1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa la Afrika lakaa kimya kuhusu kashfa ya ngono

Kabogo Grace Patricia27 Aprili 2010

Viongozi kadhaa wa Kanisa Katoliki barani humo wazungumza na AFP na kuelezea visa hivyo.

https://p.dw.com/p/N84L
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedikto XVI.Picha: AP

Wakati Kanisa Katoliki likiwa limegubikwa na kashfa za mapadri wa kanisa hilo kuwanyanyasa watoto kingono hasa katika nchi za Ulaya na Marekani, Kanisa hilo barani Afrika linaonekana kukaa kimya na kutozungumzia visa hivyo ambavyo vimegonga vichwa vya habari.

Kumekuwa na malalamiko kwamba viongozi wa ngazi za juu wa Kanisa Katoliki huko Marekani na katika bara la Ulaya kuficha visa vya watoto kunyanyaswa kingono na mapadri wa Kanisa hilo kwa kutumia mfumo wa kuwahamisha mapadri hao kutoka kwenye parokia moja kwenda kwenye parokia nyingine, ambako saingine huendeleza vitendo hivyo, badala ya kuwashitaki na kuwachukulia hatua kutokana na uovu huo wanaoufanya. Maafisa wa Kanisa Katoliki katika nchi za Nigeria, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo waliohojiwa na shirika la habari la AFP, walipuuzia maswali kuhusu tuhuma hizo za ngono na wakati mwingine wamevilaumu vyombo vya habari kwa kulikuza suala hilo.

Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki katika eneo la Kusini mwa Afrika, Askofu Mkuu Buti Tlhagale amesema kuwa kashfa ya kuwanyanyasa watoto kingono katika Kanisa Katoliki imeligusa Kanisa la Afrika, akisema kuwa visa 40 vimeripotiwa katika kipindi cha miaka 14 iliyopita katika eneo hilo. Askofu Tlhagale anasema kitendo cha mapadri wa Afrika kutojiheshimu hakijawekwa wazi sana katika vyombo vya habari ikilinganishwa na sehemu nyingine duniani.

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kinshasa, Mhashamu Laurent Monsengwo Pasinya aliiambia AFP kuwa katika utendaji wake wa miaka 30 kama askofu, hajawahi kupokea malalamiko yoyote kuhusu kashfa za ngono miongoni mwa mapadri wake. Maafisa wa Kanisa Katoliki wanasema kuwa tuhuma hizo zinatakiwa zitatuliwe ndani ya kanisa, kuliko kushughulikiwa kisheria zaidi. Msemaji wa Jimbo Kuu la Kampala, Uganda, Monsinyori John Katende amesema kuwa suala la kutubu liko ndani ya moyo wa mtu, hivyo hawawezi kuamini mfumo wa kisheria.

Aidha, mapadri wa zamani wamevielezea visa hivyo kwa namna nyingine tofauti. Felix Koffi Ametepe, padri wa zamani kutoka Burkina Faso anasema wakati yupo ndani ya kanisa aligundua visa kadhaa vya manyanyaso, vilivyokuwa vikifanywa hasa na mapadri wa kigeni.

Kwa upande wake msemaji wa Wakatoliki nchini Nigeria, Askofu Felix Ajakaiye anasema kuwa kosa lililofanywa na mapadri wachache lisitumike kulitupia lawama Kanisa Katoliki kwa ujumla. Askofu Ajakaiye anasema kinachotokea Ulaya kinaweza kutokea sehemu nyingine yoyote ile, barani Afrika na pia Nigeria. Kwa mujibu wa askofu huyo, hakuna mtu aliyekingiwa dhambi na kwamba binaadamu ni dhaifu. Afrika ni moja kati ya mabara ya dunia ambako Kanisa linakua na kwa sasa karibu watu milioni 800 barani humo ni Wakatoliki.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri:Abdul-Rahman