1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Uchumi wa dunia wayumba - IMF

Mohammed Khelef
10 Oktoba 2023

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linasema makisio yake ya ukuwaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2023 hayajabadilika, ingawa limeonya kwamba uchumi huo unazidi kudorora wakati bei za bidhaa muhimu zikiendelea kupanda.

https://p.dw.com/p/4XMfn
USA IWF Pierre-Olivier Gourinchas
Mchumi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, Pierre-Olivier Gourincha (wa pili kutoka kushoto) anasema China lazima ifanye mageuzi ili ijikwamuwe na hali ngumu ya kiuchumi.Picha: Liu Jie/Xinhua/IMAGO

Ripoti ya Muelekeo wa Uchumi wa Ulimwengu iliyotolewa siku ya Jumanne (Oktoba 10) na IMF ilisema kwamba ukuwaji wa uchumi kwa mwaka 2023 ulikuwa unaendelea kusalia kwenye asilimia 3.0, lakini makisio yake kwa mwaka 2024 yameshuka hadi asilimia 2.9, ikiwa tafauti ya 0.1 na makisio ya mwezi Julai.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Marrakesh, Moroko, ambako shirika hilo liliitisha mkutano wake wa kila mwaka, mchumi mkuu wa IMF, Pierre-Olivier Gourinchas, alisema ukuwaji wa uchumi unaendelea kusalia kwenye kiwango cha chini na kisicho na uhakika.

Soma zaidi: Mkutano wa kila mwaka wa IMF na Benki ya Dunia wafanyika Afrika

"Upandaji wa bidhaa ambao ulikuwa umeshuka kwa kiasi mwaka jana, unatazamiwa kuendelea kusalia kwenye asilimia 6.9 mwaka huu, lakini utashuka kwa asilimia 5.8 ifikapo mwezi Julai mwakani." Alisema mchumi huyo wa IMF.

Kwa ushauri wa IMF, benki kuu katika mataifa makubwa zilipandisha viwango vya riba ili kuudhibiti upandaji bei wa bidhaa, hatua ambayo, hata hivyo, imepunguza kasi ya ukuwaji wa uchumi, lakini IMF inapingana na uamuzi wowote kulegeza sera hizo za kifedha.

Marekani ipo pazuri, China taabani

Kwa mujibu wa shirika hilo, uchumi wa Marekani - ambao IMF imeyapandisha makisio yake kutoka asilimia 1.8 hadi 2.1 - unaendelea vizuri zaidi kuliko wa mataifa mengine makubwa. Hata hivyo, utashuka hadi asilimia 1.5 mwakani.

 Joe Biden / Ukraine
Rais Joe Biden wa Marekani, nchi yake inafanya vizuri kwenye makisio ya ukuwaji wa uchumi.Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Kinyume chake, makisio ya uchumi wa China yanaonesha kwamba utashuka kwa miaka miaka miwili mfululizo kutokana na mzozo wa biashara ya majenzi unaoliandama taifa hilo la pili kwa nguvu za kiuchumi ulimwenguni.

Soma zaidi: Xi: Uhusiano wa Marekani na China ni muhimu kwa dunia

Uchumi wa China unatazamiwa kukuwa kwa asilimia 5 mwaka huu, kutoka asilimia 5.2 ulivyokuwa awali, na utashuka zaidi hadi asilimia 4.2 mwakani, kutoka asilimia 4.5 ilivyokuwa imekisiwa awali.

Gourinchas ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali ya China inapaswa kuchukuwa hatua kali na za haraka ili kurejesha imani ya sekta ya ujenzi, kulegeza masharti kwenye sera zake za kifedha na kutoa ruzuku kwa viwanda na sekta binafsi.

Ujerumani kuingia kwenye mdororo wa kiuchumi

Kwa upande wa Ujerumani, IMF ilisema kuna uwezekano mkubwa wa taifa hilo kubwa kabisa kiuchumi barani Ulaya kutumbukia zaidi kwenye mdororo wa uchumi.

Deutschland, Berlin | Bundeskanzler Scholz äußert sich zum Angriff auf Israel
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, nchi yake inaelekea kwenye mdororo mkubwa wa uchumi kwa mwaka 2023.Picha: Fabian Sommer/dpa/picture alliance

Hilo litaifanya Ujerumani kuwa nchi pekee kwenye kundi la mataifa saba yenye nguvu za kiuchumi duniani, G7, kujikuta kwenye hali ya kusinyaa uchumi wake.

Soma: Ujerumani kuwa nchi ya pekee barani Ulaya kuingia kwenye mdororo wa uchumi 2023

Uchumi wa Ujerumani unatazamiwa kuyumba kwa asilimia 0.5 mwaka huu, badala ya 0.3 ilivyokisiwa awali, na utakuwa kwa asilimia 0.9 mwakani badala ya makisio ya asilimia 1.3 yaliyotolewa na IMF mnamo mwezi Julai.

Kinyume na Marekani, ukanda unaotumia sarafu ya euro uliokuwa ukitegemea kwa kiwango kikubwa kuingiza nishati yake kutoka Urusi, umekuwa na hali mbaya zaidi kutokana na kupanda kwa bei za nishati kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Vyanzo: Reuters, AFP