1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi 40 wa Houthi wauwawa kwenye mapigano Yemen

Josephat Charo
27 Juni 2021

Mapigano yamechacha kati ya vikosi vya serikali ya Yemen na waasi wa Houthi katika jimbo lenye utajiri mkubwa wa nishati la Marib yaliyosababisha vifo vya waasi wapatao 40.

https://p.dw.com/p/3vdjA
Saudische Luftangriffe im Jemen
Picha: AFP

Waasi hao wanaoungwa mkono na Iran walianzisha uvamizi mwezi Februari kuuteka mji wa Marib, eneo la mwisho lililo chini ya udhibiti wa serikali ya mjini Sanaa inayoungwa mkono na Saudi Arabia kaskazini mwa Yemen.

Miito ya kimataifa imekuwa ikitolewa kukomesha harakati za kijeshi na kuyafufua mazugumzo ya kutafuta amani kwa lengo la  kufikisha mwisho vita vya Yemen vilivyodumu zaidi ya miaka sita.

Makabiliano makali yalizuka kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa Houthi mjini Marib kuanzia Jumamosi usiku hadi mapema Jumapili, alisema luteni kanali Abdel-Raqeeb al Shadadi, mshauri wa jeshi la serikali alipozungumza na shirika la habari la Ujerumani dpa.

Mshauri huyo aidha alisema kulifanyika mashambulizi kadhaa ya Wahouthi katika maeneo yanayodhibitiwa na vikosi vinavyoiunga mkono serikali katika eneo hilo. Ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zilifanya mfululizo wa mashambulizi dhidi ya waasi na vifaa vyao vya kijeshi.

Pande zote mbili zapata hasara

"Jeshi lilitibua mashambulizi ya waasi, kuwaua zaidi ya wapiganaji 40, kuwajeruhi wengine na kuwateka wengine kadhaa," alisema. "Mapigano hayo pia yalisababisha majeruhi madogo ambayo hayakufafanuliwa miongoni mwa vikosi vya serikali," aliongeza.

Jemen Sanaa | Houthi Soldaten
Wanajeshi wa Houthi wakiwa katika gwaride wakati wa mazishi ya wapiganaji wenzao waliouwawa hivi karibuni wakati wa mapiganao na vikosi vya serikali mjini MaribPicha: Khaled Abdullah/REUTERS

Mpaka sasa hakujatolewa kauli yoyote na upande wa waasi.

Yemen imegubikwa na mapambano ya uharibifu mkubwa ya kung'ang'ania madaraka tangu mwaka 2014, wakati waasi wa Houthi walipouteka mji mkuu Sanaa na maeneo mengine ya nchi.

Miezi kadhaa baadaye, wakati waasi waliposonga mbele kuukarabia mji mkuu wa muda wa Aden, Saudi Arabia iliunda muungano wa kijeshi kuiunga mkono serikali ya Yemen na vikosi vyake dhidi ya Wahouthi mnamo Machi 2015.

Mzozo huo umeisukuma Yemen kukaribia kutumbukia katika baa la njaa na kuviharibu vituo vyake vya afya. Janga la virusi vya corona pia limeuchochea na kuuongezea makali mzozo huo katika taifa hilo masikini.

(dpa)