1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi 2020: CCM yaanza kuvuna wabunge, madiwani bila kura

Mohammed Khelef
26 Agosti 2020

Kumekuwa na matukio ya wagombea kadhaa wa ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa Tanzania kuenguliwa katika mazingira ya kutatanisha na kuwapa nafasi wagombea wa CCM kupita kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika.

https://p.dw.com/p/3hWhM
Kassim Majaliwa, Premierminister von Tansania
Picha: Büro des Premierministers von Tansania

Hadi sasa, chama tawala nchini Tanzania (CCM) kimeshajikusanyia wabunge wapatao 20 waliotangazwa washindi kwenye majimbo yao hapo jana (Agosti 25) bila kupigiwa kura na wananchi. 

Wasimamizi wa uchaguzi kwenye maeneo hayo walisema kuwa wagombea wa vyama vya upinzani hawakukidhi matakwa ya kisheria na hivyo kuwaacha wa CCM pekee wakiwa na sifa halali za kuwa wagombea. 

Miongoni mwa wanasiasa mashuhuri waliopitishwa kwa mtindo huo, ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa jimbo lake la Ruangwa, Nape Moses Nnauye kwa jimbo la Mtama, Spika wa Bunge Job Ndugai kwa jimbo la Kongwa na Waziri wa Mambo ya Kigeni Palamagamba Kabudi kwa jimbo la Kilosa.

Kwenye orodha hii, wamo pia wafanyabiashara maarufu kama vile Ahmed Shabiby ambaye alitangazwa mshindi wa ubunge jimbo la Gairo kwa kile ambacho msimamizi alisema ni "wagombea wengine kurudisha fomu saa 11 jioni badala ya saa 10 jioni" na Abdulaziz Aboud kwa jimbo la Morogoro Mjini kwa kile ambacho msimamizi alisema ni makosa kwenye fomu za wagombea wengine. 

Yumo pia Hamis Taletale aliyepita ubunge jimbo la Morogoro Kusini Mashariki bila mshindani. Mbunge huyo mteule anayefahamika kwa umashuhuri wa Babu Tale ni meneja wa msanii Naseeb Abdul (Diamond Platnumz) na ni mara ya kwanza kwake kuwania ubunge.

Wapinzani wadai kuchezewa rafu

Ripoti zinasema baadhi ya wagombea wa upinzani walikumbana na matukio ya kutekwa, kuvamiwa na wengine kuenguliwa na wasimamizi wa uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali. Karibu vyama vyote vya upinzani vimekuwa vikitoa matamko ya kulaani na kukemea hali hiyo.

Tansania Wahlkampagne Tundu Lissu, Kandidat der Opposition
Makamu Mwenyekkiti wa CHADEMA na mgombea urais wa chama hicho, Tundu Lissu.Picha: Getty Images/AFP

Mbali na hilo, vyama hivyo vimeanza michakato ya kuyakatia rufaa maamuzi yaliyotolewa na wasimamizi wa uchaguzi wanaolalamikiwa kuziendea kinyume sheria zinazoSimamia uchaguzi huo.

Miongoni mwa vyama ambavyo vimetoa msimamo wa kusonga mbele; yaani kukata rufaa hiyo; ni pamoja na chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, ambacho baadhi ya wagombea wao wanadaiwa kuenguliwa katika mazingira ya kutatanisha.

Chama hicho kimeanza kukusanya taarifa kutoka kwa wagombea wake kwa shabaha ya kuhoji uhalali uliotumika kuwapiga kalamu nyekundu wagombea wake.

Hatua kama hiyo pia inatajwa kuchukuliwa na vyama vingine, kikiwamo Chama cha Wananchi (CUF), ambapo mkurugenzi wake wa uenezi na itikadi, Mohammed Ngulangwa, ameiambia DW kwamba wamevunjwa moyo na "namna wagombea wa upinzani walivyotendewa katika hatua ya mwisho ya urejeshaji wa fomu."

ACT Wazalendo yakumbwa na panga la NEC

Chama kingine cha upinzani ambacho wagombea wake wamekumbana na hali hiyo ni ACT Wazalendo, ambacho nacho kimedokeza uwezekano wa kukata rufaa na hii leo (Agosti 26) kilikuwa kimepanga kukutana na waandishi wa habari kuzungumzia mambo hayo hayo ya uchaguzi.

Bernard Membe
Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, Benard Membe.Picha: DW/E. Boniphace

Tayari mgombea wake wa urais, Bernard Membe, alishatoa kauli ya kulaani vitendo hivyo hapo jana (Agosti 25) mara tu baada ya kutangazwa kuwania nafasi hiyo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mjini Dodoma, ambapo alionya kwamba vitendo hivyo vinaweza kuitumbukiza nchi kwenye machafuko.

"Nimeshuhudia mataifa kadhaa ya Afrika yakiingia kwenye mapigano kwa sababu ya vitendo kama hivi vya kuwazuilia wananchi haki yao ya kuchaguwa mtu wamtakaye kuwaongoza kupitia chaguzi. Watawala wajuwe kuwa wana haki ya kuteuwa wagombea, lakini wenye haki ya uchaguzi ni wananchi, si wao," alisema Membe, ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Tanzania.

Rufaa mwisho saa 10:00 alasiri

Wahlen in Tansania I  Hamida Abdallah Huaeshi I Semistocles Kaijage I Hamida Abdallah Huaeshi
Mgombea urais kupitia chama cha CUF, Ibrahim Lipumba (katikati).Picha: DW/S. Khamis

Kumekuwapo na ripoti kuwa baadhi ya wagombea walioenguliwa kwenye mchakato huo walikosea kufuata vipengele kadhaa wakati wa ujazaji wa fomu zao za uteuzi.

Hata hivyo, mkurugenzi wa idara ya habari na elimu ya mpiga kura kwa umma wa NEC, Giviness Aswile, wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) alisema kuwa tume hiyo ilikuwa ikusubiri kupata ripoti kutoka kwa watendaji wake walioko mikoani.

"Tume huenda ikaanza kuzitathmini changamoto zote zilizojitokeza kutoka kwa timu yake iliyoko mikoani baada kupokea taarifa," alisema Aswile.

Kulingana na sheria ya uchaguzi, wagombea wote wenye nia ya kutaka kukata rufaa wanao muda wa kufanya hivyo kuanzia jana jioni hadi leo saa 10:00 jioni.

Maamuzi yanayotolewa na tume ya uchaguzi kuhusiana na rufaa zote zilizokatwa hayawezi kuhojiwa wala kupingwa na ngazi nyingine yoyote.

Imetayarishwa na George Njogopa/DW Dar es Salaam