

DR Kongo  Kinshasa Vereidigung Präsident Felix Tshisekedi
Rais wa DRC Felix Tshisekedi akipokea mshipi wa urais kutoka kwa mtangulizi wake Joseph Kabila.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Chama cha Tshisekedi cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) kilipata viti 32 tu vywa uwakilishi bungeni. Bado hajateuwa waziri mkuu na amekuwa akifanya kazi na timu ya mpito ya serikali ilioachwa na mtangulizi wake.

Viongozi vya vyama vya FCC waliokutana Jumatano walikubaliana kuubadili muungano huo kutoka ushirika wa uchaguzi na kuufanya kuwa "jukwaa la kisiasa la serikali." Hii haimaanishi kuwa watapitia upya makubaliano ya kugawana madaraka walioujadili na Tshisekedi, ilisema FCC.

Kulingana na Lambert Mende, msemaji wa serikali na FCC, Tshisekedi na Kabila walikuwa na "makaribiano ya kiitikadi." Aliwaeleza wote kama "Wasocial Demokrat." Viongozi hao walikuwa na mazungumzo juu ya kuunda serikali ya muungano siku ya Jumapili.

Kuchaguliwa kwa Tshisekedi kuliashiria mabadiliko ya kwanza ya amani ya uongozi nchini DRC tangu ilipopata uhuru wake kutoka Ubelgiji mwaka 1960. Alichukuwa madaraka kutoka kwa Kabila alieiongoza nchi hiyo kwa miaka 18.

Mgombea mwingine wa upinzania, Martin Fayulu, anapinga uhalali wa uchaguzi wa Desemba 30.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Grace Patricia Kabogo