1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makada wa CCM wewaka rekodi ya kuchukuwa fomu za kugombea

George Njogopa15 Julai 2020

Joto la uchaguzi linazidi kupanda nchini Tanzania huku idadi ya makada wa chama tawala CCM wanaojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge ikipundukia, na kuweka rekodi kuelekea katika uchaguzi huo wa Oktoba 2020.

https://p.dw.com/p/3fLhV
Tansania Dar es Salaam | Bischof Josephat Gwajima | Ufufuo na Uzima Kirche
Picha: DW/S. Khamis

Katika hali isiyoyatarajiwa na wengi, majina ya wanasiasa vigogo na wale wanaochipukia katika medani za siasa yameendelea kutawala katika vinywa vya watu kutokana na kujitokeza kwa idadi kubwa ya wanaowania kuteuliwa na chama hicho katika uchaguzi ujao.

Majina hayo yanahusisha wasomi wa vyuo vikuu, waandishi wa habari pamoja na kada nyingine wanaoendelea kujitokeza wakichukua fomu zinazoendelea kutolewa hadi hapo Julai 17 na baadaye kufuatiwa na mchujo kwa wagombea hao.

Mawaziri walioingia bungeni kwa kuteuliwa na rais nao pia wamejitosa kwenye kinyang'anyiro hicho wakichukua fomu katika majimbo mbalimbali. 

Soma zaidi Unayopaswa kujuwa kuhusu uchaguzi mkuu wa Tanzania 2015

Makada wengine ambao wamewahi kuwa wagombea lakini wakaanguka katika uchaguzi uliopita wa 2015 nao pia wamerejea tena kwenye kinyang'anyiro hicho.

Hii ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi kushuhudia chama hicho tawala kikiwavutia watia nia wengi wanaowania nafasi za ubunge na uwakilishi.

Tansania CCM-Generalsekretär Amtsübergabe Abdurahman Kinana & Bashiru Ally | General Bashiru Ally
Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally.Picha: DW/E. Boniface

Kumekuwa na maoni mengi yanayoendelea kuibuliwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuhusiana na hatua hiyo ya kujitokeza watia nia wengi kupitia chama hicho tawala.

Sam Ruhuza ambaye amekuwa akifuatilia hali ya kisiasa nchini humo kwa miaka mingi anasema idadi kubwa ya hao wanaojitokeza ni mwendelezo wa kile kinachoitwa kuunga mkono juhudi.

Katika baadhi ya majimbo wagombea wamefikia 30 na huenda idadi hiyo ikaongezeka katika kipindi cha siku chache kilichosalia cha uchukuaji na urejeshaji wa fomu.

Mtihani mkubwa utakaosalia kwa chama hicho ni namna kitakavyovuka kizingiti cha kuyachuja majina hayo na hatimaye kupata jina moja.

Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Humprey Polepole anasema mchakato wa kupata majina ya wagombea utafanyika kwa njia ya uwazi na kuzingatia demokrasia.

Wakati chama hicho tawala kikianza kutoa fomu kwa wagombea wake, nacho chama kikuu cha upinzani Chadema kinakamilisha mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kupata wagombea wake wa ubunge.