1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanaume aliejaribu kumuuwa rais wa Mali afariki jela

Iddi Ssessanga
26 Julai 2021

Mwanaume alietuhumiwa kwa kujaribu kumuua kiongozi wa Mali Assimi Goita, mtu aliehusika na mapinduzi mawili katika muda wa chini ya mwaka mmoja, amefariki akiwa kizuwizini. Mshukiwa huyo alikamatwa siku ya Eid al-Adha.

https://p.dw.com/p/3y5As
Mali Bamako | Messerangriff auf Übergangspräsident | Assimi Goita
Picha: Emmanuel Daou/AFP/Getty Images

"Wakati wa uchunguzi....afya yake ilidorora" na alilazwa hospitali, lakini "kwa bahati mbaya amefariki," ilisema serikali katika taarifa na kuongeza kwamba uchunguzi umeagizwa mara moja kubaini sababu ya kifo chake.

Mwanaume aliyejihami kwa kisu alimrukia Goita baada ya swala ya Eid al-Adha siku ya Jumanne, kulingana na ripota wa shirika la AFP aliekuwepo eneo la tukio. Goita aliondolewa mara moja na kikosi chake cha usalama, na baadae alijitokeza kwenye televisheni ya taifa kusema kwamba alikuwa anaendelea vyema, na kupuuza umuhimu wa shambulio hilo.

Soma pia: Rais wa mpito wa mali yuko salama baada ya shambulio

"Hiyo ni sehemu ya kuwa kiongozi, mara zote kunakuwa na matu wenye nia mbaya," alisema. "Kuna watu ambao wakati wote wanaweza kutaka kufanya mambi ili kuvunja utulivu."

Mshambuliaji wake, mwanaume alieonekana kijana akiwa amevalia jeans na fulana, alikamatwa kwenye eneo la tukio an kuchukuliwa na maafisa wa idara ya upelelezi ya Mali.

Mali Oberst Assimi Goita, Anführer der malischen Militärjunta
Kanali Assimi Goita aliapishwa kuwa rais wa mpito mwezi Juni.Picha: Francis Kokoroko/File Photo/Reuters

Mshukiwa hakufikishwa mbele ya mamlaka za kisheria, chanzo kimoja kilichoomba kutotajwa jina kililiambia shirika la AFP siku ya Jumapili. Utambulisho wake haukuwekwa wazi, lakini kamishna Sadio Tomada alisema Jumanne jioni kwamba alikuwa mwalimu, bila kutoa ufafanuzi.

Waendesha mashtaka walikuwa wamefungua uchunguzi juu ya tukio hilo. Siku ya Jumapili, serikali ilisema kifo cha mshukiwa huyo hakikuwa kizingiti katika muendelezo wa uchunguzi, "hasa kwa sababu ushahidi wa awali na upelelezi uliokusanywa vinaonyesha kwamba halikuwa tukio la kipekee."

Shambulio hilo limehitimisha miezi kadhaa ya machafuko katika taifa ambako utulivu ni jambo la nadra tangu lipate uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960.

Goita ni nani hasa?

Goita, kanali wa kikosi maalumu alieko katika umri wa miaka 30, aliongoza mapinduzi Agosti mwaka jana dhidi ya rais aliechaguliwa Boubacar Keita baada ya wiki kadhaa za maandamano ya kupinga rushwa na kushindwa kushughulikia uasi wa wapiganaji wa Kiislamu.

Soma pia: Mahakama ya Mali yamtangaza Goita rais wa mpito

Utawala wa kijeshi, kufuatia shinikizo la kimataifa, ulikabidhi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia ambayo iliahidi kurejea utawala wa kiraia Februari 2022.

Lakini mwishoni mwa Mei, Goita, ambaye alikuwa makamu wa rais katika serikali ya mpito, alimpindua rais Bah Ndaw na waziri mkuu Moctar Ouane, akisema walitaka "kuhujumu" makabidhiano.

Mali Bamako | Messerangriff auf Übergangspräsident | Assimi Goita
Mshukiwa akisinfikizwa na maafisa wa usalama baada ya washambuliaji kujaribu kumuua rais wa mpito Kanali Assimu Goita.Picha: Emmanuel Daou/AFP/Getty Images

Mnamo Juni, Goita akiwa rais wa mpito, serikali mpya ilitangazwa, ambapo wanajeshi walipewa nafasi muhimu. Baada ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya ECOWASkuongeza shinikizo, Goita aliahidi kwamba serikali itatekeleza ahadi zote na kuitisha uchaguzi wa kuaminika, wa haki na wa wazi."

Majirani za Mali na washirika wamekuwa wakiwafuatilia mzozo huo kwa wasiwasi, wakihofia athari kwa juhudi za kuzuwiwa uasi wa wapiganaji ambao unaenea katika kanda nzima ya Sahel.

Kampeni hiyo ya umuagaji damu ilianza kaskazini mwa Mali mwaka 2012, na tangu wakati huo imesambaa nchini Burkina Faso, Mali na Niger. Maelfu ya wanajeshi na raia wameuawa na mamia kwa maelfu wameyakimbia makazi yao.

Ufaransa ambayo ndiyo inaongoza operesheni dhidi ya wapiganaji, imekosoa hasa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali. Ilisitisha ushirikiano wake wa kijeshi baada ya mapinduzi ya pili, na kisha ikatangaza kupunguza ujumbe wake wa Barkhane wenye watu 5,100.