1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa M23 wauteka mji wa madini wa Rubaya nchini Kongo

1 Mei 2024

Taarifa zinasema kuwa ni baada ya mapigano makali kati ya M23 na jeshi la Kongo ndipo kundi hilo lilifaulu kuuteka mji huo muhimu ambamo raia wote wamekimbia.

https://p.dw.com/p/4fOPq
Mji wa Rubaya Kivu ya Kaskazini unashuguli nyingi za uchimbaji madini ya kimkakati mfano wa Coltan
Mji wa Rubaya Kivu ya Kaskazini unashuguli nyingi za uchimbaji madini ya kimkakati mfano wa ColtanPicha: DW/S. Schlindwein

Mji  wa Rubaya wenye migodi mikubwa ya madini huko wilayani Masisi karibu kilometa 65 kutoka Goma, ulidhibitiwa na waasi wa M23 mwaka mmoja baada ya kuondoshwa na wapiganaji vijana wazalendo Februari mwaka jana.

Milio ya mizinga ilisikika mchana kutwa wa hiyo jana Jumanne kote kwenye mji huo ambamo M23 walikuwa wakizilenga kwa makombora ngome zote za jeshi la serikali ambalo halikufaulu kuwazuiya. Upande wao raia wamesema kuwa na wasiwasi  kufuatia ukimya wa kikosi cha nchi za jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika, SADC ambacho hadi sasa kimeshindwa kukabiliana na waasi hao.

''Ni kweli kabisa mji wa Rubaya umedhibitwa na waasi wa M23 tangu hiyo jana Jumanne, kwetu ni mshangao sababu licha ya kuwepo kwa jeshi la SADC waasi wanasonga mbele na bila kuwazuiya na hata kutokabiliana nao", alisema mkazi wa Rubaya ambaye hakutaka  kutajwa jina lake.

''Tunalo jeshi lenye nguvu lakini tatizo ni kwamba limekosa msaada''

Kongo DRK UN-Mission MONUSCO im Sake im Ost-Kongo,
Picha: DW/Flávio Forner

Kulingana na asasi za kiraia,udhibiti wa mji wa Rubaya umekuwa ni tukio baya kwa jeshi la serikali ya Kongo ambalo halijatoa taarifa kuhusu  kuchukuliwa kwa mji huo wa kimkakati. Ombeni KATABAZI ni afisa mkuu kutoka muungano wa mashirika ya kiraia mkoani kivu kaskazini amepoteza matumaini yake kwa upatikanaji wa amani.

"Rubaya ni mji wa madini na ulimwengu mzima unategemea hapo ,kwa hiyo jinsi waasi walivyouchukuwa mji huo sisi kwetu tumepoteza matumaini. Tunalo jeshi lenye nguvu lakini tatizo ni kwamba limekosa msaada.'', alisema Katabazi.

Kabla ya kuendelea kusema : ''Tunawasihi viongozi wetu kuchukua hatua za haraka na kutafuta mbinu mbadala ili kurejesha utulivu''.

Hadi leo asubuhi mamia wa raia wa Rubaya wameendelea kukimbilia msituni huku wengine wakinasa bado majumbani mwao kufuatia milio ya risasi inayosikika kwenye milima inayoinukia mji huo, vimethibitisha vyanzo vya ndani. 

Wako wapi wanajeshi wa jumuiya ya SADC ?

Kwa miezi kadhaa sasa ,waasi wa M23 walikuwa wakijaribu  bila mafanikio kuudhibiti mji huo wenye madini  ambamo  viongozi wa mashirika ya kiraia ,hata hivyo,walishutumu uuzaji haramu wa madini unaofanywa na vijana wapiganaji wazalendo. 

Haya yanajiri miezi minne baada ya kutumwa hapa mkoani kivu kaskazini kwa kikosi cha SADC  ambacho hadi sasa hakijaanzisha mashambulizi ya ardini dhidi ya kundi la M23 linalouweko mji wa Goma kwenye hali  hatarishi.