1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mo Farah afichua alivyosafirishwa UK kimagendo akiwa mtoto

Iddi Ssessanga
12 Julai 2022

Katika makala ya filamu inayotarajiwa kutolewa hivi karibuni, mwanariadha wa Uingereza Mo Farah anatoa ufichuzi wa kushangaza kwamba alikuwa mhanga wa usafirishaji watoto kimagendo.

https://p.dw.com/p/4E1m4
Britischer Olympiasieger Mo Farah
Picha: MARTIN BUREAU/AFP

Bingwa mara nne wa mashindano ya Olimpiki Mo Farah amesema alisafirishwa kwa njia za magendo kwenda nchini Uingereza kutoka Somaliland akiwa na umri wa miaka 9 na amefichua kwamba jina lake halisi ni Hussein Abdi Kahin.

Mwanariadha huyo wa mbio ndefu wa Uingereza amesema alisafirishwa hadi Uingereza na mwanamke ambaye hakuwahi kukutana naye na alilazimishwa kufanya kazi za nyumbani na kuwahudumia watoto wa familia nyingine ili apate chakula.

"Ukweli ni kwamba mimi siye yule unayedhani ni mimi," Farah aliiambia BBC katika filamu ya makala inayoitwa "Mo Farah wa kweli", inayotazamiwa kurushwa siku ya Jumatano.

Soma pia: Mo Farah asisitiza yeye mwanariadha safi

"Simulizi halisi ni kwamba nilizaliwa Somaliland, kaskazini mwa Somalia, kama Hussein Kahin," aliliambia shirika hilo la utangazaji la Uingereza.

Britischer Olympiasieger Mo Farah
Farah alisema jina lake halisi ni Hussein Abdi Kahin.Picha: Molly Darlington/Action Images/REUTERS

Farah, ambaye ni mwanariadha wa kwanza wa mbio ndefu wa Uingereza kushinda medali nne za dhahabu katika mashindao ya Olimpiki, alisema huko nyuma kwamba alikuja Uingereza kama mkimbizi kutoka Somalia akiwa na wazazi wake.

Hata hivyo, mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 39 sasa anasema wazazi wake hawajawahi kuishi Uingereza.

"Nikiwa na miaka 4, baba yangu aliuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, unajua kama familia tulisambaratishwa. Nilitenganishwa na mama yangu, na nililetwa Uingereza kinyume cha sheria kwa jina la mtoto mwingine aitwaye Mohamed Farah," alisema.

Alazimishwa kufanya kazi kama mhudumu mtoto

Farah aliiambia BBC kwamba alidhani alikuwa anakwenda Ulaya kuishi na ndugu zake.

Alikumbuka kupitia ukaguzi wa paspoti nchini Uingereza kwa jina la Mohamed akiwa na mwanamke asiyemjua alipokuwa na umri wa miaka 9.

Soma pia: Mo Farah aivunja rekodi ya Moorcroft

Baada ya kuwasili Uingereza, mwanamke huyo alimchukua nyumbani kwake katika mji wa magharibi mwa London wa Hounslow borough na kuchana karatasi iliyokuwa na mawasiliano na ndugu zake.

Familia ya mwanamke huyo haikumruhusu kwenda shuleni hadi alipofikisha umri wa miaka 12.

"Kwa miaka kadhaa niliendelea kujizuwia, lakini huwezi kujizuwia kwa muda mrefu," alisema. "Mara nyingi ningejifungia bafuni na kuanza kulia. Kitu pekee nilichoweza kufanya kusahau hali hii ilikuwa kutoka nje na kukimbia."

Britischer Olympiasieger Mo Farah
Mo Farah ameishindia Uingereza medali nne za dhahabu za Olimpiki, wa kwanza kufanya hivyo.Picha: Owen Humphreys/PA Wire/dpa/picture alliance

Hatimaye Farah alimwambia mwalimu wake wa viungo, Alan Watkinson, alichokuwa anakabiliana nacho. Kisha Watkinson aliwasiliana na idara ya huduma za kijamii iliyomsaidia kutafuta familia ya kumlea katika jamii ya Wasomali.

Soma pia: Mo Farah ashindwa kung'ara katika marathon

Farah alitambuliwa kama raia wa Uingereza mnamo mwaka 2000.

Kufuatia ufichuzi huo wa Jumanne, msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza alisema, "Hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa kwa vyovyote dhidi ya Sir Mo."

'Nataka kujihisi kawaida'

Katika filamu hiyo, Farah alisema walikuwa watoto wake waliomhamasisha kueleza ukweli kuhusu historia yake.

Soma pia: Mo Farah ashinda dhahabu ya mita 10,000

"Nimeitunza kuwa siri kwa muda mrefu sana, imekuwa ngumu kwa sababu hutaki kuikabili na mara nyingi watoto wangu wananiuliza maswali," Baba, inakuwaje hili?' Na wakati unapata jibu kwa kila kitu, lakini huna jibu kwa hilo," alisema.

"Hiyo ndiyo sababu kuu katika kuelezea simulizi yangu, kwa sababu nataka kujihisi kawaida na siyo kuhisi kama vile unajishikiza juu ya jambo," aliongeza.

Mnamo mwezi Mei, Farah alisema kazi yake ya riadha huenda ikafikia tamati baada ya kumaliza mbio za marathon za London za mita 10,000 akiwa mshindi wa pili na kuondoa uwezekano wa kushiriki mashindano ya ubingwa wa dunia ya mwezi huu.

Hata hivyo, anapanga kukimbia marathon kwa mara ya kwanza tangu 2019, atakaposhiriki mbio za Marathon jijini London Oktoba ijayo.

Chanzo: AFP, AP, Reuters