1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Tanzania kuomba kujiunga na mpango wa COVAX

Josephat Charo
17 Juni 2021

Shirika la afya duniani WHO limesema Tanzania ina matumaini ya kujiunga na mpango wa kimataifa wa ugawaji chanjo kwa nchi masikini wa COVAX.

https://p.dw.com/p/3v72x
WHO - Ebola-Lage im Kongo | Matshidiso Moeti
Mkurugenzi wa shirika la WHO barani Afrika, Matshidiso MoetiPicha: picture-alliance/dpa/KEYSTONE/S. Di Nolfi

Afisa wa WHO amesema chanjo huenda zikawasili Tanzania katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Tangu aliposhika hatamu za uongozi mwezi Machi, rais wa sasa Samia Suluhu Hassan amechukua hatua za kuifanya Tanzania iendane na viwango vya kimataifa vya afya katika ufuatiliaji wa ugonjwa wa COVID-19.

Kwa mujibu wa kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika, nchi hiyo yenye wakazi milioni 58 ni mojawapo ya matiafa manne ya Afrika ambayo hayajaanza kampeni ya utoaji chanjo dhidi ya corona.

Mkurugenzi wa shirika la WHO barani Afrika, Matshidiso Moeti, ameuambia mkutano na waandishi habari kwamba wamepokea taarifa kuwa Tanzania sasa rasmi inachukua hatua kujiungan a mpango wa COVAX.

Richard Mihigo wa mpango wa utoaji na kuendeleza chanjo barani Afrika amesema Tanzania tayari imeshachukua hatua za awali kuwasilisha fomu ya kuomba chanjo kupitia mpango wa COVAX na kuanza kuandaa mpango wa kupeleka chanjo. Mihigo ameuambia mkutano wa waandishi habari kwamba wanatarajia chanjo hizo zitawasili Tanzania wiki chache zijazo.

Maafisa wa Tanzania hawakupatikana kutoa kauli kuhusu suala hili.

Uganda Unterschrift EACOP in Kampala
Rais Samia Suluhu Hassan wa TanzaniaPicha: Presidential Press Unit/Uganda

Katika ishara nyingine ya meueleko mpya wa nchi hiyo, waziri wa fedha Mwigulu Nchemba alisema wiki iliyopita kwamba serikali ilikuwa imeliomba shirika la fedha la kimataifa IMF mkopo wa dola milioni 571 kusaidia kukabiliana na changamoto zinazotokana na janga la corona.

IMF ilisema Tanzania itatakiwa kutoa data za maambukizi ya corona kama sehemu ya mazungumzo juu ya mkopo huo. Tanzania iliacha kutoa taarifa kuhusu visa vya maambukizi ya COVID-19 na vifo mnamo mwezi Mei mwaka uliopita na licha ya mageuzi mengine ya kisera yanayofanywa na rais wa sasa, nchi hiyo haijaanza tena kutangaza hadharani data hizo.

Mkurugenzi wa shirika la WHO barani Afrika, Matshidiso Moeti amesema wanaihimiza Tanzania kuwapa taarifa za corona ili waweze kuchukua hatua madhubuti kabisa katika kutoa msaada, kwa kuwa sasa nchi hiyo inapania kulikabili janga hilo kupitia chanjo. Meoti aidha amesema kupanga, wapi kwa kuanzia, wapi kwa kulenga, yote haya ni masuala yanayoweza kubainishwa kwa misingi ya ushahidi uliopo.

Maambukizi yaongezeka barani Afrika

Sambamba na hayo Moeti amesema visa vya COVID-19 viliongeuza kwa zaidi ya asilimia 20 wiki baada ya nyingine katika nchi takriban 24 za Afrika na ufanisi wa kuwadunga chanjo waafrika unaendelea kwa mwendo wa kinyonga, huku asilimia 0.79 ya watu wakiwa wamechanjwa barani humo.

Moeti amesema Afrika inajikuta katikati mwa wimbi la tatu la corona na wameshashuhudia nchini India na kwingineko jinsi ugonjwa wa COVID-19 unavyoweza kurejea kwa kasi na kuilemea mifumo ya afya.

Visa vipya vya maambukizi vimeongezeka hadi takriban asilimia 30 katika kipindi cha wiki moja iliyopita na vifo vimepanda kwa asilimia 15, huku mataifa matano yakiwakilisha asilimia 76 ya visa vipya vya maambukizi, yakiwemo Afrika Kusini, Tunisia, Zambia, Uganda na Namibia.

(reuters)