1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marufuku dhidi ya kutoka nje yatangazwa Beni

Saumu Mwasimba
28 Juni 2021

Mji wa Beni huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umewekwa chini ya sheria ya kuzuia watu kutoka nje baada ya kutokea mashambulizi matatu ya mabomu katika mji huo wa mashariki.

https://p.dw.com/p/3vhFM
Symbolbild | DR Kongo | Anschlag der Alliierte Demokratische Kräfte Kongo
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Maafisa wametoa tahadhari kwamba kuna ripoti mashambulio zaidi yanapangwa kufanywa. Wakati akitangaza hatua hiyo ya kuwataka watu wabakie majumbani mwao jana usiku, Meya wa Beni Narcisse Muteba alisema kila mmoja anapaswa kubaki ndani kwa sababu taarifa zinaonesha kuna kitu kingine kinachopangwa.

Mnamo Jumapili mabomu yaliripuliwa katika Kanisa Katoliki la mji huo na wanawake wawili waliuwawa na saa chache baadaye shambulio la kujitoa muhanga likafanyika nje ya klabu ya pombe.

Soma pia: Tshisekedi aahidi kupambana na waasi wa ADF

Ni mara ya kwanza kwa Jengo la Kanisa Katoliki kulengwa na mashambulizi katika eneo hilo ambalo limezidi kuandamwa na hujuma za wanamgambo wa kundi la Allied Democratic Forces, ADF, ambalo linahusishwa na matukio kadhaa ya mauaji katika kipindi cha miezi 18.

Watu wengi katika mji wa Beni ni waumini wa madhehebu ya Katoliki na mashambulizi hayo jana yalitokea katika kipindi cha saa moja kabla ya sherehe kuwapa watoto kipaimara.

Meya wa mji wa Beni ametoa agizo la kufungwa shule, makanisa na masoko wakati ulinzi ukiwa umeimarishwa.
Meya wa mji wa Beni ametoa agizo la kufungwa shule, makanisa na masoko wakati ulinzi ukiwa umeimarishwa.Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limesema wanamgambo wa itikadi kali wanaodaiwa kufungamana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu ndio waliohusika na mashambulizi mawili ya mabomu katika mji wa mashariki wa Beni.

Soma pia: Mauaji ya waasi wa ADF nchini DRC kupata suluhu?

Meya wa mji huo ametoa agizo la kufungwa shule, makanisa na masoko wakati ulinzi ukiwa umeimarishwa. Jeshi hilo la Kongo limesema mashambulizi ya Jumapili yanaonesha kufanywa na kundi la wanamgambo wa ADF, ambalo huko nyuma lilikuwa likitumia mabomu ya kutengeneza wenyewe.

Tuhuma za jeshi zimesadifiana na chapisho la madai yaliyotolewa na kundi la itikadi kali la Dola la Kiislamu linalosema kwamba limehusika na mashambulio hayo likisema watu wawili waliuwawa.

Hata hivyo, haikuwezekana kuthibitisha madai hayo yaliyotolewa kupitia ukurasa uliothibitishwa wa kundi hilo wa mtandao wa Telegram.