1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Tanzania wamuomba rais kusimamia haki

Admin.WagnerD1 Aprili 2021

Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF nchini Tanzania Profesa Ibrahim Lipumba amshauri rais Samia Suluhu Hassan kijiwekea lengo la kufuata misingi ya demokrasia, kukuza uchumi na kutenda haki.

https://p.dw.com/p/3rTZE
Tansania Dar es Salaam | Partei CUF | Ibrahim Lipumba
Picha: DW/S. Khamis

Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF nchini Tanzania Profesa Ibrahim Lipumba amemshauri rais wa Jamhuri za Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kujiwekea lengo la kushinda tuzo za utawala bora inayotolewa na wakfu wa Mo Ibrahim kwa kufuata misingi ya demokrasia, kukuza uchumi na kutenda haki. 

Katika kipindi cha miaka mitano taifa hilo la Afrika Mashariki linatajwa kuporomoka katika viwango vya dunia vya demokrasia kutoka asilimia 64 wakati wa utawala wa awamu za nne wa Rais Jakaya Kikwete hadi asilimia 32 mwaka 2020.

Profesa Lipumba amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kutambua ukweli kwamba chaguzi za serikali za mitaa wa mwaka 2019 pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 hazikufuata misingi ya demokrasia, na kuweka mazingira mazuri ya siasa nchini humo, ili watu walumbane kwa hoja badala ya kutumia nguvu ya dola.

Soma Zaidi: Rais Samia Suluhu amsimamisha kazi mkurugenzi wa mamlaka ya bandari

Profesa Lipumba ameishauri serikali pia kuanzisha utaratibu wa utendaji wa kimkataba kwa mawaziri na watendaji wa juu serikalini, ambayo itakuwa inapitiwa kila baada ya mwaka ili ikitokea haja ya kutengua uteuzi wa mtendaji au kutumbua kama ilivyozoeleka, utumbuaji huo uwe unafuatana na utendaji kazi unaopimika.

Tansania Daressalam | Amtseinführung neue Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan akila kiapo cha kuwa rais wa Tanzania wiki mbili zilizopita.Picha: Stringer/REUTERS

Akizungumzia janga la corona linaloendelea kuitikisa dunia, profesa Lipumba amemtaka rais Samia Suluhu Hassan kurejelea msimamo wa awali wa hayati rais John Pombe Magufuli, kwa kutambua ukweli kwamba ugonjwa huo upo nchini na kushirikiana na shirika la afya duniani WHO, kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo na pia kupunguza gharama za upimaji ambazo amezitaja kuwa za juu sana na zisizohimilika na mwananchi wa kaiwada.

Hata hivyo mwenyekiti huyo wa chama cha CUF ambaye ameonesha matumaini makubwa kwa rais Samia Suluhu Hassan, ameunga mkono uamuzi wa hayati Magufuli wa kutoifunga nchi, akisema hali ya kiuchumi haingeweza kuruhusu ufungaji wa nchi, na kutolewa mfano wa nchi nyingine zilizochukuwa msimamo sawa, ikiwemo Sweden.

Soma Zaidi:Mfahamu Rais ajaye wa Tanzania Samia Suluhu Hassan 

Ameshauri pia wataalamu wa sayansi kupewa nafasi ya kufanya kazi zao kwa weledi na uhuru zaidi na kuyataja maradhi hayo kwa jina lake halisi badala ya kuyaita changamoto ya kupumua. Profesa Lipumba pia ameitaka serikali kukubali kuongozwa na sayansi katika utaratibu mzima wa utoaji chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Tayari mataifa jirani na Tanzania katika kanda ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya uchumi ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC yamepokea chanjo na yamo katika mpango wa kimataifa wa ugawaji wa chanjo, lakini Tanzania ilitoa msimamo wa kutokubali chanjo yoyote na bado haijatangaza kubadili msimamo huo hata baada ya kubadili uongozi kwa njia ya kikatiba.

Soma ZaidiMaoni: Vyeo vya Rais Samia visiwachanganye Watanzania

Hawa Bihoga