1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yawafukuza Waafghanistan wasio na vibali

31 Oktoba 2023

Idadi kubwa ya Waafghanistan wamefurika kwenye malori na mabasi nchini Pakistan, ili kurejea nchini mwao kabla ya kukamilika kwa tarehe ya mwisho iliotolewa kwa wale wasio na vibali vya kuishi nchini humo.

https://p.dw.com/p/4YFsR
Malori yaliowabeba Waafganistan yakiwa mpakani Torkham, Pakistan, yakisubiri kuvuka kuingia Afghanistan
Malori yaliowabeba Waafganistan yakiwa mpakani Torkham, Pakistan, yakisubiri kuvuka kuingia AfghanistanPicha: Muhammad Sajjad/AP Photo/picture alliance

Pakistan ilitangaza Novemba mosi ni siku ya mwisho kwa wahamiaji wote wasio na nyaraka za kisheria ikiwa ni pamoja na zaidi ya Waafganistan milioni moja kuondoka nchini humo au kuondoshwa kwa lazima.

Kampeni hiyo yakuwafukuza wahamiaji wasio na vibalirasmi imeibua shutuma chungu mzima kutoka kwa mashirika ya Umoja wa mataifa, mashirika ya haki za binadamu na utawala unaoongozwa na Taliban nchini Afhganistan.

Maafisa wa Pakistan wameendelea kuonya kwamba watu ambao wapo nchini humo kinyume na sheria watakamatwa na kufukuzwa baada ya oktoba 31.

Kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa zaidi ya Waafghanistan milioni mbili wanaishi nchini humo bila ya vibali na takriban 600,000 kati yao walikimbia baada ya Taliban kuchukua madaraka mnamo 2021

Soma pia:.Pakistan kuwafurusha wahamiaji mwezi ujao 

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch siku ya Jumanne, limeishutumu Pakistan kwa kutumia vitisho, kuwanyanayasa na kuwaweka kizuizini ili kuwalazimisha watafuta hifadhi wa Afganistan wasio na vibali kurejea nchini mwao.

Aidha shirika hilo limetoa wito kwa mamlaka ya Pakistan kusitisha zoezi hilo na badala yake kushirikiana na shirika la Umoja wa mataifa la kushughulikia wakimbizi UNHCR kuwasajili watafuta  hifadhi wasio na vibali.

Pakistan: Hatuwalengi Waafganistan ni wahamiaji wasio na vibali

Mamlaka ya Pakistan inasisitiza kuwa haifanyi kampeni hiyo kuwalenga waafghanistan, lakini kampeni hiyo inafanyika huku mahusiano baina ya majirani hao yakizorota.

Islamabad inaishutumu Kabul kwa kuwafumbia macho wapiganaji washirika wa Taliban ambao wanapata hifadhi nchini Afghanistan na kuendesha mashambulizi nchini Pakistan.

Waafganistan wakiwa kwenye lori wakisafiri kuelekea katika mpaka wa Torkham, Pakistan kuvuka kuingia Afghanistan
Waafganistan wakiwa kwenye lori wakisafiri kuelekea katika mpaka wa Torkham, Pakistan kuvuka kuingia AfghanistanPicha: Muhammad Sajjad/AP Photo/picture alliance

Baadhi ya watafuta hifadhi ambao wameishi Pakistan kwa zaidi ya miongo mitatu wanasema hawana chaguo ispokuwa kutii agizo la amamalaka, wanarejea Afganistan.

Wanasema wameishi nchini humo kwa miongo kadhaa na wengine wamezaliwa nchini humo na maisha yalikuwa mazuri lakini tangazo la kampeni hiyo limewavunja moyo.

"Tumeamua kuondoka na kurudi kwetu ili kuepusha kudharauliwa, hivi ndivyo inatokea Karachi na miji mingine." Alisema  Shafique Ullah ambae ni miongoni mwa wahamiji ambao wameishi Pakistan kwa miaka zaidi ya 45.

Soma pia:Taliban yakanusha madai ya Pakistan kuwa kundi hilo linafanya mashambulizi kwenye mipaka

Maafisa wa Pakistan wanasema vivuko vya Torkam na Chaman vitasalia wazi hadi saa nne usiku ili kuruhusu wale ambao wamefika katika maeneo hayo kuvuka na kuondoka nchini humo. Zaidi ya Waafghanistan 200,000 wamerejea nchini mwao tangu tangazo la kampeni hiyo. 

Ukandamizaji huo pia umewatia wasiwasi maelfu ya Waafghanistan nchini Pakistan wanaosubiri kuhamishiwa nchini Marekani baada ya kukimbia nchini mwao punde tu Taliba ilipochukua madaraka, chini ya mpango maalumu wa wakimbizi.

Mwanadiplomasia wa Marekani, ambae hakutaka kutajwa jina alisema mpango huo wa Washington unalenga kuwezesha makazi salama na kuwahamisha zaidi ya Waafghanistan 25,000 wanaostahiki nchini Pakistan hadi Marekani.
 

Mapango yawahifadhi wasio na makaazi Pakistan