1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yasema UKIMWI unaweza kumalizwa ifikapo 2030 ikiwa....

Iddi Ssessanga
1 Desemba 2023

Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya Ukimwi duniani, Umoja wa Mataifa umesema bado inawezekana kufikisha mwisho janga hilo kufikia mwaka 2030, lakini endapo tu jamii za huduma mashinani zitawezeshwa.

https://p.dw.com/p/4ZeS6
Kampeni ya kupambana na UKIMWI |Siku ya UKIMWI Duniani.
Umoja wa Mataifa unasema inawezekana bado kumaliza janga la UKIMWI ifikapo 2030.Picha: Saikat Paul/Pacific Press/picture alliance

Shirika la kupambana naUKIMWI la Umoja wa Mataifa, UNAIDS, lilisema katika Ripoti yake ya kila mwaka ya Siku ya UKIMWI Duniani kwamba majibu yanayoongozwa na jamii hayatambuliki, hayafadhiliwa ipasavyo na katika baadhi ya maeneo yanashambuliwa.

"Ujumbe wa ripoti hii ni wa matumaini makubwa. Ingawa dunia kwa sasa haiko katika njia ya kukomesha UKIMWI kama tishio la afya ya umma, inaweza kuendelea," ripoti hiyo ilisema.

Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza uliweka lengo mwaka 2015 la kukomesha UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo 2030.

Kuna watu milioni 39 duniani kote wanaoishi na VVU -- virusi vinavyosababisha UKIMWI. Kati yao, milioni 20.8 wako mashariki na kusini mwa Afrika na milioni 6.5 wako Asia na Pasifiki.

Lakini kati ya milioni 39, milioni 9.2 hawana matibabu ya kuokoa maisha.

Soma pia: UNAIDS inamatumaini yakumaliza UKIMWI ifikapo 2030

"Sheria na sera zenye madhara kwa watu walio katika hatari ya kuambukizwa VVU -- ikiwa ni pamoja na watu wanaofanya biashara ya ngono, wanaume wanaofanya ngono na wanaume, watu waliobadili jinsia na watu wanaotumia dawa za kulevya -- zinaweka jamii zinazojaribu kuwafikia kwa huduma za VVU katika tishio," UNAIDS ilisema.

Südafrika Welt-Aids-Tag 2016
Afrika Kusini ilizindua chanjo ya majaribio dhidi ya UKIMWI mnamo mwaka 2016, ambayo wanasayansi walikuwa na matumaini ya kumaliza janga hilo. Hata hivyo juhudi zinaendelea.Picha: Getty Images/AFP/M. Safodien

Shirika hilo lilisema programu zinazotolewa na mashirika ya kijamii yaliyo mstari wa mbele zinahitaji usaidizi kamili kutoka kwa serikali na wafadhili ili kumaliza janga la UKIMWI.

Karibu dola bilioni 20.8 zilipatikana kwa ajili ya programu za VVU katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati mwaka 2022, hii ikiwa ni pungufu ya dola bilioni 29.3 zinazohitajika kufikia 2025.

Gharama ya kila mwaka ya matibabu imeshuka kutoka dola 25,000 kwa kila mtu mwaka 1995 hadi chini ya dola 70 katika nchi nyingi zilizoathiriwa zaidi na VVU siku hizi. Ripoti hiyo ilisema ufadhili unaopitishwa kupitia jamii umepungua kutoka asilimia 31 mwaka wa 2012 hadi asilimia 20 mwaka wa 2021.

Soma pia:Tanzania yabadili gia mapambano dhidi ya Ukimwi

"Jumuiya siyo kikwazo: zinaangazia njia ya mwisho wa UKIMWI," mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima alisema.

Shirika hilo lilisema ukandamizaji dhidi ya makundi yaliyotengwa unazuia jamii zilizo mstari wa mbele kutoa huduma za kinga na matibabu ya VVU, huku ufadhili mdogo ukiwaacha wakihangaika kuendesha shughuli zao na kuwazuwia kutanuka.   

Kulikuwa na maambukizi mapya ya VVU milioni 1.3 duniani kote mwaka jana -- kutoka kilele cha milioni 3.2 mwaka 1995. Mwaka 2022, asilimia 86 ya watu wote wanaoishi na VVU walijua hali zao za VVU. Kati yao, asilimia 89 walikuwa wakipata matibabu. Na kati yao, asilimia 93 walipuguza kiwango cha virusi.

Afrika AIDS-Bekämpfung | Kenia
Wahamasishaji wa mapambano dhidi ya UKIMWI wakipuliza kondomu wakati wa 'olimpiki ya kondomu' ,jijini Nairobi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi 2021.Picha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

UNAIDS ilisema asilimia 53 ya watu wote wanaoishi na VVU walikuwa wanawake na wasichana. Botswana, Eswatini, Rwanda, Tanzania na Zimbabwe tayari zimefikia kile kinachoitwa malengo ya 95-95-95 katika kukabiliana na janga hili.

Hii ina maana kwamba asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao; Asilimia 95 ya wanaojua kuwa wana VVU wako kwenye matibabu ya kuokoa maisha ya kupunguza makali ya VVU; na asilimia 95 ya watu wanaopata matibabu ili kufikia ukandamizaji wa virusi -- na hivyo kuna uwezekano mdogo sana wa kuwaambukiza wengine.

Ripoti hiyo ilisema watu 630,000 walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI mwaka jana. Tangu kuanza kwa janga hili, watu milioni 85.6 wameambukizwa VVU na milioni 40.4 wamekufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI.

Siku ya UKIMWI Duniani, ilioanzishwa mwaka 1988 huadhimishwa kila tarehe Moja Desemba.

Nozi, mwanaharakati 'asiyejizuia' kuhusu masuala ya UKIMWI

Chanto: AFPE