1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoIvory Coast

Kameruni yatinga hatua ya mtoano baada ya kuilaza Gambia 3-2

24 Januari 2024

Kameruni ilitoka nyuma na kufunga mabao mawili ndani ya dakika tano za mwisho na kutinga hatua ya 16 bora kwa kuilaza Gambia 3-2 kwenye mechi ya kusisimua ya kundi C.

https://p.dw.com/p/4bbcg
AFCON | Mechi ya kundi C kati ya Gambia na Kameruni
Beki wa Gambia Muhammed Sanneh akimzuia mshambuliaji wa Kameruni Kevin NkoudouPicha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP

Kameruni ambao ni mabingwa mara tano wa michuano hiyo ilimaliza katika nafasi ya pili, ikiwa na alama 4 nyuma ya Senegal iliyoongoza kundi hilo ikiwa na alama 9.

Vijana wa Rigobert Song sasa watachuana na Super Eagles Nigeria katika uwanja wa Felix Houphouet Boigny mjini Abdijan siku ya Jumamosi.

Gambia inayojulikana kwa jina la utani kama "The Scorpions" nusra waizime ndoto ya Kameruni ya kufuzu raundi ya mtoano kwa kufunga bao la dakika ya 93 ya mchezo, japo bao hilo lilifutwa na refarii baada ya beki Muhammed Sanneh, kupitia ushauri wa teknolojia ya vidio, VAR, kuonekana aliucheza mpira huo kwa mkono.

Soma pia: Ivory Coast ukingoni mwa kutolewa nje ya michuano ya AFCON

Kipigo cha 2-0 cha Guinea mbele ya mabingwa watetezi Senegal kuliipa nafasi Kameruni kukwea hadi nafasi ya pili kutokana na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, japo Guinea imefuzu pia katika raundi ya 16 bora kwa kuwa miongoni mwa timu nne bora zilizoshika nafasi ya tatu.

Kocha wa Kameruni Rigobert Song alimuweka benchi Andre Onana na nafasi yake mchumani ikachukuliwa na binamu ya kipa huyo wa Manchester United, Fabrice Ondoa.

Algeria yafungishwa virago baada ya kufungwa na Mauritania 

Mshambuliaji wa Mauritania Souleymane Anne akipambana kuuchukua mpira mbele ya wachezaji wa Algeria
Mshambuliaji wa Mauritania Souleymane Anne akipambana kuuchukua mpira mbele ya wachezaji wa AlgeriaPicha: Kenzo Tribouillard/AFP

Algeria imeyaaga michuano ya AFCON baada ya Mauritania kuifunga 1-0 na kujikatia tiketi ya raundi ya 16 bora.

Beki wa kati Yali Dellahi aliifungia Mauritania bao hilo la kipekee kunako dakika ya 37 ya mchezo na kuwakata makali Algeria, ambao ni mabingwa mara mbili wa AFCON.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa, Algeria imeondolewa katika michuano hiyo katika hatua ya makundi kwa makala ya pili mfululizo.

Riyad Mahrez na wenzake wamemaliza mkiani mwa kundi B ikiwa na alama mbili pekee wakati Mauritania ikisonga mbele kama moja ya timu bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu.

Mauritania sasa itazipiga na Cape Verde iliyoongoza kundi B. Mechi hiyo itatifua vumbi katika dimba la Felix Houphouet Boigny mjini Abdijan siku ya Jumatatu.

Soma pia: Kombe la Afrika: Nyota wa soka wawa mashujaa wa kitaifa 

Algeria kwa upande wao, watafunganya virago wakiungana na Ghana ambayo licha ya kuwa jina kubwa katika soka la Afrika, iliambulia katika nafasi ya tatu katika kundi B ikiwa na alama mbili pekee.

Na katika mechi ya kundi D, Angola iliandikisha ushindi wa 2-0 mbele ya Burkina Faso na kutinga hatua ya 16 bora kama vinara wa kundi hilo.

Vijana hao wanaotiwa makali na kocha Pedro Goncalves sasa watamenyana na timu ya tatu kutoka aidha kundi E ama F huku Burkina Faso ikipangwa kucheza na mshindi wa kundi E Jumanne ijayo.

Mechi hizo zinaendelea tena leo huku Namibia ikiwa na kibarua dhidi ya Mali, Afrika Kusini ikizipiga na Tunisia wakati Taifa Stars ya Tanzania itamenyamana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kabla ya Zambia kumaliza udhia na Morocco.