1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi Nikki Haley aondolewa haraka kuwaepuka waandamanaji

Zainab Aziz
26 Oktoba 2017

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley jana aliondolewa kwa haraka kutoka kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa ya Sudan Kusini katika mji wa Juba wakati kundi la waandamanji lilipojitokeza.

https://p.dw.com/p/2mWM7
Südsudan - Referendum 2011 - Fahne
Picha: picture alliance/dpa/M. Messara

Bi Nikki Haley afisa wa cheo cha juu zaidi katika utawala wa rais wa Marekani Donald Trump kuizuru Afrika, alikuwa nchini Sudan Kusini kwa ajili ya kukutana na raia walioathiriwa na vita vya karibu miaka minne. Baada ya mtafaruku huo kutokea walinzi wa usalama waliamua mara moja kuwa eneo hilo halikuwa salama tena kwa balozi huyo pamoja na ujumbe wake na hivyo wakalazimika kukatisha ziara hiyo baada ya muda mfupi tu.

Balozi huyo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na ujumbe wake waliwasili jana jioni mjini Kinshasa katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchi ambayo inakumbwa na mgogoro wa kisiasa na wa kibinadamu. Waziri wa mambo ya nje wa Kongo Leonard She Okitundu alithibitisha kuwasili kwa Haley katika mazungumzo na shirika la habari la Ufaransa AFP. Haley anatarajiwa kuwepo nchini Kongo hadi kesho Ijumaa ikiwa ndio utakuwa mwisho wa ziara yake katika bara la Afrika. Awali alizitembelea nchi za Ethiopia na hapo jana Sudan ya Kusini ambayo pia inakabiliwa na kuongezeka kwa machafuko katika siku za hivi karibuni.

USA Nikki Haley in New York
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki HaleyPicha: picture-alliance/Kyodo

Bi Haley alimweleza rais wa Sudan Kusini Salva Kiir walipokutana kwamba Marekani imefadhaishwa na hali ya Sudan Kusini baada ya nchi yake kuwekeza takriban Dola bilioni 11chini ya utawala wa Salva Kiir. Haley alisema wamesikitishwa na kile wanachokiona ni kinyume kabisa na kile walichofikiri wanawekeza nchini Sudan Kusini kwa ajili ya uhuru na haki ya jamii watakaoishi kwenye mazingira salama lakini ni tofauti kabisa. Hata hivyo balozi Nikki Haley amesema watajitahidi kuhakikisha amani na usalama vinakuwa ni mambo ya kudumu katika Sudan Kusini.

Serikali ya Sudan yasema nini?  

Upande wa serikali ya rais wa Sudan Kusini Salva Kiir haukutoa maelezo yoyote baada ya mkutano huo. Haley alisema mwezi uliopita kwamba anataka kuokoa makubaliano ya amani ya mwaka 2015 yaliyosambaratika mnamo mwezi Julai mwaka jana, wakati ambapo wapatanishi wa kanda hiyo wamezindua jitihada mpya za kuyafufua makubaliano hayo.

Sudan Kusini ilipata uhuru wake mnamo mwaka 2011 kwa msaada mkubwa kutoka Marekani. Mgogoro huu ulianza mwezi Desemba mwaka 2013 wakati rais Salva Kiir alipomtuhumu naibu wake wa zamani, Riek Machar, kwa kupanga mipango ya kuipindua serikali yake. Mwanzoni, kabila la Dinka, anakotokea Kiir walianzisha chuki dhidi ya watu wa kabila la Nuer, la Riek Machar, vita hivyo sasa vimesababisha kujipenyeza kwa makundi tofauti yenye maslahi tofauti.

Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hali hii ya machafuko katika baadhi ya nchi za Afrika inaikumba pia Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako machafuko yameongezeka zaidi licha ya kuwepo askari wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani wapatao elfu 18.  Hii ni ziara ya kwanza ya bibi Nikki Haley barani Afrika. Leo anatarajiwa kuzuru eneo la Kaskazini la Kivu kabla ya kurejea mjini Kinshasa kwa ajili ya kukutana na rais Joseph Kabila, upande wa upinzani na makundi ya kiraia.  Haley anatarajiwa kumshinikiza rais Kabila ili akubaliane na ratiba ya uchaguzi.  Ziara ya balozi huyo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa inafanyika wakati nchi hiyo ya Afrika ya Kati yenye utajiri mkubwa wa madini ikikabiliwa na mizozo ya kisiasa, kibinadamu na hali mbaya ya usalama.

DR Kongo Kinshasa Präsident Kabila
Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph KabilaPicha: Imago/Xinhua

Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitarajiwa kufanya uchaguzi mwaka huu utakaozingatia makubaliano yaliyofikiwa na upande wa upinzani yaliyolenga kuepusha umwagikaji damu baada ya rais Kabila kukataa kuachia madaraka wakati muda wake ulipomalizika mwezi Desemba maka jana.  Jamii ya Kimataifa imesisitiza kufanyike uchaguzi wa urais haraka iwezekanavyo lakini mpaka sasa hakujakuwepo na ratiba yoyote ya uchaguzi. 

Tume ya uchaguzi ya nchini Kongo iliyo na wajibu wa kuandaa uchaguzi imesema haitawezekana kufanyika uchaguzi mpaka mwa 2019.  sababu moja kuu inayozuia uchaguzi huo kuandaliwa ni vurugu zinazoendelea katika jimbo la kati la Kasai ambalo lina utajiri mkubwa wa madini ya Almasi. kamishna mkuu wa tume ya uchaguzi nchini humo amesema uasi katika eneo hilo umekuwa ukiendelea kwa muda wa mwaka mmoja sasa.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga