1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan lataka mazungumzo mapya masharti

Daniel Gakuba
20 Juni 2019

Baraza la kijeshi linalotawala Sudan limesema mazungumzo juu ya kuundwa kwa utawala wa mpito yanapaswa kuanza bila masharti yoyote, hiyo ikiashiria kuendelea kwa mvutano baina ya baraza hilo na viongozi wa upinzani.

https://p.dw.com/p/3KkVX
Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Jenerali Abdel-Fattah Burhan, mkuu wa baraza la kijeshi linalotawala SudanPicha: picture-alliance/AA

Mkuu wa baraza la kijeshi linalotawala Sudan Jenerali Abdel-Fattah Burhan amebainisha msimamo wa jeshi katika mazungumzo na wahudumu wa afya mjini Khartoum jana jioni, akisema jeshi halina masharti yoyote ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo kutafuta serikali ya mpito, na kuutaka upande mwingine pia kuacha kuweka masharti.

''Tunatoa wito mpya kwa wadau wote wa kisiasa, na tunawaambia, hakuna haja ya masharti kabla ya mjadala. Hakuna haja ya kurefusha matatizo kwa watu wetu.'' Alisema Jenerali Burhan, na kuongeza kuwa  watu wanahangaika, na sera  ya nje imeathirika kwa sababu Sudan haina serikali.

''Hatuwezi kubakia hivi muda mrefu zaidi. Mapinduzi mengine yanaweza kutokea kwa sababu ya mkwamo uliopo.'' Alionya.

Jaribio jingine la mapinduzi

Wiki iliyopita, baraza tawala la kijeshi lilisema tayari kumekuwepo jaribio jingine la kijeshi lililolenga kuliangusha baraza hilo, na kwamba makundi mawili ya maafisa wa kijeshi waliokuwa nyuma ya jaribio hilo yamekamatwa na kuwekwa kizuizini.

Sudan Khartum - Unruhen
Ukandamizaji wa jeshi kuvunja kambi ya waandamanaji uliuwa watu zaidi ya 120Picha: Getty Images/AFP

Jenerali Burhan amesema anatambua mchango wa vuguvugu la waandamanaji lijulikanalo kama ''Azimio la Uhuru na Mabadiliko'' FDFC kwa kifupi katika kuuangusha utawala wa Rais Omar al-Bashir, na kwamba lakini wanajua pia kuwa suluhisho linapaswa kuwa lenye kuwaridhisha Wasudan wote.

Viongozi wa vuguvugu la maandamano hawakupatikana mara moja kujibu rai hiyo ya jeshi, lakini mwishoni mwa juma lililopita, chama cha wasomi wa Sudan kilisema bado upinzani unashikilia unashikilia masharti uliyoyaweka kabla ya kukaa chini tena pamoja na wanajeshi.

Wanajeshi waondoke mitaani

BG Sudan Proteste
Waandamanaji wanadai serikali ya kiraia kuchukuwa madaraka nchini SudanPicha: Reuters

Masharti hayo ni pamoja na kuondolewa wanajeshi na wanamgambo kutoka mitaani, kurejeshwa kwa mtandao wa intaneti, na pia uchunguzi wa kimataifa katika ukandamizaji wa jeshi wa tarehe 3 Juni ambamo watu zaidi ya 120 waliuawa. Jeshi limekataa uingiliaji wa nje katika uchunguzi huo, na badla yake limeanzisha upelelezi wao wenyewe kubainisha ukweli juu ya kilichotokea.

Jenerali Abdel-Fattah Burhan ametetea kuvunjwa kwa kambi za waandamanaji mbele ya makao makuu ya jeshi, akisema ilikuwa dhahiri kwamba mawakala wa kigeni walikuwa wamejipenyeza kiintelijensia na kidiplomasia katika kambi hizo. Jenerali huyo alisema jeshi liliyavumilia hayo ili kuweza kuiondoa nchi katika mkwamo unaoikabili.

ape, afpe