1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGabon

Kiongozi wa kijeshi Gabon kuapishwa leo

Sudi Mnette
4 Septemba 2023

Kiongozi wa kijeshi, Brice Nguema aliyemuondoa madarakani Rais Ali Bongo anatarajiwa kulihutubia taifa kwa mara ya kwanza kama rais wa mpito baada ya kula kiapo chake baadae leo hii.

https://p.dw.com/p/4VvDL
General Brice Clothaire Oligui Nguema
Picha: Gabon24/AP/picture alliance/dpa

Katika mapinduzi ya nane kwa kipindi cha miaka mitatu katika eneo hilo la Afrika Magharibi, maafisa wa kijeshi wakiongozwa na Jenerali Brice Nguema walijinyakulia madaraka Agosti 30, ikiwa ni dakika chache baada ya tangazo la tume ya uchaguzi lililompa Rais Bongo muhula mwingine wa tatu madarakani katika uchaguzi  ambao matokeo yake waliyoyafutilia mbali wakisema yaligubikwa na ulaghai.

Nguema ambae alichaguliwa na wenzake kama kiongozi wao, ataapishwa ili achukue nafasi ya kile wanachokiita Rais wa Mpito, na baadae atatoa hotuba yake ya kwanza kupitia televisheni ya umma ya taifa hilo. Mapinduzi hayo ambayo yaliufikisha mwisho uongozi wa miaka 56 wa familia ya Bongo yalizusha nderemo na vifijo ndani Gabon, lakini ulilaaniwa na mataifa ya nje.

Utulivu wa raia nchini Gabon.

Gabun | Militärputsch
Polisi wakiwa katika doria katika mbalimabli ya GabonPicha: AA/picture alliance

Oscar Maubogno ni mfanyabiashara ndogondogo wa huko Gabon. amenukuliwa akisema "Tulidhani itakuwa kama 2009 na 2016, ambapo kulikuwa na vifo na umwagaji damu katika nchi yetu. Lakini tunamshukuru Mungu, mambo ni shwari sasa jeshi limechukua nafasi."

Kutokana na mapinduzi hayo viongozi wa jumuiya ya kanda ya Afrika ya Kati ECCAS leo hii wanatarajiwa kukutana ana kwa ana kwa shabaha ya kujadili namna ya watakavyoweza kuyashughulikia. Wiki iliyopita waliwataka washirika wakiongozwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuunga mkono kurejea kwa haraka muongozo wa utaratibu wa kikatiba kwa Gabon.

Kizungumkuti cha jeshi kukaa mamlakani.

Hadi wakati huu mamlaka ya kijeshi  bado haijasema inatarajia kushikilia madaraka kwa muda gani. Ijumaa iliyopia Nguena alisema mamlaka hiyo itafanya juhudi za haraka katika kurejesha demokrasia ya taifa hilo lakini pia alitoa onyo kuwa karaka ya kupita kiasi inaweza kusababisha matokeo ya uchaguzi usio haminika.

Upande mkuu wa upinzani wa Gabon, Alternance 2023, ambao unadai kuwa ndio washindi  halali wa uchaguzi wa Agosti 26, ametoa wito jumuiya ya kimataifa kuhimiza jeshi lenye kudhibiti nchi kukabidhi madaraka kurudi kwa raia.

Soma zaidi:Upinzani Gabon washinikiza wanajeshi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia

Hadi wakati huu Rais Bongo bado yupo chini ya kizuizi cha nyumbani.  Kiongozi huyo alichaguliwa mwaka 2009, akichukua hatamu ya uongozi kutoka kwa marehemu baba yake aliyeingia madarakani mwaka 1967.

Wanaowapinga wanasema viongozi hao wametoa mchango mdogo sana kwa taifa panapohusika mgawanyo wa rasimiali ya mafuta na madini ya taifa hilo lenye jumla ya watu milioni 2.3.