1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto ndiyo waathiriwa wakubwa katika vita vya Syria

13 Juni 2013

Watoto wanalengwa katika vita vya hila nchini Syria na hutumika kama ngao na wapiganaji. Ripoti iliyotolewa hivi punde na Umoja wa Mataifa inaelezea masaibu ya kusikitisha na kugutusha yanayowakumba watoto wa Syria.

https://p.dw.com/p/18odY
Picha: Moritz Wohlrab, Aktion Deutschland hilft

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon amesema kwenye ripoti hiyo kuwa vita hivyo vinawaathiri watoto katika kiwango alichokiita cha 'kutokubalika wala kuvumilika' huku wengi wao wakiwa miongoni mwa maelfu ya waliouawa tangu vita hivyo vianze miezi 26 iliyopita.

Muwakilishi maalum wa Umoja huo kuhusu watoto katika maeneo ya mizozo, Leila Zerrougui, amesema afisi yake imepokea ripoti za kuaminika kuwa watoto nchini Syria wanauawa au kujeruhiwa katika miripuko ya mabomu yanayofyetuliwa kiholela, wanalengwa na askari doria na wanatumika kama ngao na wapiganaji.

Zerrougui amewasilisha ripoti hiyo ambayo inasema watoto wa kiume wengine wadogo wa hata miaka kumi wanatumika na makundi ya wapiganaji kama wapiganaji au wasafirishaji silaha.

Mtoto kutoka Syria anayeteseka
Mtoto kutoka Syria anayetesekaPicha: picture-alliance/dpa

Kumeripotiwa kuwa kundi kuu la wapiganaji la waasi lijulikanalo kama Free Syrian linawasajili watoto, wengi wao wa kati ya umri wa miaka 15 na 17. Visa vya ghasia za kingono vimeripotiwa kutumika na wanajeshi wa utawala wa Rais wa Syria, Bashar al Assad dhidi ya watoto hao wa kiume ili kuwashurutisha kutoa taarifa wanazohitaji.

Watoto wanateswa na pande zote

Ripoti hiyo inaeleza kuwa watoto wa umri mdogo wanateswa kama watu wazima yakiwemo mateso ya kutumia umeme, vipigo, kuwekwa katika hali ya kuchusha, vitisho na kudhalilishwa kingono huku maelfu wao wakitizama jamaa zao wakiuawa au kujeruhiwa.

Zerrougui amesema kila mmoja anayehusika kwa njia moja au nyingine katika mzozo huo wa Syria, anapaswa kuchukua hatua za dharura kuwalinda watoto na kuongeza kuwa kuruhusu mahitaji ya kimsingi kuwafikia ni jambo muhimu kwani watoto hawastahili kuendelea kufa kwa sababu hawawezi kupata huduma za madaktari au mahitaji ya kimsingi.

Ripoti hiyo pia imeirodhesha Mali miongoni mwa nchi ambazo zinawatumikisha watoto kama wapiganaji wa kivita. Waasi wa Tuareg, wapiganaji wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali, wamewatumia mamia ya watoto kama wapiganaji nchini Mali.

Wapiganaji watoto
Wapiganaji watotoPicha: Getty Images

Watoto wa kike hatarini zaidi

Zerrougui amewaambia waandishi wa habari kuwa watoto ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini Mali ambayo ina takriban watu milioni 15.8 wametekwa nyara na makundi ya wapiganaji na watoto wa kike wamelazimishwa kuwa wake wa wapiganaji hao.

Tangu kuzuka kwa maasi mwezi Machi mwaka jana kumeripotiwa visa chungu nzima vya watoto wa kike kubakwa wengine na magenge, kutumikishwa kingono na kulazimishwa kuolewa na wapiganaji wa makundi mbali mbali.

Chad, Jamhuri ya Afrika ya kati, Somalia, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Sudan kusini, Myanamar, Afghanistan na Ufilipino pia zimetajwa katika ripoti hiyo. Hata hivyo Nepal na Sri Lanka zimeondolewa kutoka orodha hiyo ya fedheha ya Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Caro Robi/afp

Mhariri: Josephat Charo