1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Gaza-Jengo la shirika la misaada ya binadamu lashambuliwa.

Eric Kalume Ponda15 Januari 2009

Tunaanza na hali ya mashariki ya kati ambapo Mashirika ya misaada ya binadamu yanayohudumu katika eneo la vita la ukanda wa Gaza, kwa mara nyingine yamesimamisha shughuli zao katika eneo linalokumbwa na vita.

https://p.dw.com/p/GZC4
Mji wa Gaza ukiteketea kufuatia shambulizi la IsraelPicha: AP


Imeripotiwa Moto mkali bado unaendelea kuteketeza ghala la shirika la misaada la Umoja wa mataifa kufuatia shambulizi la wanajeshi wa Israel katika makao ya shirika hilo mjini wa Gaza.Kadhalika mashambulizi zaidi yamefanywa katika hospitali na jengo linalotumiwa na mashirika ya habari ya kimataifa huku Israel .


Kwa mujibu wa maafisa wa shirika la huduma za binadamu la Umoja wa mataifa, misaada ya madawa na chakula vimeteketezwa na moto huku wanajeshi hao wakidaiwa kutumia mabomu ya kamikali ya Fosiforasi wakati wa oparesheni hiyo.


Mbali na misada ya binadamu jengo hilo pia ni hifadhi kubwa ya mafuta yanayotumiwa kuendesha shughuli za mashirika hayo mjini Gaza. Msemaji wa shirika la UNRWA Chris Gunnes, anasema kuwa jengo hilo pia ni hifadhi ya wakimbizi 700 wa Kipalestina waliokimbilia usalama wao.


Katika shambulio jingine, wanajeshi wa Israel walirusha kombora katika jengo linalotumiwa na waandishi wa habari wa kigeni mjini Gaza na kuwajeruhiwa waandishi wawili wa habari ambao yasemekana wako hali mahututi.


Pia hospitali ya Al-Quds inayotumiwa na shirika la msalaba mwekundu haikusazwa wakati wanajeshi hao wa Israel walipokuwa wakifanya operesheni hiyo katika mitaa ya mji wa Gaza.

Waandishi wa habari waliokuwemo kwenye jengo hilo wanasema kuwa Israel ilirusha kombora katika jengo hilo la ghorofa 13 la Al-Shurouq lililoko kati kati mwa mji wa Gaza.


Maelfu ya wakaazi wa mitaa ya mji wa Gaza wametoroka makaazi yao kufuatia mashambulio hayo ya jeshi la Israel

katika eneo la Tel Hawwa ndani ya mji wa Gaza.


Isreal kupitia msemaji wake Mark Regev inakanusha kuhusika na shambulizi katika makao ya mashirika ya misaada ya binadamu UNRWA,ikisema kuwa inaheshimu na kufahamu maeneo yote yanayotumiwa na mashirika yanayotoa huduma za binadamu katika eneo hilo, na shambulizi hilo limetekelezwa na Hamas.


Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak ameomba msamaha kwa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon.


Katibu mkuu huyo ambaye yuko mjini Tel Aviv kutafuta kusitishwa kwa mapigano hayo alishtumu vikali shambulio hilo alitaka uchunguzi zaidi ufanywe kuhusiana na tukio hilo.


Kadhalika waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown alisema kuwa kitendo hicho cha Israel hakiwezi kukubaliwa na jamii ya kimataifa.


Katika ujumbe wake kamishna wa huduma za binadamu wa Umoja wa ulaya Louis Michel alihuzunishwa na kitendo hicho cha Israel kushambulia makao ya Umoja wa mataifa.


Wakati huo huo mjumbe wa Israel kwenye mpango wa amani unaoongozwa na Misri Amos Gilad ambaye amewasili mjini Cairo, alifanya mashauriano na mpatanishi aliyeteuliwa na Misri kuongoza mashauriano hayo Omar Suleiman baada ya kuchunguza mapendekezo yaliyowasilishwa na wajumbe wa chama cha Hamas kabla ya kuiarifu serikali yake.

Mpango huo ulioanzishwa Januari 6 unahimiza kukomeshwa kwa mapigano mara moja, kuondoka kwa wanajeshi wa Israel katika ardhi ya Gaza na kufunguliwa kwa maeneo ya mpakani.


Lakini Israel inasema kuwa watakubali mpango huo iwapo baadhi ya masharti yaliyotolewa yataondolewa.

Hadi kufikia sasa jumla ya Wapalestina 1,055 wameuawa, 670 wakiwa raia nayo Israel ikipoteza wanajeshi 10 na raia 3 katika vita hivyo.



Ponda-Afp