1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen shabaha ya kushambuliwa na jukwaa la kushambulia kwa Al Qaeda

Mohmed Dahman23 Septemba 2008

Kuanzia mashambulizi dhidi ya meli za mataifa ya magharibi hadi kuripuliwa kwa hivi karibuni kwa ubalozi wa Marekani Yemen sio nchi ngeni kwa kundi la Al Qaeda.

https://p.dw.com/p/FNCb
Ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Yemen Sanaa baada ya kushambuliwa hivi karibuni.Picha: AP

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema thamani halisi ya nchi hiyo kwa mtandao wa kundi hilo inaweza kuwa ni mahala kwa wanachama wa kundi hilo kujikusanya upya na kujiandaa kufanya mashambulizi mahala kwengineko.

Yemen kama nchi inayoangaliwa kuwa shababa inayolengwa kwa mashambulizi na jukwaa la kuandaa mashambulizi kwa ajili ya kundi la Al Qaeda.

Watu 17 waliuwawa wiki iliopita kutokana na miripuko miwili ya kujitolea muhanga maisha kwa mabomu yaliotegwa kwenye magari kwenye eneo la ubalozi wa Marekani ambalo ni shambulio kubwa kabisa kufanyika nchini Yemen tokea kuripuliwa kwa meli ya mafuta ya Ufaransa Limburg.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema mbinu ya hali ya juu kabisa iliotumika katika shambulio hilo ambapo kwayo washambuliaji walijigeuza kwa kuvaa sare na kutumia magari ya kijeshi kunaonyesha Al Qaeda inaimarika upya katika nchi ambayo haina rasilmali za kutokomeza wanamgambo kwa kulinganisha na mashambulizi yanayozidi kuongezeka sehemu nyengine za eneo hilo linalozalisha mafuta kwa wingi kabisa duniani.

Mchambuzi alieko Dubai Umoja wa Falme za Kiarabu Mustafa Alani anasema hakuna mtu anayepaswa kukaa kitako tu na kuangalia kile kinachotokea nchini Yemen na anafikiri watakuja kushuhudia operesheni za hali ya juu kabisa na uwezekano wa operesheni hizo kuvuka kwa kuingia mataifa ya Ghuba.

Kwa maoni yake watakuja kushuhudia mahusiano zaidi kati ya kundi hilo la Yemen na wale walioko Pakistan au Afghanistan na kwamba Al Qaeda imeathirika vibaya sana nchini Iraq lakini kwa kulikandamiza kundi hilo katika nchi moja huwa linaibuka mahala kwengine.

Ikiwa katika njia muhimu za kupita meli na jirani ya Saudi Arabia nchi inayozalisha mafuta kwa wingi kabisa duniani Yemen inakabiliwa na matatizo mengi uasi huko kaskazini,hali ya kutoridhika ilioko kusini mwa nchi hiyo na miminiko wa wakimbizi wa Somali mambo ambayo huashiria hatari kupindukia mipaka yake.

Serikali ya Yemen ilijiunga na vita vilivyoongozwa na Marekani dhidi ya ugaidi kufuatia mashambulizi ya Septemba 11 dhidi ya miji ya Marekani hapo mwaka 2001.Tokea wakati huo imewafunga gerezani au kuwauwa madarzeni ya watuhumiwa wanamgambo wa Kiislam lakini kutokana na nchi hiyo kuwa ya milima na ya kikabila ambapo udhibiti wa serikali una kikomo inaendelea kuwa ya kuvutia kwa makundi yaliopigwa marufuku.

Umaskini uliokithiri elimu duni kukiandamana na idadi ya watu walio vijana inayozidi kuongezeka kunaipa Al Qaeda chanzo cha wazi cha kuwaandikisha wanamgambo.

Baadhi ya masheik wa itikadi kali wako karibu au wanavumiliwa na serikali ya Yemen kwa kule kuendelea kwa nchi hiyo kuwa ya uhafidhina mkubwa wa Kiislam.

Hivi karibuni serikali ya Yemen imesema imewakamata watuhumiwa 30 wa Al Qaeda kwa kuwahoji juu ya shambulio la ubalozi wa Marekani.Wengine wengi wamekuwa wakizidi kushikiliwa tokea wakati huo.

Nicole Stracke mchambuzi katika Kituo cha Utafiti cha Ghuba kilioko Dubai anasema shambulio hilo hivi sasa ni jibu kwa mkakati wa kupambana na ugaidi wa serikali kwa sababu katika miezi ya hivi karibuni serikali imewakamata au kuwauwa wengi wa wanaharakati hao.

Kwa kadri Yemen itakavyokosa utulivu ndivyo itakavyozidi kuwavutia wanamgambo ambao Marekani inataka kuwadhibiti.

Wachambuzi wanasema Al Qaeda nchini Yemen wamekuwa wakizidi kuwategemea matajiri wanaowapendelea wa Saudi Arabia kwa ajili ya fedha na msaada kutokana na serikali ya Saudi Arabia kuweza kuzuwiya mashambulizi nchini humo.