1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda:Kiswahili lazima shule za msingi na sekondari

Admin.WagnerD6 Julai 2022

Wakati sherehe za maadhimisho ya siku ya Lugha ya Kiswahili duniani zikianza leo visiwani Zanzibar, serikali ya Uganda imetangaza kukifanya Kiswahili kuwa somo la lazima katika shule za msingi na sekondari.

https://p.dw.com/p/4Dkh5
Uganda | Yoweri Museveni während Interview
Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

Mbali na kufundishwa katika ngazi hiyo ya elimu kadhalika wanasiasa,watumishi wa umma na wanahabari wametakiwa kujifunza na kuitumia lugha hiyo ambayo wazungumzaji wake wanazidi kuongezeka ulimwenguni.

Akitangaza maamuzi ya baraza la mawaziri, waziri wa habari Dkt. Chris Baryomunsi amesema hata viongozi ikiwemo wanasiasa na watumishi wa umma watatakiwa kuwasilisha taarifa za serikali wakizingatia pia kutumia lugha ya Kiswahili.

Wadau wa kiswahili ambao wamekuwa wakishauri serikali kutumia lugha hiyo kwa muda mrefu wamesifu hatua hiyo ya serikali na kuongeza kuwa sasa wanalojukumu la kukisambaza kiswahili katika taifa hilo a Afrika Mashariki.

Soma pia:Vyombo vya habari na mustakabali wa Kiswahili

Mkuu wa kitivo cha lugha ya Kiswahili chuo kikuu cha Makerere Dkt Levi Masereka aliiambia Dw kwamba, jukumu hilo wamelipokea.

"Sisi walimu tumepewa kipaumbele na majukumu ndio kwanza yameanza" aliiambia Dw ikiwa ni muda mfupi tango kutolewa kwa tangazo la serikali.

Ongezeko la wasomi wa lugha hiyo laishawishi serikali

Kwa miaka kadhaa sasa , serikali ya Kampala imekuwa ikishikilia msimamo wake kwamba  haiwezi kufanya Kiswahili kuwa somo la lazima kutokana na uhaba wa walimu wa Lugha hiyo.

Katika kipindi cha miaka kumi sasa, vyuo vikuu ya vile vya walimu vimeweza kutoa walimu wengi wa lugha hiyo.

Wengine kadhaa wameendelea na kupata shahada za uzamili na uzamifu na wadau wana imani kuwa sasa kuna nguvu kazi ya kutosha kukidhi mahitaji ya kufundisha lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wao, raia wa kawaida wamekubali kwamba Kiswahili ni lugha muhimu kwa biashara na utangamano wao na raia wengine wa mataifa ya Afrika Mashariki.

Soma pia:Tanzania yataka Kiswahili kitambuliwe lugha ya asili ya Afrika

Wanaelezea kuwa Uganda imeachwa nyuma katika mawasiliano ya Kiswahili lakini sasa watajitahidi kujifunza.

Angalau walimu na wapenzi kadhaa wa Kiswahili wamesafirikwenda Zanzibar kushiriki katika sherehe za maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani.

Sherehe hizo zimeanza leo kwa kongamano na kilele ni hapo kesho tarehe 7 Julai iliyotangazwa rasmi na shirika la Umoja Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO.  

Kiswahili katika Sayansi na Teknolojia