1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia imeshindwa kufikia lengo la kusitisha ukataji miti

24 Oktoba 2023

Mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti wameonya Jumanne kwamba ulimwengu unafeli katika ahadi yake ya kuachana na ukataji miti ifikapo mwaka 2030. Madhara yatokanayo na vitendo hivyo yadhihirika kote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/4Xws5
Brasilien  Amazon Drought / Dürre am Amazonas
Edmilson Marques (mkulima) wakati akijaribu kuzuia moto unaoenea msituni na kulinda mazao yake. Manaus, Brazil-Oktoba 10, 2023 Picha: Gustavo Basso/DW

Mnamo mwaka 2021, viongozi kutoka zaidi ya nchi na wilaya 100 wanaowakilisha idadi kubwa ya misitu duniani, waliahidi kuwa ifikapo mwaka 2030, wangesitisha vitendo vinavyopelekea kuharibiwa kwa misitu na badala yake wangelichukua hatua mbadala za kuitunza.

Lakini tathmini ya kila mwaka iliyotolewa hii leo, imefichua kuwa ukataji miti duniani uliongezeka kwa asilimia 4 mwaka jana, na kwamba ulimwengu bado unajikongoja ili kufikia malengo ya mwaka 2030.     

Erin Matson, mhariri mkuu wa Tathmini hiyo kuhusu  Tamko la Misitu  anasema malengo ya mwaka 2030 si jambo zuri tu kufikiwa, bali ni muhimu kwa kudumisha mazingira bora kwa ajili ya maisha ya binadamu.

Brasilien Ibama Regenwald Abholzung
Eneo la msitu wa mvua la Amazon lililokumbwa na vitendo haramu vya ukataji miti- Ibama Brazil-23.08.2023Picha: Nádia Pontes/DW

Misitu, sio tu makazi muhimu kwa maisha ya wanyama lakini hutumika pia kama vidhibiti muhimu vya hali ya hewa duniani na huvuta hewa chafu ya kaboni inayozalishwa kutokana na shughuli za binadamu.

  Soma pia:  Misitu ya Afrika Magharibi yanatoweka   

Hata hivyo mwaka jana, vitendo vya ukataji miti vilikuwa juu kwa asilimia 20 zaidi kuliko ilivyotakiwa ili kutimiza ahadi ya viongozi ya kuilinda misitu, huku hekta milioni 6.6 za misitu zikipotea, na asilimia kubwa ikiwa ni misitu muhimu katika eneo la kitropiki.

Tathmini hiyo, iliyotolewa na zaidi ya makundi 24 ya mazingira na mashirika ya utafiti, inaonya pia kuwa uharibifu wa misitu bado ni tatizo kubwa. Uharibifu huo unazingatia aina mbalimbali za madhara, ikiwa ni pamoja na mioto ya nyika na kupotea kwa bioanuai, ambavyo huathiri hali jumla ya misitu.  

Matson amesema kila mwaka data hubadilika na kwamba kilicho muhimu ni mwelekeo, huku akisisitiza kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka 2018 hadi 2020, tulikuwa katika mwelekeo mbaya.

Soma pia: Mkutano wa kilele wa msitu wa Amazon wafanyika Brazil      

Tathmini hiyo haikuwa mbaya kote ulimwenguni. Takriban nchi 50 ikiwemo Brazil, Indonesia na Malaysia zilikuwa katika mwelekeo mzuri wa kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukataji miti na kuiteketeza misitu.


Lakini ripoti hiyo inaonya kwamba mafanikio hayo yamo hatarini. Mfano Indonesia,  kuna wasiwasi kwamba sheria mpya ya kuunda nafasi za kazi inaweza kudhoofisha mafanikio hayo. Na huko Brazil, wakati kukishuhudiwa muamko wa kuulinda msitu wa Amazon, pori la Cerrado ambalo ni muhimu pia kwa ikolojia limekuwa likilengwa.     

VAE, Abu Dhabi | #COP28 Aufsteller
Mtu akipita mbele ya maandishi ya "#COP28" wakati wa warsha wa siku moja kuhusu hatua za hali ya hewa, huko Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, Oktoba 1, 2023.Picha: Amr Alfiky/REUTERS

Ripoti hiyo imesifu sheria mpya zilizoanzishwa na Umoja wa Ulaya zinazonuiwa kuzuia uagizaji wa bidhaa zinazochochea ukataji miti. Lakini imetoa wito wa kuchukuliwa hatua kali za kimataifa, ikiwa ni pamoja na fedha zaidi za kulinda misitu, na kukomesha ruzuku kwa sekta kama vile kilimo ambacho kinasababisha ukataji miti.

Ripoti hiyo inakuja kabla ya viongozi mbalimbali kukutana mwezi ujao kwa mazungumzo mapana kuhusu ya hali ya hewa, lakini watafiti hao wanahofia kwamba suala la ukataji miti linaweza kutopewa kipaumbele kwenye majadiliano hayo, hasa juu ya nishati mbadala na mustakabali wa nishati ya kisukuku.

      

(Chanzo: AFP)