1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasayansi Tanzania kutafiti virusi vinavyodhuru binadamu

George Njogopa26 Machi 2020

Wanasayansi nchini Tanzania wanasema wanaanzisha utafiti kwa ajili ya kubaini virusi vinavyosababisha madhara kwa binadamu ikiwemo virusi vitokavyo kwa wanyama na kwenda kwa binadamu.

https://p.dw.com/p/3a3hA
Coronavirus in Mali Bamako testlabor
Picha: AFP/M. Cattani

Utafiti huo unaoratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ukiwashirikisha maprofesa kutoka Chuo cha Kilimo (SUA) na Chuo cha Nelson Mandela, pia utagusia maeneo mengine kama yale yanayohusu malaria na magonjwa ya moyo.

Kaimu mkurugenzi wa idara ya utafiti wa Costech, Profesa Mohammed Sheik amesema "tayari kiasi cha dola milioni 200 kimetengwa kwa ajili ya kufanikisha utafiti huo utakaoinufaisha pia kanda ya Afrika."

Wakati wanasayansi hao wakianza kukuna kichwa kubaini hali ya virusi vinavyosababisha madhara kwa binadamu, Tanzania imethibitisha mtu wa pili aliyeambukiziwa virusi vya Corona visiwani Zanzibar, na kufanya idadi ya watu walioambukizwa nchini kufikia 13.

Coronavirus- COVID-19 - Mikrografie
Utafiti wa Tanzania utalenga kubaini virusi vinavyosababisha madhara kwa wanadamu, ikiwemo vinavyotokana na wanyama.Picha: Imago/NIAID

Mgonjwa huyo mwanamke ni raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 29, mke wa raia wa Ghana, ambaye alithibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona wiki iliyopita. Watu hao wawili wametengwa kwa uchunguzi wa kiafya na kupewa matibabu, ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

Mbowe ajiweka karantini

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa chadema na kiongozi rasmi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe ameamua kujiweka karantini pamoja na familia yake baada ya mtoto wake kujikuta ameambukizwa virusi vya corona.

Serikali imeendelea kuwarai wananchi kuchukua tahadhari juu ya janga hilo huku ikipokea msaada wa vifaa vya matibabu kwa ajili ya kukabiliana na virusi hivyo kutoka kwa mfuko wa Jack Ma na mfuko wa Alibaba wa China.

Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Muhammad Bakari Kambi amesema mchango huo umekuja wakati muafaka wakati Tanzania ikiwa imeimarisha mikakati ya kukabiliana na janga hilo ambalo lilipiga hodi kwa mara ya kwanza nchini Machi 16.

Waziri wa afya Ummy Mwalimu alisema Alhamisi kuwa mgonjwa wa kwanza aliyekutwa na maambukizi hayo ya Covid-19 amethibitika kupona baada ya vipimo kuonyesha kuwa hana tena maambukizi hayo.