1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moroko yaichabanga Tanzania 3-0 AFCON

Mohammed Khelef
17 Januari 2024

Moroko imeonesha ubabe wake mbele ya timu ya taifa ya Tanzania kwa kuichabanga mabao 3-0 katika Uwanja wa Laurent Pokou mjini San Pedro nchini Ivory Coast, ikiwa ni mechi ya kwanza kwenye Kundi F.

https://p.dw.com/p/4bOR8
AFCON2024, Moroko, Tanzania,
Mlinzi wa Moroko, Achraf Hakimi (kushoto) na kiungo wa Tanzania, Himid Mao, wakiwania mpira kwenye mechi ya kwanza ya Kundi F katika Michuano ya Kombe la Afrika, AFCON2024, katika Uwanja wa Laurent Pokou mjini San Pedro, Ivory Coast, siku ya Jumatano (Januari 17, 2024).Picha: Sia Kambou/AFP

"Mchezo mzuri usiku wa leo vijana wetu, Taifa Stars. Japo bahati haikuwa upande wetu. Tunaendelea kuwatakia kila la kheri na Taifa liko nyuma yetu katika mechi zenu zinazofuata." Aliandika Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kupitia mtandao wa X muda mchache tu baada ya meli hiyo iliyochezwa usiku wa Jumatano (Januari 17) kumalizika.

Alikuwa ni nahodha wa simba hao wa milimani, Romain Saïss, aliyekuwa wa kwanza kuziona nyavu za Taifa Stars katika kipindi cha kwanza cha mchezo. Mabao mengine yalipachikwa na Azzedine Ounahi na Youssef En-Nesyri. 

Soma zaidi: Kombe la Afrika: Nyota wa soka wawa mashujaa wa kitaifa

Licha ya kuwa kwake timu kubwa barani Afrika kwa miongo kadhaa, Moroko inawania kutwaa kombe hilo la michuano ya bara hilo kwa mara ya pili tu, ikiwa ni miaka 48 tangu ilitwae nchini Ethiopia.

Shamrashamra za Kongo kuelekea mechi ya AFCON

Hata hivyo, ushindi huu wa jana kwenye kiwango cha makundi dhidi ya Tanzania ulitarajiwa kwani Moroko ni ya 13 kwa kiwango cha soka ulimwenguni, ikiitangulia Taifa Stars kwa nafasi 108. 

Miaka miwili iliyopita, Moroko ilikuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika nusu fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar, baada ya kuibwaga mimba ya soka duniani, zikiwemo Uhispania na Ureno kwenye mechi  za mtoano. 

Moroko iko mbali sana ya Tanzania

Wachezaji saba kati ya kumi na moja waliocheza mechi ya jana, walikuwamo kwenye kikosi kilichocheta nusu fainali hiyo dhidi ya Ufaransa nchini Qatar. 

Soma zaidi: Tanzania kuzipiga na Morocco katika mechi ya ufunguzi AFCON

Wachezaji watatu kati yao wanachezea ligi ya Uhispania, La Liga, wawili kutoka Premier League, wawili kutoka Ligue (Anh) 1 ya Ufaransa na wawili kutoka Saudi Pro League ya Saudi Arabia. Waliosalia walikuwa wachezaji wanaocheza soka ya kulipwa katika klabu za Uturuki na Misri. 

Taifa Stars vs Morocco michuano ya AFCON

Kikosi cha Moroko kilikuwa tafauti kabisa na cha washindani wao, Taifa Stars, ambacho hakina majina yanayofahamika kimataifa, zaidi ya Tarryn Allarakhia anayechezea klabu moja nchini Uingereza na Mbwana Samatta ambaye amewahi kuchezea klabu za Uingereza na Uturuki.

Haikuwa jambo la ajabu, kwa hivyo, kwamba mchezo mzima ulimilikiwa na Moroko. 

Kwa upande wa mechi ya pili kwenye kundi hilo la F, Zambia iligawana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo sare ya bao moja kwa moja.

Bao la Kongo liliwekwa kimiani na Yoane Wissa, mzaliwa wa Ufaransa anayechezea soka ya kulipwa inayoshiriki Premier League nchini Uingereza, Brentford, huku lile la Zambia likiwekwa na Kings Kangwa, anayecheza soka ya kulipwa na klabu ya Red Star nchini Serbia.