1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Edward Lowassa afariki dunia

10 Februari 2024

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Edward Lowassa afariki dunia. Kwa muda mrefu alikuwa akitibiwa nchini Afrika Kusini, amefariki dunia Jumamosi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko jijini Dar es salaam.

https://p.dw.com/p/4cFt7
Tanzania - Mwanasiasa Edward Lowassa
Aliyekuwa Waziri Mkuu nchini Tanzania Edward Lowassa akiwasalimu wafuasi wake katika kampeni ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2015: Dar Es Salaam:01.10.2015Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Katika tangazo lake fupi, Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango, amesema Lowassa ameiaga dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Jakaya Kikwete.

"Amefariki dunia  leo wakati akipatiwa matibabu kwa ugonjwa wa kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu. Lowassa ameugua kwa muda mrefu  na amekuwa akipatiwa matibabu,” alisema makamu huyo wa rais.

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo hicho akimwelezea kiongozi huyo kuwa ni miongoni mwa watu wa kukumbukwa nchini Tanzania huku akitangaza siku tano za maombolezo.

 "Tumempoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu..." ameandika Rais Samia katika ukurasa wake wa X.

Tanzania -  Magufuli akisalimiana na Lowassa
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Edward Lowassa (kulia) akisalimiana na Aliyekuwa Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli. Kwa sasa wote ni marehemu.Picha: DW/S. Khamis

Lowassa anatazamwa na wengi kama miongoni mwa viongoni wa kupigiwa mfano kutokana na misimamo yake huku akionyesha ukosoaji mkubwa ndani ya chama chake CCM katika baadhi ya mambo alionyesha kutokubaliana nayo.

Soma pia:Edward Lowassa arejea CCM 

Ni mmoja wa wanasiasa watakaoendelea kukumbukwa katika siasa za Tanzania, hasa alipochaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa kumi wa Tanzania mnamo Desemba 30, mwaka 2005 huku akiweka rekodi ya kuwa Waziri mkuu aliyedumu kwa muda mfupi katika nafasi hiyo na akajiuzulu  Februari 7, 2008 akihusishwa katika kashfa ya Richmond.

Lowassa atakumbukwa daima

Tanzania- Mwanasiasa Edward Lowassa
Aliyekuwa Waziri Mkuu nchini Tanzania Edward Lowassa aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Alikuwa waziri mkuu kati ya mwaka 2005 hadi 2008 chini ya uongozi wa rais Jakaya Kikwete. Alizaliwa Agosti 26, 1953 na wakati wa uhai wake alikuwa  mbunge wa Jimbo la Monduli mkoani Arusha kwa tiketi ya CCM.

Alikuwa mwanasiasa aliyekubalika na kupendwa wa wengi na baadhi walimtazama kama kiongozi ambaye angeliweza kupeperusha bendera ya chama chake katika uchaguzi wa mwaka 2015.  Hata hivyo, chama chake kilimtupa mkono hatua ambayo ilimfanya kujiunga na chama cha upinzani Chadema na kuleta ushindani mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Soma pia: Lipumba asema Lowasa aliingia upinzani kwa lengo la kusaka urais

Akimzungumzia mwanasisa huyo, mkurugenzi wa itikadi, uenezi na mambo ya nje wa chama kikuu cha upinzani Chadema, John Mrema amesema Lowassa alikuwa mwanasiasa wa aina yake.  Amesema anamkumbuka mwanasiasa huyo kama mtu hodori na shupavu ambaye daima alipenda kusimama katika kile alichokiamini.

Anasema anakumbuka namna alivyozunguka naye katika maeneo mbalimbali ya nchi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambapo kupitia kampeni hizo alipata fursa ya kumfahamu vyema mwanasisa huyo.

"Kusema kweli alikuwa kiongozi mwenye misimamo..hakujali lile lilipo mbele yake..nitaendelea kumkumbuka kwa mengi Lowassa, " alisema Mrema.