1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa nchi Afrika wajadili maendeleo ya bara hilo

25 Julai 2023

Mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu rasilimali watu umeanza leo nchini Tanzania huku mada kubwa ni kuhusu namna bara hilo linavyoweza kuongeza uwekezaji katika eneo hilo kwa shabaha ya kurahakisha maendeleo.

https://p.dw.com/p/4ULYe
Äthiopien 60. Jahrestag der Afrikanische Union (AU)
Picha: Solomon Muchie/DW

Viongozi wa Afrika wanakutana kuzitupia macho changamoto zinazorudisha nyuma ustawi wa maendeleo jumla ya raslimali watu na kwamba mkutano huo unaangazia mwelekeo wa Umoja wa Afrika sambamba na malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Ajenda inayozingatiwa katika mkutano huu ni namna vijana waliotapakaa kote Afrika wanavyoweza kufunguliwa milango na kuchukua hatua za mbele katika kuendesha shughuli za kiuchumi na uzalishaji mali.

Soma pia:Afrika inaweza kudhibiti soko la malighafi za nishati safi?

Waandaji wa mkutano huo, serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia wameiweka mada juu ya uharakishaji ukuaji wa uchumi wa Afrika wakitilia mkazo vijana ambao wanachukua asilimia 60 ya idadi jumla ya watu barani Afrika inayofikia bilioni 1.2.

Vijana wakubwa na umasikini Afrika

Mkutano huo unabainisha kuwa kundi la vijana wanaendelea kuangukia katika lindi la umaskini huku baadhi yao wakikosa ujuzina maarifa ya uzalishaji mali.

Kwa maana hiyo mkutano huo unakusudia kuweka vipaumbele vitavyowezesha vijana wengi kunasuka hapo walipo na kuzikaribia fursa za kimaendeleo zinazochomoza barani humu.

Nchi tajiri kiuchumi zatakiwa kupunguza umasikini duniani

Akizungumza katika siku ya kwanza ya mkutano huo unaowakutanisha mawaziri wa kisekta kama vile fedha na maendeleo, Makamu wa Rais wa Tanzania Dr Philip Mpango alizihimiza nchi za Afrika kuweka ajenda ya pamoja itakayoainisha mipango na fursa kwa ajili ya kuwakwamua vijana na bara lenyewe kwa ujumla.

Soma pia:Viongozi wa Afrika Magharibi kujadili njia za kuhakikisha usalama nchini Mali, baada ya kufika mwisho kwa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Alisema idadi ya watu barani Afrika imekuwa ikongezeka kila mwaka, lakini ongezeko hilo haliendani na kiwango halisi cha ukuaji wa uchumijambo ambalo alisema linapaswa kutafutiwa jawabu kwa haraka.

Afrika iko mbioni kuanzisha ukanda huru wa soko la pamoja na nguvu kazi ya vijana ndiyo inayotajwa kuwa tegemeo la uzalishaji mali.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Stergomena Tax aliyezungumza kabla ya kuanza kwa mkutano huo alisema ingawa Afrika imekuwa ikipigiwa mfano kwa kuwa na nguvu kazi kubwa ya vijana, lakini nguvu kazi hiyo bado haijatumika ipasavyo.

Kwa maana hiyo alisema mwishoni mwa mkutano huo, wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika wataainisha mikakati kwa ajli ya kuliendeleza eneo hilo la vijana.

Mawaziri wa kisekta wamekuwa na mijadala inayoendelea kuangalia maeneo mbalimbali kabla ya hapo kesho wakuu wa nchi kuhitimisha mkutano huo kwa kuweka maazimio ya pamoja.

Tayari wakuu wa hao wa nchi wameanza kuwasili na ratiba iliyopatikana hivi punde inaonyesha baadhi ya wakuu wanaotazamiwa kuwasili jioni hii kutoka Kenya, Malawi, Sierra Leone, Msumbiji, Somalia, Misri, Ghana na Namibia.