1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM Tanzania yaanza mchujo wa wagombea ubunge

George Njogopa18 Agosti 2020

Chama tawala nchini Tanzania CCM kimeanza vikao vyake muhimu vya kuyatathmini majina ya wagombea wa nafasi za ubunge kuelekea uchaguzi mkuu huku tarehe ya kuchukua na kurejesha fomu kwa nafasi hizo ikizidi kukaribia.

https://p.dw.com/p/3h7eF
Tansania Wahlen 2020 | John Magufuli
Picha: picture-alliance/AP Photo

Kamati Kuu ya CCM inakutana katika wakati ambapo zimesalia siku saba tu kabla ya dirisha la kuchukua na kurejesha fomu hizo lifungwe rasmi na tume ya taifa ya uchaguzi.

Mara hii CCM kinakuwa chama cha mwisho mwisho kuyatangaza majina ya wagombea wake wa nafasi zote za ubunge, uwakilishi na udiwani hatua ambayo pengine ikawa mtego kwa wagombea wake wataoshindwa kupenya kwenye hatua hiyo ya mchujo.

Tansania Wahlen 2020
Wajumbe wa mkutano mkuu wa chama cha Mapinduzi wakihudhuria mkutano mjini Dodoma Julai, 11, 2020.Picha: imago images/Xinhua

Chama hicho kimesema majina ya wagombea wake yatajulikana siku ya Alhamisi na kwa maana hiyo wagombea waliotia nia na kufanya vizuri kwenye kura za maoni ambao huenda wakakatwa na chama hicho kwa sababu mbalimbali, watakuwa wamechelewa kuanza majadiliano na vyama vya upinzani kwa shabaha ya kuhamia huko na kuwania ubunge.

Soma pia Magwiji wabwagwa kura ya maoni ya CCM Zanzibar

Katibu mkuu wa CCM, Bashiru Ally amesema wagombea wote wa ubunge na uwakilishi waliotia nia kwenye uchaguzi wa mwaka huu wanapaswa kusalia kwenye majimbo yao ya uchaguzi wakisubiri kufahamu hatma yao.

Changamoto ya rushwa na vurugu

Chama hicho kinakabiliwa na mtihani wa kushughulikia vitendo vya rushwa na vurugu za hapa na pale zinazodaiwa kutawala wakati wa kura za maoni zilizofanyika kwa siku mbili katika wiki za hivi karibuni.

Soma pia Hussein Mwinyi kuwania urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM

Kumekuwa na sauti pamoja na picha za video zinazovuja zikiwaonyesha baadhi ya makada wa chama hicho wakipanga mikakati ya ugawaji wa fedha wakati wa kura za maoni.

Suala la makada wa CCM ambao walifanya vibaya kwenye kura za maoni lakini bado wanatajwa kuwa na ushawishi ndani ya chama ni jambo lingine ambalo wafuatiliaji wa masuala ya siasa wanasubiri kuona namna litavyoshughulikiwa na chama hicho.

Wakati CCM ikiingia kwenye vikao vyake muhimu vya maamuzi kwa wagombea wa ubunge na uwakilishi vyama vingine vikuu vya upinzani Chadema na ACT Wazalendo vimevuka kipengele hicho na wagombea wake wameendelea kujitokeza wakichukua fomu.

Soma pia CCM yaanza mchakato wa kuwachuja watia nia wa ubunge

Chama kingine cha upinzani cha NCCR Mageuzi bado hakijatangaza wagombea wake na duru za habari zinasema huenda kikafanya hivyo katika siku chache zijazo.

Mwandishi: George Njogopa