1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuta n'kuvute vyama vya siasa Tanzania kuhusu DP World

24 Julai 2023

Vyama vya kisiasa nchini Tanzania sasa vimeanza kutumia majukwaa ya wazi na mikutano ya hadhara kuwashawishi wananchi juu ya kile kilichomo kwenye mkataba wa bandari kati ya nchi hiyo na kampuni ya kigeni ya DP World

https://p.dw.com/p/4UJPd
AfCFTA
Picha: Xinhua News Agency/picture alliance

Karata za vyama vya siasa kugeukia majukwaa ya wazi inakuja wakati wingu nene likiendelea kugubika hatma ya makubaliano ya mkataba huo ambao mjadala wake umegeuka mada inayotupiwa macho kila uchao.

Chama kikuu cha upinzani Chadema kikiwa na viongozi wake wakuu, kimeanza kuwaalika wanaharakati pamoja na vigogo wa sheria na viongozi wa dini, kuuchambua na kuukosoa mkataba huo huku kikizidisha lawama kwa serikali katika kile inachosema kuingia kwenye mikataba mibovu.

Hoja zinazotolewa na chama hicho pamoja na wanasheria zinaakisi kile kinachoelezwa kuhusu baadhi ya vipengele kwenye mkataba huo kukosa afya kwa ustawi wa taifa, kama vile wawekezaji kuwa na usemi mkubwa kuhusu bandari za Tanzania.

Soma Pia:Waziri Makame Mbarawa atetea makubaliano na DP World

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika maeneo ya Temeke jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema taifa linapaswa kuwa na usemi mmoja kupigania maslahi ya taifa na kukikosoa chama tawala CCM katika kile alichosema "kutengeneza mzigo usiobebeka”

Kwa mara ya kwanza mjadala kuhusu mkataba wa DP World umewakaribisha katika meza moja wanasiasa waliowahi kuhitilafiana huko nyuma.

Mwanasiasa wa zamani na aliyewahi kuwa kiongozi wa Chadema, Dr Wilbroad Slaa alitumia jukwaa hilo hilo kuukosoa mkataba huo huku akiwahimiza wanasiasa wengine kurejea katika meza ya umoja kwa ajili ya kupaza sauti.,

"Tulialika vyama vingine na dakika za mwisho wakajitoa, tukiacha unafiki huu hii nchi haitabomolewa." Alisema mwanasiasa huyo ambae aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweeden.

CCM:Serikali kamilisheni haraka mkataba wa bandari

Nacho chama tawala CCM kinazunguka katika maaeneo mbalimbali ya nchi kuunadi mkataba huo na kuweka msimamo wake kikisema kitaendelea kuutetea.

Tansania Dodoma Präsidentin Samia Suluhu Hassan CCM-Partei
Chama tawala CCM Tanzania kikiwa katika mkutanoPicha: CCM office

Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chongolo anayezunguka na makada wake pamoja na maafisa wa serikali wakiwemo mawaziri ndiye anayeongoza ajenda ya kuusemea mkataba huo.

“Hatuna hofu wala shaka na kwamba jambo hili ni utekelezaji wa ilani ya CCM, wanaongaika kulifanya suala la bandari liwe la Samia, wameshindwa kusoma alama za nyakati.Tumewagundua na tumewajua pamoja na njia wanazozitumia,” alisema Chongolo.

Soma pia:Viongozi Tanzania wadai kutishiwa kuhusu suala la Bandari

Hayo yakiendelea bado haijajulikana nini hatma ya mjadala huo, na kile kinachosubiriwa na wengi ni kuona kwamba hoja za upande upi zitazingatiwa iwapo mjadala huo utafikia tamati.

Serikali ya Tanzania na Dubai ziliingia mkataba Oktoba 25 mwaka jana kwa ajili ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari (IGA).

Bunge limeshapitisha azimio la kuridhia ushirikiano huo kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya DP World inayomilikiwa na Serikali ya Dubai.

Makubaliano hayo yalibainisha maeneo mahususi ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandariza bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.