1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli atimiza siku 100 za uongozi

12 Februari 2016

Katika siku za kwanza za uongozi wake, rais wa Tanzania John Magufuli, amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa kuleta mabadiliko katika maeneo mengi. Watanzania na wachambuzi wazungumzia mafanikio yake.

https://p.dw.com/p/1HuFK
Rais Magufuli wa Tanzania
Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Miongoni mwa mambo ambayo Rais Magufuli amefanikiwa ni kuwafanya watu wengi wamzungumzie. Kila Mtanzania ana mtazamo fulani kuhusu kiongozi huyo na kuhusu vita vyake dhidi ya rushwa na juhudi zake za kupunguza matumizi ya serikali. Wachambuzi wanasema Magufuli ameweza kuwadhihirishia Watanzania kwamba kweli wana serikali inayofanya kazi.

Katika siku 100 za mwanzo za uongozi wake, Magufuli hajasita kuwaogopesha wanasiasa wenzake: Alifuta safari za "business class" na kupunguza idadi ya ujumbe wa kuhudhuria mikutano nje ya nchi. Pamoja na hayo alifuta sherehe za Uhuru Disemba 9 na badala yake kuwataka wananchi watumie siku hiyo kufanya usafi. Wananchi wengi wamempongeza, wakisema si rahisi kwa rais wa Kiafrika kufanikisha mambo kama hayo ndani ya siku 100.

Uongozi wa mtu mmoja tu?

Baadhi wanamwita "bulldozer" wengine wanamwita "jembe". Na katika siku za mwanzo kama rais, Magufuli ameonyesha kwanini amepewa majina hayo. Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kwamba asipoangalia anaweza akaenda mbali mno. "Kuendesha serikali si suala la mtu mmoja," anaonya mchambuzi Muhammad Yusuf wa Taasisi ya Utafiti wa Sera za Umma Zanzibar. "Angefanya vizuri zaidi kama angehakikisha kwamba taasisi zote za serikali zinafanya kazi kufuatana na sheria na katiba. Lakini hatakiwi kuingilia kile wanachotakiwa kufanya."

Naye mtaalamu wa masuala ya habari kutoka, Mlagiri Kopoka kutoka Mwanza Tanzania, akaongezea kwamba wapo wanaolalamika kuhusu Magufuli kuwa mkali mno. Upo wasiwasi kwamba kwa hatua anazochukua anaweza akawa anaingilia mifumo ya kidemokrasia.

Mchoro wa Said Michael kuhusu siku 100 za utawala wa Magufuli
Picha: DW/Said Michael

Mfano kwa majirani

Katika mitandao ya kijamii Magufuli amekuwa mtu anayeonekana kupendwa, si tu na Watanzania bali hata na wananchi wa nchi jirani kama Kenya. Kupitia maneno #WhatWouldMagufuliDo watumiaji wa mitandao wamekuwa wakitumia ubunifu na ucheshi kuonyesha namna ambavyo Magufuli amewafanya watake kubana matumizi.

Pamoja na hayo, baadhi ya rraia wa Kenya wameelezea kurtamani kuwa na rais kama Magufuli, wakisema yeye angekuwa na uwezo mkubwa zaidi kupambana na matatizo kama rushwa kuliko rais wao Uhuru Kenyatta.

Miezi ya kwanza ya tatu ya uongozi haitoshi kutoa tathmini iwapo Magufuli ni rais mzuri au la. Kwa sababu hiyo wachambuzi na wananchi wamekumbusha kwamba itabidi ionekane kwanza iwapo ataweza pia kutimiza ahadi alizotoa na iwapo mabadiliko aliyoanza nayo yatakuwa ya muda mrefu

Mwandishi: Philipp Sandner

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Khelef