1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la kuhesabu kura laendelea Tanzania

Kabogo Grace Patricia1 Novemba 2010

Kura hizo zinahesabiwa baada ya wananchi wa Tanzania hapo jana kupiga kura za kumchagua rais, wabunge na madiwani, uchaguzi ulioelezwa kufanyika katika hali ya utulivu.

https://p.dw.com/p/PvFp
Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi mkuu uliofanyika jana nchini Tanzania.Picha: EUEOM

Zoezi la kuhesabu kura nchini Tanzania linaendelea, katika uchaguzi mkuu ambao rais aliyeko madarakani Jakaya Kikwete anagombea muhula wa pili wa miaka mingine mitano. Waangalizi wa kimataifa wamesema kuwa zoezi la kupiga kura lilifanyika kama ilivyopangwa.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi huo, mwangalizi wa Umoja wa Afrika, Yvonne Kilonzo alisema, ''uchaguzi umefanyika kwa amani na hakukuwa na vitisho wala matukio ambayo yangeweza kumfanya mtu kuwa na wasiwasi na kwamba kila kitu kimekwenda vizuri.''

Hata hivyo, kulikuwa na taarifa za wapiga kura kutoyaona majina yao katika daftari la wapiga kura, pamoja na kukosekana kwa vifaa vya kupigia kura. Kwenye vituo vichache kati ya vituo 52,000 vya kupigia kura muda wa kupiga kura uliongezwa kidogo.

Katika uchaguzi huo, Rais Kikwete anapata upinzani mkubwa kutoka kwa Dr. Wilbrod Slaa wa chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema na Ibrahim Lipumba wa chama cha Wananchi-CUF.

Aidha, imeelezwa kuwa kampeni za uchaguzi huo mkuu zilikuwa motomoto katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki yenye idadi kubwa ya watu wapatao milioni 41, inayolima kwa wingi kahawa na kuchimba madini ya dhahabu na ambayo inatembelewa na watalii kwa wingi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,AFPE)

Mhariri: Sekione Kitojo