1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanachama wa G20 wakubali kudhibiti biashara ya mtandao

John Juma
28 Juni 2019

Rais Donald Trump ameonekana kuchukua mwelekeo wa upatanishi miongoni mwa viongozi wenzake licha ya mivutano iliyopo kati yake na China na pia Iran.

https://p.dw.com/p/3LHhr
Japan Osaka | G20 Gipfel | Joko Widodo | Moon Jae-in
Picha: President Secretary/Laily Rachev

Kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda na zile zinazoinukia kiuchumi ulimwenguni G20, zimekubaliana zenyewe kudhibiti biashara ya mtandaoni. Hayo yamesemwa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakati ambapo viongozi wa nchi hizo wakikutana kwenye mkutano wa kilele mjini Osaka Japan. Wakati huohuo Rais Donald Trump ameonekana kuchukua mwelekeo wa upatanishi miongoni mwa viongozi wenzake licha ya mivutano iliyopo kati yake na China na pia Iran. 

Kwenye mkutano huo, rais wa Marekani Donald Trump ameonekana kuchukua mkondo wa upatanisho na viongozi wengine licha ya migawanyiko mikubwa iliyoko kuhusu biashara na mabadiliko ya tabia nchi.

Trump alimtaja kansela wa Ujerumani kuwa mwanamke mzuri na anafurahi kuwa naye kama rafiki. Hii ni licha ya mashambulizi yake ya awali dhidi ya Ujerumani kuhusu mchango wake kifedha katika jumuia ya kujihami NATO. Trump na Merkel wanatarajiwa kufanya mkutano leo jioni kujadili masuala ya kimahusiano kati ya nchi zao ikiwemo biashara na uwekezaji. Bibi Merkel ameongeza pia kuwa:

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwa na rais wa China Xi Jinping
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwa na rais wa China Xi JinpingPicha: picture alliance/dpa/B. von Jutrczenka

"Tutajadili masuala ya kimataifa haswa yale ambayo yamekuwa yakitokea Afrika magharibi. Pia tutazungumzia vita dhidi ya ugaidi na ninatarajia mazungumzo mazuri. Bila shaka Iran pia itakuwa kwenye ajenda yetu"

Vilevile Trump alimsifu waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo kwa kuruhusu kampuni nyingi za magari ya Japan kuwekeza Marekani. Huku mzozo kati ya Marekani na China kuhusu nyongeza kwa ushuru wa bidhaa, pamoja na mzozo wa Iran na Marekani, halikadhalika suala tete la athari za mabadiliko ya tabia nchi, ukitishia kugubika mkutano huo, Abe ametoa wito wa kukuza umoja miongoni mwa wakuu wa nchi hizo.

Katika kikao maalum, viongozi wa nchi hizo zenye nguvu zaidi kiuchumi duniani G20, wamekubaliana kuwepo na sheria au kanuni za kimataifa katika nyanja ya kidijitali na intaneti. Kansela Angela Merkel amewaambia waandishi wa habari kuwa anaamini makubaliano ya kudhibiti sekta ya mitandao yanapaswa kutekelezwa na shirika la Biashara Duniani (WTO), lakini akaelezea pia kuwa udhibiti huo mara nyingi hulemaza maendeleo ya uchumi wa kidijitali.

Rais wa indonesia Joko Widodo akikutana na rais wa Korea Kusini pembezoni mwa mkutano wa G20 mjini Osaka.
Rais wa indonesia Joko Widodo akikutana na rais wa Korea Kusini pembezoni mwa mkutano wa G20 mjini Osaka.Picha: President Secretary/Laily Rachev

Kwa upande mwingine, Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amemhimiza rais wa Urusi Vladimir Putin kumaliza matendo yanayotishia Uingereza na washirika wake, ikiwa anataka mahusiano kati ya nchi yake na mataifa ya magharibi yaimarike.

Bibi May amemwambia Putin kuwa Uingereza iko wazi kwa mahusiano tofauti lakini ili hilo litimie, ni lazima serikali ya Urusi pia ichague njia tofauti. May ameongeza kuwa mahusiano kati ya nchi hizo mbili hayawezi kurejea katika hali ya kawaida hadi Urusi iache matendo yake yasiyofaa ikiwemo, kuingilia masuala ya mataifa mengine, upotoshaji wa habari na udukuzi.

Uhusiano kati ya Urusi na Uingereza uliharibika baada ya Uingereza kuituhumu Urusi kuhusika na mkasa wa shambulizi la sumu dhidi ya jasusi wa zazamni wa Urusi Sergei Skripal na binti yake mwezi machi mwaka uliopita.

Mkutano huo wa kilele utamalizika kesho Jumamosi.

Vyanzo: DPA, AFPE