1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaadhimisha miaka 20 tangu kufariki Nyerere

14 Oktoba 2019

Tanzania siku ya Jumatatu imeadhimisha miaka ishirini tangu kufariki kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na safari hii sherehe za maadhimisho hayo zimefanyika huko Lindi.

https://p.dw.com/p/3RFPr
Julius Nyerere erster Präsident Tansania
Picha: Getty Images/AFP

Rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli amekemea vikali suala la rushwa nchini humo na kutaka wahusika wawachukulie hatua wale wanaopatikana na hatia.

Wananchi kutoka kona mbalimbali ya nchi wanaungana kwa pamojawakikumbuka miaka 20 baada ya muasisi wa taifa  la  Tanzania  Mwalimu  Julius Kambarage Nyerere kwa kuangalia mwelekeo wa taifa lao tangu kuondokewa kwa muasisi wake huyo.

Wamekuwa wakiungana kwa njia za majadiliano kwa kushiriki makongamano ya wazi, kuendesha mijadala kupitia njia ya vyombo vya habari na kushiriki majadiliano yasiyo rasmi kupitia majukwaa mbalimbali kama vile mitandao ya kijamii.

Mwalimu Nyerere alikuwa mtu muungwana

Katika makongamano mengi yaliyofanyika, wazungumzaji wamekuwa wakimtaja Mwalimu Nyerere kama kiongozi aliyedhubutu, mpenda watu mwadilifu na aliyependa kuheshimu utawala wa sheria.

Tanzania Dar es Sallam Jakaya Kikwete ehemaliger Präsident von Tanzania
Rais wa zamani wa Tanzania Jakaya KikwetePicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Hilo limethibitishwa pia, na Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete ambaye maelezo yake aliyoyatoa wakati akizungumza kwenye kongamano moja yamezua mjadala na kuzalisha msamiati mpya katika medani za siasa za Tanzania.

Rais Kikwete alimtaja Mwalimu Nyerere kama mtu muungwana aliyejawa na ubinadamu na kwa maana hiyo aliwasihi wanaotaka kumuenzi kwa vitendo basi wasiwe viongozi wa kujimwambafai akimanisha kufanya mambo katika hali ya umwamba mwamba.

Ingawa mijadala inayoendelea sasa ni ile inayoangazia urithi wa Baba wa Taifa kwa Tanzania, lakini suala la utawala wa kisheria na upanuaji wa demokrasia nayo pia hujadaliwa.

Akizungumza kwenye kongamano moja kabla ya maadhimisho haya ya leo, mwanasiasa wa siku nyingi, Getruda Mongella alisema suala la ustawishaji wa demokrasi halipaswi kupuuzwa.

Watanzania wanapaswa kujifunza mengi

Kwa siku nzima ya leo, vyombo vya habari kama vile vituo vya televisheni, redio vimekuwa vikipeperusha ujumbe wa sehemu za hotuba za Mwalimu Nyerere alizozitoa wakati wa kupigania uhuru, akiwa madarakani na baada ya kung'atuka kwenye uongozi.

Präsident John Magufuli aus Tansania
Rais John Pombe Magufuli wa TanzaniaPicha: Reuters/T. Mukoya

Msomi wa siku nyingi, Dr Azalia Lwaitama anasema wakati Watanzania wakiwa kwenye kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa taifa, kuna mengi wanapaswa kujifunza kutoka kwake.

Mwalimu Nyerere ni moja ya viongozi wachache wa afrika waliokuwa na ndoto ya kutaka kuingunisha afrika kuwa kitu kimoja. Pia, alikuwa mkali kwa chama alichokiasisi CCM na kwa viongozi wa serikali.

Mbali ya kuwa mstari wa mbele katika kupigania ukumbozi wa kusini mwa afrika, mwalimu Nyerere pia alikuwa msemaji mkubwa wan chi za dunia ya tatu akipigania usawa na haki za kiuchumi.