1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa aaga dunia

Amina Mjahid
10 Februari 2024

Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania Edward Lowasa amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu. Lowassa amefariki dunia katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko jijini Dar es salaam.

https://p.dw.com/p/4cFub
Tanzania
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Edward Lowassa Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Katika tangazo lake fupi, Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango, amesema Lowassa ameiaga dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo hicho akimwelezea kiongozi huyo kuwa ni miongoni mwa watu wa kukumbukwa nchini Tanzania huku akitangaza siku tano za mamombolezo.

Edward Lowassa arejea CCM

Lowassa anatazamwa na wengi kama miongoni mwa viongoni wa kupigiwa mfano kutokana na misimamo yake huku akionyesha ukosoaji mkubwa ndani ya chama chake CCM katika baadhi ya mambo alionyesha kutokubaliana nayo.

Akimzungumzia mwanasisa huyo, mkurugenzi wa itikadi, uenezi na mambo ya nje wa chama kikuu cha upinzani Chadema, John Mrema amesema Lowassa alikuwa mwanasiasa wa aina yake.

Amesema anamkumbuka mwanasiasa huyo kama mtu hodori na shupavu ambaye daima alipenda kusimama katika kile alichokiamini.