1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lissu asema hatambui matokeo ya udanganyifu

Iddi Ssessanga
30 Oktoba 2020

Mgombea urais wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema - Tundu Lissu, ametangaza kutokuyatambua matokeo ya uchaguzi yaliokumbwa na udanganyifu. Marekani imesema kuna mashaka makubwa kuhusu uaminifu wa uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/3kd6l
Tansania | Oppositionsführer Tundu Lissu
Picha: Eric Boniphace/DW

Zoezi la kuhesabu kura likiendelea upande wa bara, visiwani Zanzibar, mgombea wa chama tawala CCM, Dk. Hussein Mwinyi, tayari ametangazwa mshindi. Marekani imesema kuna mashaka makubwa kuhusu uaminifu wa uchaguzi huo.

Rais wa Tanzania John Magufuli alipata uongozi wa mapema baada ya matokeo kuanza kukusanywa, akishinda kwa karibu asilimia 85 ya kura kutoka majimbo 32 yaliotangazwa na tume ya uchaguzi NEC, kati ya jumla ya majimbo 264.

Soma pia: Uchaguzi Tanzania: Rais Magufuli achukua uongozi wa mapema

Chama chake cha CCM kimekuwa madarakani tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mnamo mwaka 1961, lakini mashirika ya haki za binadamu yanalalamikia kwamba nchi hiyo imetumbukia katika utawala wa kimabavu katika kipindi cha miaka mitano iliyoshuhudia ukandamizaji mkubwa dhidi ya upinzani.

Mpinzani mkuu wa Magufuli, mgombea wa chama cha Demokrasia na MaendeleoChadema, Tundu Lissu, aliyataja matokeo yaliokuwa yanaingia kuwa "haramu", na kuwahimiza wafuasi wake kuandamana kwa amani, huku akiiomba pia jamii ya kimatifa kutoyatambua matokeo hayo, na kuongeza kuwa kilichotokea siyo uchaguzi bali udanganyifu usio kifani.

Tansania Wahlen | Präsident John Magufuli
Rais Magufuli alikuwa akiongoza kwa tofauti kubwa ya kura mbele ya Tundu Lissu.Picha: Ericky Boniphace/AFP

"Katika vituo vingi nchini kote, maelfu ya vituo vya kupigia kura, mawakala wetu wa uchaguzi walikatishwa tamaa kwa maksudi, wakazuwiwa kufanya kazi yao, na matokeo yake walicheleweshwa sana kuingia katika vituo vya kupigia kura," alisema Lissu Alhamisi mbele ya waandishi habari.

Soma pia: Chama cha CCM chadhibiti Dar es Salaam baada ya uchaguzi

Lissu mwenye umri wa miaka 52, alirejea Tanzania mwezi Julai baada ya kukaa nje ya nchi kwa miaka mitatu alikokuwa akitibiwa majeraha ya risasi 16 katika kile anachoamini lilikuwa jaribio la mauaji ya kisiasa.

Kurejea kwake kuliutia nguvu upinzani uliokuwa umedhoofishwa na miaka kadhaa ya mashambulizi, kamata kamata na marufuku dhidi ya mikutano ya kisiasa, na alivutia umati mkubwa katika mikutano yake yote ya kampeni.

Hata hivyo,  wabunge kadhaa wa upinzani wamepoteza viti katika ngome zao za muda mrefu, kama mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, aliyekuwa mbunge wa Hai mkoani Kilimanjarao, na kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe mkoani Kigoma kwenye pwani ya ziwa Tanganyika.

Kati ya viti 264 vya kuchaguliwa, CCM ilikuwa imeshinda viti 128, na kupoteza kimoja tu kwa chama cha Wananchi CUF.

Afrika Tansania Dar es Salaam Wahlen
Marekani inasema tofauti kubwa za ushindi wa chama cha mapinduzi zinatia shaka uaminifu wa uchaguzi.Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Marekani yakemea kamatakamata ya wapinzani

Taarifa kutoka Ubalozi wa Marekani nchini humo, ilisema kasoro na tofauti kubwa za ushindi wa chama tawala vinaibua mashaka makubwa kuhusu uaminifu wa matokeo na dhamira ya serikali juu ya maadili ya kidemokrasia.

Soma pia: Matokeo yakitikisa Chadema kanda ya kaskazini

Naye Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula wa kanisa la ufufuo la Moravia, alisema kilichotokea katika uchaguzi huo ni mapinduzi ya demokrasia.

"Mimi kama askofu na maaskofu wengine wanaosimamia haki, natangaza wazi kwamba uchaguzi uliofanyika Tanzania haukuwa huru na wa haki," alisema kiongozi huyo wa kidini.

"Na kwa sababu hizo, wale wote watakaotangazwa kama washindi watakosa uhalali wa Watanzania. Katika maneno mengine, uchaguzi ulikuwa wa udanganyifu, ni mapinduzi."

Chama cha ACT Wazalendo, kilisema mgombea urais wake wa Zanzibar Seif Sharif Hamad alikamatwa kwa mara ya pili wiki hii, pamoja na viongozi wengine wa chama, na kwamba afisa wa chama hicho Ismail Jussa alipigwa vibaya na wanajeshi.

Soma pia: Uchaguzi Tanzania: CCM yapata viti vingi, upinzani wapoteza

Balozi wa Marekani Donald J. Wright, alisema katika ujumbe wa Twitter wakati akitaka kuachiwa kwa Hamad, kwamba kukamatwa kwa viongozi wa upinzani siyo kitendo cha serikali yenye imani na ushindi wake wa uchaguzi.

Tansania Dodoma | Headquater | Uchaguzi House Tanzania
Makao makuu ya Tume ya Uchaguzi Tanzania NEC, yalioko mjini Dodoma.Picha: DW

Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ilisema Hamad alimaliza katika nafasi ya pili kwa kupata silimia 19 ya kura, huku mgombea wa chama tawala Dk. Hussein Mwinyi akishinda kwa asilimia 76.

Polisi haikuzungumzia tukio la kukamatwa Hamad, lakini ilithibitisha kukamatwa kwa watu wasiopungua 70 katika muda wa siku mbili katika matukio yanayohusiana na uchaguzi.

Soma pia: Wapinzani Tanzania walalamikia 'rafu' uchaguzi mkuu

Tume ya uchaguzi ya Tanzania imekanusha madai ya kuwepo na kasoro kwenye mchakato wa kura. Baadhi ya wakosoaji wa Magufuliwameelezea wasiwasi kwamba iwapo chama tawala kitashinda theluthi mbili ya viti bungeni, rais huyo anaweza kujaribu kubadilisha katiba na kurefusha kipindi cha urais kwa zaidi ya mihula miwili.

Vyanzo: rtre, ap, afpe, afptv