1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanane wakamatwa Uturuki, mashambulizi ya mwaka mpya

2 Januari 2017

Kituo cha habari nchini Uturuki kimesema polisi nchini humo wamewakamata washukiwa wanane kuhusiana na shambulizi la kigaidi lililotekelezwa na kundi linalojiita dola la Kiislamu mjini Istanbul mkesha wa mwaka mpya. 

https://p.dw.com/p/2V9XL
Türkei Istanbul - Polizei sichert Nachtclub nach Angriff
Picha: Getty Images/AFP/Y. Akgul

Kituo hicho cha habari cha Anadolu kinachomilikiwa na serikali, kilisema kuwa mshambulizi aliyetoroka baada ya kuwafyetulia risasi mamia ya watu waliokuwa wameenda kuhudhuria sherehe za kukaribisha mwaka mpya na kuuwa 39 kati yao hakuwa miongoni mwa wale wanaouzuiliwa. Kundi la dola la Kiislamu lilitoa taarifa inayodai kuwa lilihusika katika shambulizi hilo katika kilabu cha Reina mjini Istanbul.

Kulingana na taarifa hiyo iliyotolewa, shambulizi hilo lilitokana na agizo kutoka kwa kiongozi wa kundi hilo Abu Bakr al- Baghdadi la kuilenga Uturuki. Hata hivyo shirika la habari la dpa halikuweza kubainisha uhalali wa taarifa hiyo lakini inaonekana kuambatana na madai ya awali ya kundi hilo. Polisi bado wanaendelea kumsaka mshambuliaji huyo.

Wengi wa waliofariki ni raia wa kigeni

Ripoti za awali zilikuwa zimesema kuwa huenda kulikuwa na zaidi ya washambuliaji wawili lakini waziri mkuu wa Uturuki Binali Yidirim alizungumzia tu mshambuliaji mmoja. Wengi wa wale waliofariki walikuwa raia wa kigeni, saba kutoka Saudi Arabia, watatu kutoka Lebanon, watatu kutoka Iraq, wawili kutoka kila nchi za Tunisia, Morocco, Jordan na India na mmoja kutoka kila nchini za kuwait, canada, Israeli, Syria na Urusi. Wawili kati ya waliofariki wanaaminika kuwa raia wa Ujerumani.

Türkei Istanbul - Sanitäter transportieren verletzte nach Angriff auf Nachtclub
Majeruhi wa shambulizi dhidi ya kilabu cha Rheina apelekwa katika ambulansiPicha: Reuters/Stringer

Wakati huo huo, shirika la habari la serikali nchini Syria limesema kuwa wanamgambo wa kundi la al-Qaida wameharibu nguzo za umeme karibu na mji mkuu wa nchi hiyo na kusababisha kukatika kwa umeme katika mkoa wa Quneitra kusini mwa Syria. Shirika la habari la Syria SANA,limeripoti kuwa wapiganaji wa kundi la fatah al–sham walizishambulia kwa mabomu nguzo tatu kusini magharibi mwa Damascus na kusababisha kukatika kwa umeme katika eneo la Quneitra.

Mashambulizi zaidi dhidi ya ngome za kundi la dola la kiislamu

Ripoti hizo zinajiri huku mkataba wa kusitisha mashambulizi kati ya Urusi na Uturuki ukidumishwa kwa siku ya nne licha ya kuweko kwa ukiukaji wa hapa na pale. Kundi la wanamgambo la fatah al-Sham pamoja na kundi la dola la Kiislamu hayajajumuishwa katika mkataba huo. 

Hii leo, shirika la habari la Anadolu lilitangaza kuwa zaidi ya ngome 100 za kundi la wanamgambo la dola la Kiislamu zimeshambuliwa na Uturuki na Urusi katika operesheni tofauti.

Shirika hilo limesema kulingana na ofisi ya mkuu wa majeshi nchini Uturuki, ndege za uturuki zililenga maeneo manane yanayothibitiwa na kundi hilo la dola la Kiislamu huku mashambulizi mengine yaliohusisha mizinga mikubwa yakilenga maeneo 103 karibu na Al Bab na kuwauwa wanamgambo 22. Ndege za Urusi pia zilishambulia maeneo yanayothibitiwa na kundi hilo la dola la kiislamu huko Dayr Kak umbali wa kilomita 8 kutoka Kusini Magharibi mwa Al Bab.

Mwandishi: Tatu Karema/ dpae/ ape
Mhariri:Iddi Ssessanga