1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yakabiliwa na baa la njaa

3 Julai 2014

Shirika la Msaada, Disasters Emergency Committee (DEC) limeonya kuwa Sudan Kusini itakabiliwa na baa la njaa wiki chache zijazo ikiwa hakutatolewa haraka kiasi kikubwa cha fedha za kununulia chakula cha msaada.

https://p.dw.com/p/1CUsN
Maelfu ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini wamemiminika nchini Ethiopia wakikwepa matatizo nyumbani kwao
Maelfu ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini wamemiminika nchini Ethiopia wakikwepa matatizo nyumbani kwaoPicha: Reuters

Katika ripoti yake ya jana jioni, shirika hilo ambalo linayajumuisha mashirika makubwa 13 ya msaada, imeelezwa kuwa ikiwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vitaendelea, na wito wa fedha zaidi za msaada ukapuuzwa, maeneo kadhaa ya taifa hilo changa zaidi duniani yatakabiliwa na janga la nja ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.

Maelfu ya watu wamekwishauawa katika vita hivyo vilivyoanza Desemba mwaka jana, huku zaidi ya milioni 1.5 wakiwa wamelazimika kuyahama makazi yao. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi UNHCR limesema kiasi cha fedha lilichonacho ni sawa na asilimia 40 ya mahitaji yake kununulia chakula cha kutosha kwa wakimbizi. Nakisi iliyopo katika bajeti ya shirika hilo ni ya takribani dola bilioni moja.

Mkuu wa DEC Saleh Saeed kuna kitisho kilicho dhahiri katika maeneo mengi, kinachoashiria kwamba mamilioni ya watu wataathiriwa pakubwa na upungufu huo wa chakula.

DEC inasema matatizo yanaweza kukithiri kuanzia mwezi August, 2014
DEC inasema matatizo yanaweza kukithiri kuanzia mwezi August, 2014Picha: Reuters

Vigezo vya kutokea kwa janga

Kulingana na viwango vya Umoja wa Mataifa, hali ya ukosefu wa chakula hugeuka janga pale asilimia 20 ya wakazi wa eneo fulani wanapokuwa wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, kiwango cha utapiamlo kikiwaathiri asilimia 30 ya wakazi, na ikiwa kutakuwa na vifo vya watu wawili kila siku, katika eneo la wakazi elfu 10.

Ingawa mvua za msimu huu wa kilimo zinatarajiwa kuwa za kawaida au pungufu kidogo ya kiwango cha kawaida, Umoja wa Mataifa umesema sababu ya ukosefu wa chakula haina uhusiano na matatizo ya hali ya hewa, bali na mapigano baina ya serikali na waasi.

Mashirika yaliyo ndani ya DEC ambayo ni pamoja na Oxfam, Tearfund na Save the Children, yana kiasi cha fedha ambacho hakifiki hata nusu ya mahitaji yake kuweza kuzuia Sudan Kusini isikabiliwe na baa la njaa.

Vita ndilo tatizo

Uhasama baina ya rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar umesababisha kuenea kwa matatizo makubwa katika jamii.

Shirika la Umoja wa Mataifa WFP kwa ajilia ya Msaada wa Chakula limesema kwamba idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini inaendelea kumiminika nchini Ethiopia wakikimbia matatizo nchini mwao. Abdou Dieng ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo amesema kuwa tayari wakimbizi 158, 000 kutoka Sudan Kusini wamekwishawasili nchini Ethiopia tayari.

Wakati wasudan kusini wakiendelea kuteseka, serikali na waasi bado wanang'ang'ania ushindi wa kivita
Wakati wasudan kusini wakiendelea kuteseka, serikali na waasi bado wanang'ang'ania ushindi wa kivitaPicha: Reuters

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba kila wiki Ethiopia hupokea wakimbizi zaidi ya 1,500. Umoja huo umeonya kwamba ikiwa hali hii itaendelea, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu Ethiopia itakuwa ikiwapa hifadhi wakimbizi zaidi ya laki tatu kutoka Sudan Kusini.

Na hali haiboreka nchini Sudan Kusini, kutokana na vita vinavyoendelea. Rais Salva Kiir na mpinzani wake Riek Machar walitia saini makubaliano ya tatu ya kusitisha uhasama, na kukubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika muda wa siku sitini, lakini bado vita vinaendelea licha ya makubaliano hayo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef