1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake wamebaki wamekwama katika biashara ndogo ndogo, Afrika mashariki.

Sekione Kitojo29 Septemba 2007

Nchini Malawi kiasi cha zaidi ya robo ya masuala yote ya nyumbani yanaongozwa na wanawake. Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi na kiasi cha asilimia 80 ya Wamalawi wanategemea moja kwa moja sekta hii. Kukiwa na wastani wa watoto sita kwa kila kaya, wanawake wengi hufanya biashara ndogo ndogo ili kuongeza kipato kitokanacho na kilimo.

https://p.dw.com/p/CH7U

Wakati biashara inazidi kuwa ya kisasa zaidi na ikisambaa duniani kote, wanawake wafanyabishara wadogo nchini Malawi wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kwenda na wakati na mabadiliko, hususan kwasababu watu wazima wanaojua kusoma na kuandika ni asilimia 44 tu. Kiasi cha asilimia 77 ya wanaume wanajua kusoma na kuandika.

Ni asilimia tano tu ya wanawake wa Malawi , zambia , Zimbabwe, Swaziland, Namibia na jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo wanatambua nafasi zilizopo za masoko katika eneo hilo, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kwa niaba ya umoja wa soko la pamoja la mataifa ya Afrika mashariki na kati COMESA.

Matokeo ya utafiti huo pia yanaonyesha kuwa wanawake wafanyabiashara katika eneo la COMESA wanakabiliwa na changamoto za aina moja kuhusiana na uwezo wao wa kupenya katika soko la nje. Ugunduzi huu ni wito wa uamsho kwa wanawake katika eneo hilo, kwa mujibu wa Mary Malunga , mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya kitaifa vya wanawake wafanyabiashara katika eneo la COMESA (FEMCOM.)

Pia anaongoza chama wa wafanyabiashara wanawake nchini Malawi NABW. FEMCOM kimekuwa kikifanyakazi kuelekea kutangaza mipango ambayo inawaunganisha wanawake katika biashara na maendeleo tangu mwezi Julai 1993. Hivi sasa chama hicho kimejikita katika mpango wa kujenga welewa wa masoko ya nje miongoni mwa wanawake katika eneo la biashara huria katika eneo la COMESA , FTA. Kundi la FTA linajumuisha nchi za Djibouti , Misr, Zimbabwe , Zambia, Madagascar, Sudan, Mauritius , Malawi na Kenya. Tunataka kujenga uwezo wa wanachama wa FEMCOM katika biashara na utawala wa biashara ya nje ili kwamba wanawake katika eneo hilo wataweza kushindana kwa kiwango kizuri katika masoko ya eneo hilo na duniani kote.

Sekta ambazo FEMCOM zinalenga zaidi ni pamoja na kilimo, uvuvi, madini, nishati, usafiri na mawasiliano. Shirika hilo pia linaangalia mali asili kwa lengo la kuimarisha hali ya kiuchumi ya wanawake. COMESA ina sera ya jinsia ambayo inatamka wazi umuhimu wa jukumu la mwanamke katika shughuli za eneo hilo.

Licha ya kuwa na sera hiyo pamoja na mtazamo wenye kutukuka pamoja na malengo ya COMESA, anasema Malunga , kutokuwa na usawa katika jinsia bado ni kikwazo kikubwa kinachoathiri juhudi za ujumuisho katika eneo hilo. Wanawake hususan wanaonekana kuwa na nafasi finyu katika masoko ya kimkoa na kimataifa. Lakini sababu zinazosababisha hali hiyo bado hazijaainishwa kikamilifu, anadokeza Malunga.

Welewa wa utawala wa biashara wa umoja wa COMESA miongoni mwa wafanyabiashara wanawake nchini Malawi umegundulika kuwa mdogo sana. Hali na kiwango cha ushiriki wa wafanyabiashara wanawake nchini Malawi katika biashara katika eneo la COMESA ni kwa kutumia tu biashara isiyo rasmi katika mipaka.