1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi ajiuzulu baada ya serikali kulaumiwa, Korea kusini.

25 Novemba 2010

Wanajeshi wa Korea kusini wataanza mazoezi ya kijeshi mwishoni mwa juma.

https://p.dw.com/p/QIGr
Mwanajeshi wa Korea kusini aonesha mabaki ya kombora lililovurumishwa kutoka kaskazini.Picha: AP

Waziri huyo wa ulinzi, Kim Tae-Young amejiuzulu baada ya wabunge kuikashifu serikali kwa kutochukua hatua za haraka baada ya mashambulio ya makombora ya Korea ya Kaskazini.

Rais Myung bak amekubali kujiuzulu kwa waziri huyo wa ulinzi ili aweze kutuliza hali na kurejesha heshima ya jeshi la taifa hilo.

Jeshi la Korea kusini limesema linaamini lilisababisha uharibifu mkubwa wakati lilipojibu mashambulio ya makombora ya Korea kaskazini.

Hatua hiyo inajiri baada ya serikali kulaumiwa vikali na wabunge kwa kutochukua hatua za haraka kukabiliana na Korea kaskazini.

Wanajeshi katika kisiwa kilichoshambuliwa cha Yeonpyeong, wamejitetea wakisema walivurumisha makombora 80 na wanaamini yalisababisha uharibifu mkubwa upande wa Korea Kaskazini.

Luteni kanali, Ju Jong-Wha wa jeshi hilo amekanusha kuwa walichukua muda mrefu kabla ya kuishambulia Korea kaskazini.

Korea Kaskazini iliyotengwa na jumuiya ya Kimataifa imetoa taarifa ikiinyoshea kidole cha lawama Marekani kwamba haiwezi kuepuka dhamana ya kuhusika na mashambulio ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo vya watu wanne wakati jeshi la Pyongyang lilipovurumisha mabomu katika eneo ambako kuna bahari hiyo inayozozaniwa.

Utawala huo wa Kaskazini pia hakuacha kuitupia maneno jirani yake Korea Kusini.Imeionya nchi hiyo inayoiita kibaraka wa Marekani itafakari tabia yake la sivyo itajikuta ikishambuliwa tena na tena bila ya uoga.

Aidha taarifa iliyotolewa leo na Korea Kusini inaeleza kwamba nchi hiyo inapanga kuongeza kwa kiasi kikubwa wanajeshi wake ikiwa ni pamoja na jeshi al nchi kavu katika visiwa vyake vitano vilivyoko kwenye eneo la bahari hiyo ya Yellow Sea.Juu ya hayo Kusini pia imesema imeshaongeza kiwango cha bajeti yake kuelekea mpango wa kuvishughulikia vitisho vya mara kwa mara vya Korea Kaskazini.

Tayari Korea Kusini imeshaimarisha idadi ya wanajeshi wake katika bahari hiyo.China inayoonekana kuwa mshirika mkubwa wa Korea Kaskazini imesema kwamba inapinga uchokozi wa kijeshi katika rasi ya Korea na kuzitolea mwito pande zote mbili kuvumiliana.

Rais Wen Jiabao amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba katika hali iliyojitokeza sasa katika eneo hilo,ni vyema kwa pande zote husika kujizuia kufanya vitendo vya uchokozi na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zaidi kutuliza mvutano huo.

Matamshi hayo ya Wen Jiabao ndio taarifa ya kwanza kutoka China tangu Korea Kaskazini iliposhambulia kisiwa cha Korea Kusini na kuua wanajeshi wawili na raia wawili huku watu wengine 18 wakiwa wamejeruhiwa na wengi kuyakimbia makaazi yao hapo jumanne.

China imetolewa mwito na Marekani pamoja na washirika wake katika eneo hilo kusaidia kuikanya Korea Kaskazini na pia kuishawishi irudi haraka katika mazungumzo ya Nuklia ya Pande sita yaliyokwama.

Mwandishi, Saumu Mwasimba, Peter Moss

Mhariri.Aboubakary Liongo