1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Zaidi ya watu 100 wauwawa katika milipuko Iran

3 Januari 2024

Takriban watu 103 wameuwawa na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa nchini Iran, baada ya mabomu mawili kulipuka mbele ya umati wa watu waliojitokeza katika kumbukumbu ya Jenerali Qasem Soleiman alieuwawa na Marekani.

https://p.dw.com/p/4aplZ
Kerman, Iran  |  Majeruhi wakiingizwa katika gari la wagonjwa.
Waathirika wa mlipuko wakiingizwa kwenye gari la wagonjwa, baada ya milipuko ya mabomu kutokea kwenye kumbukumbu ya mika minne tangu kifo cha Qasem Soleiman.Picha: Mahdi K. Ravari/Mehr News/AP/dpa/picture alliance

Milipuko huyo ambayo imetajwa na televisheni ya taifa Iran kama shambulio la kigaidi, imetokea wakati hali ya wasiwasi ikitanda katika eneo la mashariki ya kati, ikiwa ni siku moja baada ya kuuwa kwa afisa wa ngazi za juu wa kundi la Hamas Saleh al-Arurikatika shambulio la droni ambayo Lebanon imeinyooshea kidole Israel.

Milipuko hiyo ilitokea karibu na msikiti wa Saheb al-Zaman uliopo katika eneo la Kerman kusini mwa mji alikozikwa Soleimani, wakati wafuasi wake walipokusanyika katika kumbukumbu ya miaka minne ya kifo chake kilichotokana na mashambulizi ya droni ya Marekani nje kidogo ya uwanja wa ndege wa Baghdad.

Naibu Gavana katika mji wa Kerman ametaja milipuko hiyo iliyouwa watu zaidi ya 100 na kujeruhi wengine zaidi 140 kuwa ni shambulio la "kigaidi." Aliongeza kuwa mabomu hayo yalilipuka kwa kupishana kwa dakika kumi.

Shirika la habari la Tasnim la Iran, likinukuu vyanzo vya habari, limesema mifuko miwili iliokuwa na mabomu ililipuka kwenye eneo hilo na kuongeza kuwa wahusika wa milipuko hiyo walitumia rimoti katika kuyaongoza.

Soma pia:Marekani yamuua kamanda wa juu wa Iran

Mkuu wa kikosi cha uokoaji Kerman Reza Fallah amesema hali bado si shwarikatika eneo hilo kwa sasa kuwafikia majeruhi kutokana na njia kutopitika kutokana na umati wa watu.

"Kwa sasa tunawahamisha majeruhi katika eneo hilo. Umati ni mkubwa na kazi ni ngumu sana njia zote za kuelekea katika eneo la tukio hazipitiki." Alisema Fallah.

Video zilizochapichwa katika mitandao ya kijamii zinaonesha umati wa watu wakihangaika kukimbia huku na kule wakilizunguka eneo la kaburi kwa ajili ya usalama, huku wafanyakazi wa kikosi cha uokoaji na magari ya kubebea wagonjwa yakiwa katika eneo hilo kwa ajili ya uokoaji.

Hadi sasa hakuna upande ambao umedai kuhusika na shambulio hilo la Kerman.

Soleiman ni nani katika siasa za Mashariki ya Kati?

Soleiman aliongoza Kikosi cha Quds, kitengo cha operesheni za kigeni cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kinachosimamia operesheni za kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Marekani yamuua afisa mwandamizi wa Iran

Kiongozi Mkuu waIran Ayatollah Ali Khamenei alimtaja Soleiman kama "shahid alie hai" enzi za uhai wake na alijulikana kama shujaa kwa kulishinda kundi la dola la kiislam nchini Syria na Iraq.

Mbele ya Wairani wengi, uwezo wake wa kijeshi na kimkakati ulikuwa muhimu katika kuzuia mgawanyiko wa makabila mbalimbali ya nchi jirani kama vile Afghanistan, Syria na Iraq.

Soma pia:Iran yasema bado ina nia ya kumuua Donald Trump

Kwa muda mrefu alionekana kama hasimu wa Marekani na washirika wake, huku katika uwanja wa nyumbani, Soleimani alikuwa mmoja wa viongozi muhimu katika eneo la kikanda, akiepenyeza ajenda ya kisiasa na kijeshi ya Iran nchini Syria, Iraq na Yemen.

Siku chache baada ya kifo chake mnamo 2020, mamilioni ya watu walijitokeza baada ya kifo chake wakionesha kile walichokitaja ni umoja wa kitaifa ambapo mkanyagano uliotokea na watu takriban 56 waliuwawa na wengine zaidi ya 200 walijeruhiwa.

Utafiti uliofanya mwaka 2018 na Iran Poll na chuo Kikuu cha Maryland ulibaini kuwa Soleiman alikuwa na umaarufu wa asilimia 83 nchini Iran, akimzidi rais wa wakati huo Hassan Rouhani na waziri wa mambo ya nje wa wakati huo Mohammad Javad Zarif.