1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiNigeria

Nigeria:Jeshi lakanusha vitendo vya utoaji mimba kwa mateka

26 Aprili 2023

Jeshi la Nigeria linapinga uwepo wa mpango wa siri wa utoaji mimba kwa wanawake waliookolewa kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram.Mashirika ya haki za binadamu yanasema ni muhimu uchunguzi wa kina ufanyike.

https://p.dw.com/p/4QVJY
Nord-Nigeria Dorf Ngarannam | Bintu im Interview
Picha: DW

Tume ya Haki za binadamu ya Nigeria ambayo kwa sasa inachunguza madai hayo ya utoaji mimba yalioungwa mkono na jeshi miongoni mwa wanawake mateka wa Boko Haram,  imeahidi kuwa ripoti yake ya mwisho itakuwa ya kina huku jeshi la nchi hiyo likikanusha mara kwa mara kutokea kwa vitendo hivyo.

Jopo maalum la tume hiyo limekuwa likifanya mikutano ya hadhara tangu Februari mwaka huu, lilipoanzisha uchunguzi maalum juu ya matukio hayo.

Mpango wa siri wa utoaji mimba ulidaiwa kutekelezwa na jeshi la Nigeria kama sehemu ya mapambano yake dhidi ya kundi lenye itikadi kali la Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Ripoti ya uchunguzi iliyotolewa mwezi Disemba mwaka jana ilidai kuwa jeshi lilisimamia takriban vitendo 10,000 vya uavyaji mimba kwa wanawake na wasichana waliokuwa wakizuiliwa na kubakwa na wanamgambo hao wenye itikadi kali ya Kiislamu.

Soma pia: Watoto 150 wa shule watekwa nyara Nigeria

Mkuu wa Majeshi wa Nigeria, Luteni Jenerali Farouk Yahaya amesema alipokuwa akitoa ushahidi mbele ya jopo maalum mwezi uliopita kuwa

jeshi limenafanikiwa na si wengi wanaofurahia mafanikio yao na kwa sababu  hawawezi kubadili chochote ndio maana wanawapaka tope.

Luteni Jenerali Yahaya amesisitiza kuwa wao si magaidi wa Boko Haram na kwamba wamefunzwa kuwa wataalamu na mafunzo hayo ni endelevu. Amekanusha pia kutokea kwa vitendo hivyo vya siri vya utoaji mimba, ambavyo ilisemekana vilitekelezwa kwa waliokuwa wake wa wapiganaji wa Boko Haram, waliookolewa na waliyokuwa wakiishi katika kambi za wakimbizi wa ndani.

Jeshi lakanusha ripoti ya utoaji mimba

Kulingana na ripoti ya awali ya shirika la habari la Reuters,  vitendo vya utoaji mimba viliendeshwa kati ya mwaka 2013 na 2022 na kwa kiasi kikubwa bila idhini ya wanawake husika.

Nigeria Zwangsabtreibungen, Soldaten mit Boko Haram Flagge
Majeshi wa Nigeria wakiwa na Bendera ya Kundi la Kigaidi la Boko Haram baada ya kuchukua udhibiti wa mji wa Damasak, huko Nigeria (18.03.2015)Picha: REUTERS

Jenerali Tukur Yusuf Buratai, Mkuu wa Majeshi wa zamani aliyehudumu kati ya mwaka 2015 na 2021, ameiambia DW kwamba anatilia mashaka uwepo wa mpango huo wa siri wa uavyaji mimba.

Soma pia: Boko Haram yatwaa udhibiti wa jamii za katikati ya kaskazini mwa Nigeria

Buratai ameendelea kueleza kuwa jeshi hilo lilikuwa na utaratibu maalum wa kuwahudumia wajawazito na kwamba waliwekwa kwenye vituo maalum na waliruhusiwa kujifungua kwa njia ya kawaida. Na kusema haelewi msingi wa madai hayo.

Makundi kadhaa ya utetezi yadai uchunguzi

Lakini baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wanatilia mashaka kauli za Jeshi kukana kuhusika katika vitendo hivyo na wametaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu madai hayo.

Udeme Edoemaowo kutoka Mtandao wa Kupambana na Unyanyasaji wa Majumbani ameiambia DW kwamba mashirika ya kiraia yanatafakari uwezekano wa kuanzisha uchunguzi wao wenyewe.  Tume ya Haki za Kibinadamu ya Nigeria   imesema imejitolea kufanya uchunguzi wa kina.

Lakini Edoemaowo anasema muungano wake wa mashirika ya kiraia bado utataka kuthibitisha madai yenyewe na wanapaswa kwenda hadi huko Maiduguri kufanya kila waliwezalo ili kuhakikisha wanapata ukweli kuhusu suala hilo.

Soma pia: Wabeba silaha waua 3, wawateka 20 chuoni Nigeria

Madai yanayoficha tatizo kuu

Andy Parah, wakili wa Nigeria mwenye makazi yake Abuja, ameiambia DW kwamba jeshi lazima liepuke kuficha taarifa zozote kuhusiana na matukio hayo, lakini amesema madai hayo yanaweza kuwapumbaza na wakapuuzia mapambano makali yanayoendelea dhidi ya kundi hilo la Boko Haram.

Mkuu wa Majeshi wa Zamani Jenerali Buratai, amesema anazingatia madai hayo kuwa mkakati au kampeni ya uasi dhidi ya Nigeria na hata Afrika kwa ujumla, bila hata hivyo kutoa ushahidi wa madai hayo.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametaka ripoti ya mwisho ya uchunguzi huo iwekwe hadharani, jambo ambalo Tume ya Haki za binadamu imehakikisha kuwa litafanyika.