1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CUF yapinga vikali kuibuka kwa pendekezo jipya kuhusu katiba

George Njogopa28 Machi 2022

Mwenyekiti wa chama cha CUF, Ibrahim Lipumba amepinga vikali pendekezo linalotaka mchakato wa uandikaji katiba mpya uanze baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

https://p.dw.com/p/498fw
Tansania Dar es Salaam | Partei CUF | Ibrahim Lipumba
Picha: DW/S. Khamis

Akiwasilisha maazimio yaliyofikiwa na baraza kuu chama chake mbele ya waandishi wa habari, Profesa Lipumba amesisitiza kiu ya wadau wa siasa nchini ni kuona mchakato wa uandikaji katiba mpya unaanzishwa mara moja na hilo linawezekana kwa kuanza kuipitia sheria iliyofungua njia kuandika katiba mpya.

Katiba mpya baada ya uchaguzi wa 2025 ?

Mwanasiasa huyo ameyapinga vikali mapendekezo yaliyowasilishwa hivi karibuni kwa Rais Samia Suluhu Hassan na kamati ya wadau wa siasa ikifahamika kama kikosi kazi waliosema kwamba Tanzania ianzishe mchakato wa uandikaji katiba mpya mara baada ya kukamilika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

''Baraza Kuu linapinga vikali kuibuka kwa pendekezo jipya ambalo halikuwa zao la mkutano wa Dodoma kuwa mchakato wa kupata katiba mpya usubiri mpaka baada ya uchaguzi mkuu.''

Karibu idadi kubwa ya vyama vya upinzani vinaonekana kutofautiana na msimo huo wa kamati ya wadau wa siasa, isipokuwa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo ambacho kiongozi wake yupo kwenye kikosi kazi, kinachotaka mchakato wa katiba mpya utanguliwe kwanza na mabadikio katika tume ya uchaguzi, kikitaka kile inachosema tume huru ya uchaguzi.

Soma pia→CUF: licha ya uchumi kuimarika Tanzania wananchi wanaishi katika umasikini

Serikali yatakiwa kuweka wazi ripoti ya tume ya uchunguzi

CUF yashauri kufumuliwa jeshi la polisi nchini Tanzania
CUF yashauri kufumuliwa jeshi la polisi nchini TanzaniaPicha: DW/S. Khamis

Mbali ya hali ya kisiasa, Profesa Lipumba ametaja maazimio mengine yaliyofikiwa na chama hicho ikiwamo shinikizo la kutaka kuwekwa hadharani ripoti ya mauji yanayodaiwa kufanywa na askari polisi dhidi ya raia huko Mtwara na Kilindi.

''Baraza Kuu limesikitishwa na matukio polisi kufanya mauaji ya  raia mara kwa mara. Baraza Kuu linaitaka serikali kuweka wazi taarifa ya tume iliyoundwa na waziri mkuu.''

Chama hicho hakijajiweka kando kuhusiana na mzozo wa vita unaoendelea huko Ukraine na kimeitolea wito Urusi kusitisha mara moja mashambulizi yakie na kutaja idadi ya watu wanaopoteza maisha na kukimbia kuwa ni janga lisilopaswa kufumbia macho.

Hata havyo chama hicho hakusema lolote kuhusu hatua ya Tanzania kutochukua upande katika vita hivyo, ingawa kimesisitiza kuwa bega kwa bega na wanachi wanaathirika kutokana na vita hivyo inayoingia mwezi wa pili sasa tangu ilipoanzishwa.

Soma piaUpinzani Tanzania wataka mabadiliko ya mifumo ya utawala

Hivi karibu Tanzania ilijizuia kupiga kura ndani ya Umoja wa Mataifa, lakini mataifa mengi barani Ulaya yalichukua uamuzi wa kuilani Urusi kutokana na uvamizi wake Ukraine. Wizara ya mambo ya nje ya ilisisitiza msmamo wa Tanzania wa kuendelea na sera ya kutofungamana na upande wowote katika baadhi ya masuala tete yanayoikabili dunia.