1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wademocrat wauzidisha mzozo wao na Trump

9 Mei 2019

Kamati ya sheria ya Bunge la Marekani imepiga kura kumuwajibisha Mwanasheria Mkuu William Barr kwa kulidharau bunge, baada ya kukaidi agizo la kutoa ripoti isiyohaririwa ya uchunguzi wa Urusi kuingilia uchaguzi Marekani.

https://p.dw.com/p/3IDMT
USA | Justizminister William Barr | Washington
Picha: Reuters/File Photo/J. Ernst

Uchunguzi huo ulifanywa na mchunguzi maalumu Robert Mueller.

Kura hiyo ya Jumatano ilihitimisha siku iliyoshuhudia mzozo unaozidi kuongezeka baina ya Wademocrat na rais Donals Trump ambaye kwa mara ya kwanza katika uongozi wake alitaja msingi wa fursa ya pekee anayokuwa nayo rais, akidai ana haki ya kuzuia wabunge wasiipate ripoti nzima ya uchunguzi wa Mueller kuhusu Urusi kumsaidia katika uchaguzi uliopita.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Jarrold Nadler amesema hatua ya wizara ya sheria ya Trump ni ishara mpya iliyo wazi ya rais huyo kulinyima bunge haki yake ya kikatiba ya uangalizi kwa uongozi.

Trump ni kama dikteta

"Hii tuliyochukua leo ilikuwa hatua kubwa sana, kumpata na hatia ya kutotii bunge Mwanasheria Mkuu wa Marekani. Hatupendelea kufanya hivi ila hatuna namna. Mwanasheria Mkuu Barr amethibitisha kwamba yeye ni mwanasheria wa Rais Trump na si mwanasheria mkuu wa Marekani, kwa kuudanganya umma mara mbili kuhusiana na yaliyomo katika ripoti ya Mueller," alisema Nadler.

USA Mueller Bericht l  Justizausschuss des Senats l Chairman Jerry Nadler
Mwenyekiti wa kamati ya sheria Jerry NadlerPicha: picture alliance/newscom/M. Theiler

Nadler amesema hatua ya Trump ya kulizuia bunge katika kila uchunguzi ni kama udikteta ambao hauwezi kukubalika. Lakini mbunge huyo hakutoa jawabu alipoulizwa kuhusiana na kuzindua mchakato wa kujaribu kumuondoa madarakani Trump.

Trump ambaye atakuwa anatafuta kuchaguliwa kwa mara ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2020 amezuia chunguzi kadhaa zinazofanywa na wabunge wa chama cha Democratic, kama ripoti hiyo ya Mueller, ulipaji wake wa kodi na rekodi zake za zamani za kifedha.

Trump Jr amewahi kutoa ushahidi mbele ya kamati hiyo

Wakati huo huo Kamati ya ujasusi ya seneti inayoongozwa na Warepublican nchini humo imechukua hatua ya kushangaza ya kumuita mwanawe Trump, Donald Trump Junior, kutoa ushahidi kama sehemu ya uchunguzi wake wa Urusi kuingilia uchaguzi uliopita wa Marekani.

Donald Trump und Mike Pence
Rais Donald TrumpPicha: picture-alliance/AP/S. Walsh

Trump Junior mwenye umri wa miaka 41 amewahi kutoa ushahidi faraghani mara moja katika kamati hiyo na aliulizwa kuhusu mkutano aliohudhuria katika jengo la Trump tower pamoja na maafisa wengine wa kampeni ya Trump na wakili mmoja wa Urusi Juni 9 mwaka 2016.

Wakuu wa kamati hiyo hawakuthibitisha ni kipi wanachotaka kujadili na mwanawe Trump wa kwanza ambaye kwa sasa ndiye anayeongoza makampuni ya Trump.