1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kati ya Uturuki na Afrika mjini Istanbul

18 Agosti 2008

Haja ya kuimarishwa zaidi ushirikiano yasisitizwa.

https://p.dw.com/p/F0P2
Rais wa Uturuki Abdullah Gül.Picha: AP

Wakati nchi zinazoinukia kwa kasi kiuchumi duniani China na India zikijipanua katika bara la Afrika ,Uturuki nayo imepania kuimarisha uhusiano wake na bara hilo.Viongozi wa nchi 53 za Afrika wakiwemo marais 7 wanahudhuria mkutano wa kwanza wa kilele kati ya Uturuki na Afrika mjini Istanbul. Mkutano huo wa siku tatu unaoanza leo unalenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kibiashara kati ya pande hizo mbili.

Mkutano huu wa kwanza wa ushirikiano kati ya Uturuki na Afrika unafanyika kuanzia leo hadi tarehe 21 ukiwajumuisha washiriki wa ngazi ya juu kutoka nchi kiasi cha 53 za Afrika.Lengo kubwa la Uturuki katika mkutano huo ulioandaliwa kwa usaidizi wa jumuiya ya Afrika ni kuimarisha ushirikiano wake na bara hilo.

Uturuki inapanga kuwa nchi itakayoongoza katika nyanja za uzalishaji,uwekezaji,technologia,uvumbuzi,nishati,utalii na fedha.

Kwa mujibu wa bwana Musa Kulaklikaya mkuu wa shirika la Uturuki la ushirikiano wa kimataifa na maendeleo TIKA, akizungumza kabla ya mkutano huo amesema ushirika wa uturuki barani Afrika umeanza tangu mwaka 2000 na mkutano huu wa Istanbul unatoa nafasi muhimu kwa nchi hiyo kuimarisha ushirikiano huu.

Anasema kuwa,"Mkutano huu wa kilele wa viongozi wakuu wa nchi na serikali ambao utafuatiwa na mikutano mengine itakayofanyika sambamba itakayohudhuriwa na wadau wengine,utakuwa ni nafasi nzuri ya kuimarisha uhusiano kati ya uturuki na Afrika na kufanyia utafiti nyanja kadhaa za ushirikiano kati ya pande hizo mbili.’’

Aidha bwana Kulaklikaya amezungumzia umuhimu wa Uturuki wa kutafuta nafasi ya kuwekeza barani Afrika na hasa kutokana na kujikita barani humo China na India.

Amesema ili Uturuki kujitangaza zaidi baranai Afrika katika suala la ushirikiano,wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imeamua kuongeza idadi ya ofisi zake za kibalozi kote barani humo kwa kufungua ofisi 15 mpya za ubalozi na ubalozi mdogo mpya katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la sahara.bwana Kulaklikaya anasema Uturuki inazidi kujikita hatua kwa hatua barani Afrika.Akaongeza,

"Ofisi zetu zinafanya kazi katika nchi 17 za Afrika lakini kwa mchango wa wadau wengine usaidizi wa uturuki unaweza kuonekana katika zaidi ya nchi 30 kote barani Afrika.’’

Mkakati wa Uturuki wa kuijongelea karibu Afrika ulianzishwa mwaka 1998 ukiwa na lengo la kuongeza ushirikiano na nchi za bara hilo kisiasa,kiuchumi,kibiashara,kijeshi na kitamaduni.Chini ya mtazamo huo Uturuki mwaka 2005 iliutangaza kuwa ni mwaka wa Afrika kama anavyosema Selda Ozdenoglu mtaalamu wa masuala ya Afrika kwamba kuanzia wakati huo Uturuki haijaweza kulifumbia macho bara hilo.

’’Kwa kweli bara la Afrika ni muhimu kwa Uturuki,hadi sasa hakuna uhusiano wa muda mrefu uliowekwaKwa vile Afrika ni bara muhimu kwa ulimwengu mzima na Uturuki ni nchi ambayo ingependa kuwa na jukumu katika ulingo wa kimataifa kwa hivyo ingekuwa vigumu kivyovyote nchi hiyo kutokuwa na shauku katika Afrika.Ingekuwa bora zaidi ingekuwa kumeshakuweko uhusiano wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili.’’

Shabaha ya Uturuki ni kufanya biashara na Afrika itakayofikia dolla bilioni 30 kufikia mwaka 2010.