1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la dunia 2010 kanda ya Afrika

9 Oktoba 2008

kinyanganyiro cha kuania tiketi za kombe la dunia kinapambamoto mwishoni mwa wiki hii:

https://p.dw.com/p/FX0I

Kinyanganyiro cha kuania tiketi za kombe la dunia 2010 kwa kanda zote ulimwenguni, kinapambamoto kesho Ulaya,Asia,Afrika na Amerika kusini.Katika kanda ya Afrika, kinyanganyiro cha tiketi 5 za bara hilo kinafikia kilele chake huku timu 16 zikiongozwa na Simba wa nyika-Kamerun na Nigeria, zikania kwa kila hali kucheza huko Angola na Afrika Kusini 2010 .

Kwa sura inavyoonesha ,simba wa nyika- Kamerun , Super Eagles-Nigeria,chipukizi Ruanda na Benin, zina hakika zitavuka salama-usalimini duru hii .

Timu zilizosalia zitabidi kupania sana ili kubakia katika kundi la timu 12 washindi au ndani ya timu 8 bora za nafasi ya pili ili kusonga mbele.

Hali inatatanisha zaidi kufuatia mpango wa kufuta matokeo ya mwisho ya timu zitakazomaliza nafasi ya pili dhidi ya zile zilizomaliza mkiani mwa makundi ya timu 4-4.Hii ni kwa sababu Ligi 2 ndogo zitabakia na timu 3-3 .

Timu zitapaswa kuhitaji alao pointi 6 ili kujiunga na kundi la timu bora za nafasi ya pili.Katika utaratibu huu, Cape Verde yenye miadi na Taifa Stars-Tanzania, mjini Dar-es-salaam kesho, Angola,Sierra Leone na Botswana, huenda zikaangukiwa na bahati mbaya ya kumalizia nafasi ya pili kutoka makundi yao na halafu kupigwa kumbo nje ya kombe la Afrika na la dunia 2010.

Katika hali ya shaka shaka kama hii , timu gani zitasonga mbele na zipi zitapigwa kumbo, wenyeji Bafana bafana hawatasonga mbele duru ijayo.Ingawa wamehakikishiwa nafasi kucheza kombe la dunia , watakosa kucheza kombe la Afrika ikiwa ni mara ya kwanza tangu kupita miaka 16.

Angola, wenyeji wa kombe la Afrika la Mataifa ,ndio timu iliozisangaza timu nyengine za Afrika ilipotoroka na tiketi ya kombe la dunia 2006 Ujerumani ilipoiiga kumbo Nigeria .Mara hii Angola iko hatarini ya kupigwa kumbo nje ya kombe la dunia kwavile, itakua moja ya timu 16 zinazoania nafasi licha ya kwa mwenyeji.

Simba wa nyika-Kamerun wameshanguruma na hawawezi kupigwa kumbo na wakiitoa kesho Mauritius mjini Yaounde watasonga mbele.Cape Verde lakini, lazima ishinde Taifa Stars ilioanza kuja kwa meno ya juu ili iwe na nafasi ya kumaliza wapili kutoka kundi lao.Taifa Stars wameahidi kuwapa changamoto kali mjini Dar-es-salaam hapo kesho katika kundi hili la kwanza.

Ama katika kundi la 2, Guinea itaparamia kileleni mwa kundi hili ikiwa itatamba nyumbani mbele ya Harambee Stars -Kenya pia ambayo ina nafasi ya kusonga mbele.Ikiwa Guinea itashindwa kutamba nyumbani,Zimbabwe itasonga mbele mradi tu nayo iishinde Namibia-iliocheza kama Angola katika kombe lililopita la dunia hapa Ujerumani.Kenya inaongoza kundi hili la pili.

Kundi la 3,Benin ndio inaongoza kileleni,lakini ni kundi ambalo linadhibitiwa na Angola ambayo yamkini, ikiizidi nguvu Niger mjini Luanda itamaliza nafasi ya pili.Matumaini pekee kwa Ugandan Cranes ni kutamba mbele ya Benin kesho mjini Kampala na kutumai Angola inateleza.

Katika changamoto za kundi la 4,Bafana Bafana au Afrika Kusini, itaaibika kwa kumaliza mkiani ikiwa watashindwa kushinda kesho huko Guinea ya Ikweta.Igawa Sierra Leone wamewasangaza wengi kwa mchezo wao maridadi hadi sasa, kuishinda Nigeria si rahisi .

Kundi la 5 pia linatatanisha huku viongozi wake Libya ,Gabon na Black Stars Ghana iliotamba Ujerumani katika kombe la dunia 2006,zote zanyanganyia nafasi ya kwanza.Ghana yatazamiwa kuzima vishindo vya Lesotho nyumbani Accra wakati Libya inahitaji sare tu na Gabon kubakia kileleni na kuwapiga kumbo Afrika ya kati.

Katika kundi la 6 kati ya 12,Gambia na Senegal ziko pointi 1 tu nyuma ya viongozi Algeria wenye miadi na Liberia.Senegal na Gambiai lakin,i zinabidi kuoneshana nani mwenye nguvu zaidi kesho mjini Dakar .