1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la EUFOR halitajihusisha na mzozo kati ya Chad na Sudan

Halima Nyanza14 Februari 2008

Kiongozi wa jeshi hilo asema mfumo wake haujabadilika

https://p.dw.com/p/D7TO
Wanajeshi wa Ufaransa wakishika doria mjini NdjamenaPicha: AP

Kiongozi wa Kikosi cha Jeshi la kulinda amani cha Umoja wa Ulaya kinacholinda wakimbizi wa Darfur, Jenerali Jean Philippe Ganascia, ameahidi kuwa jeshi hilo halitajihusisha na mzozo kati ya serikali ya Chad na waasi wa nchi hiyo.

Kiongozi huyo wa Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Ulaya ambaye anatokea Ufaransa, amefahamisha kwamba mfumo wa jeshi hilo, katika operesheni zake haujabadilika wala kuwa na upendeleo.

Ameongeza kusema kuwa kazi yao iliyowapeleka huko ni kulinda raia.

Umoja wa Ulaya juzi ulianza tena kusambaza wanajeshi wake nchini Chad na Jamhuri ya Afrika ya kati, baada ya kusimamisha zoezi hilo kwa muda baada ya waasi kuvamia mji mkuu wa Chad, Ndjamena.

Kikosi hicho kinatarajiwa kuwa na wanajeshi 3700.

Wizara ya ulinzi ya Ufaransa iliarifu kuwa, hakuna mwanajeshi yeyote wa wa nchi hiyo au kutoka katika kikosi hicho maalum, atakayejiingiza katika mapigano kati ya serikal na waasi wa Chad.

Lakini hata hivyo, waasi wa Chad waliipinga kauli hiyo, ambapo msemaji wao alisema Ufaransa imekuwa ikihatarisha maisha wa raia wa nchi hiyo kwa kuruhusu jeshi lake kumuunga mkono rais wa nchi hiyo, Idris Debby.

Siku tatu tu baada ya waasi kufukuzwa, February sita, Rais wa Chad anaelezwa kutoa taarifa ambayo inaleta utata.

Rais Derby alitaka kusambazwa haraka kwa kikosi hicho na kuongeza kuwa hali hiyo.

Kazi ya wanajeshi hao inaweza kuwa ngumu kwa madai ya uungwaji mkono unaofanywa na majeshi ya Ufaransa kwa serikali ya Chad.

Wanajeshi hao wa kulinda amani watakuwa katika maeneo ya mashariki ya Chad karibu na mpaka wa Sudan na karibu pia na sehemu ambayo waasi wamekuwa wakiendesha shughuli zao.

Chad imekuwa ikilalamika kuwa waasi hao wanakingiwa kifua na Sudan.

Kikosi hicho cha Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Ulaya kilichoanza shughuli zake mwishoni mwa mwezi Januari, kilisimamisha kazi hiyo February mosi baada ya waasi wa Chad kuuzingira mji mkuu wa nchi hiyo, Ndjamena.

Majeshi ya Chad yaliwafurumusha waasi hao waliokuwa na lengo la kumpindua Rais wa nchi hiyo Idris Derby baada ya mapigano makali yaliyotokea Februari mbili na tatu.

Kikosi hicho cha kulinda amani cha Umoja wa Ulaya, kinatekeleza agizo la Umoja wa Mataifa kulinda wakimbizi wanaokimbia mapigano katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan na pia watu waliolazimishwa kuhama makazi yao na waasi nchini Chad na kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya kati.

Wakati huohuo Ireland imefahamisha kuwa itaanza kusambaza wanajeshi wake wa kulinda amani nchini Chad wiki ijayo, na kwamba kikosi kizima cha wanajeshi kitaanza kusambazwa katikati ya mwezi wa tatu.

Nayo Ufaransa tayari ina zaidi ya wanajeshi elfu moja nchini Chad, nchi ambayo ilikuwa koloni lake.

Operesheni hiyo ya Umoja wa Ulaya ambayo ilipaswa kuanza Novemba mwaka uliopita, imekuwa ikiahirishwa mara kadhaa kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo kupata wanajeshi wa kutosha.