1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

Utawala wa kijeshi Mali wazuia shughuli za kisiasa

Sylvia Mwehozi
11 Aprili 2024

Utawala wa kijeshi nchini Mali umeamuru kusimamishwa kwa shughuli zote za kisiasa, ukisema kuwa hatua hiyo inahitajika ili kudumisha utulivu wa umma.

https://p.dw.com/p/4edpY
Mali | Kanali Assimi Goita,
Kiongozi wa kijeshi wa Mali Kanali Assimi Goita(katikati) akihudhuria sherehe za uhuru mjini Bamako mwaka 2023Picha: AP Photo/picture alliance

Utawala wa kijeshi nchini Mali umeamuru kusimamishwa kwa shughuli zote za kisiasa, ukisema kuwa hatua hiyo inahitajika ili kudumisha utulivu wa umma.

Akisoma amri iliyotolewa na kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita, msemaji wa serikali Kanali Abdoulaye Maiga amesema kuwa "kwa ajili ya utulivu wa umma, shughuli za vyama vya siasa na shughuli za kisiasa zimesimamishwa kote nchini, hadi pale itakapoamuriwa tena".Mali yaitaka MINUSMA kuondoka nchini humo mara moja

Amri hiyo inatolewa baada ya zaidi ya vyama 80 vya kisiasa na mashirika ya kiraia mnamo Aprili mosi, kutoa taarifa ya pamoja ya kutaka uchaguzi wa rais kufanyika "haraka iwezekanavyo" na kukomesha utawala wa kijeshi.

Mali | Assimi Goita
Kiongozi wa kijeshi wa Mali Kanali Assimi Goita, Picha: Malik Konate/AFP

"Tutatumia njia zote za kisheria na halali kurejesha utaratibu wa kawaida wa kikatiba katika nchi yetu," ilisema taarifa ya pamoja iliyotiwa saini zaidi na watu zaidi ya 20, ukiwemo muungano mkubwa wa upinzani na chama cha rais wa zamani aliyepinduliwa.

Nchi hiyo ya Afrika Magharibi imetawaliwa na wanajeshi tangu mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021, huku hali mbaya ya usalama ikichangiwa na mzozo wa kibinadamu na kisiasa.

Mnamo Juni mwaka 2022, serikali ya kijeshi ilisema uchaguzi wa rais utafanyika Februari na mamlaka kukabidhiwa kwa raia mnamo Machi 26. Lakiniuchaguzi huo uliahirishwa na utawala wa kijeshi haikutoa taarifa zaidi kuhusu nia yake.

Msemaji wa serikali Kanali Maiga alihalalisha kusimamishwa kwa shughuli za chama na "mijadala isiyo na maana" wakati wa jaribio la mjadala wa kitaifa mapema mwaka huu. Sauti za upinzani zimezuiwa kwa kiasi kikubwa chini ya utawala wa kijeshi.

Mali | Maandamano - Bamako
Waandamanaji wakiwa na bendera mjini Bamako wakipinga vikwazo ilivyowekewa Mali na ECOWASPicha: Florent Vergnes/AFP/Getty Images

"Vitendo vya uasi vya vyama vya siasa vinaongezeka," ilisema amri hiyo, iliyosomwa kwa waandishi wa habari na Kanali Maiga. Msemaji huyo aliongeza kuwa "hatuwezi kufanya mazungumzo muhimu kama haya... huku kukiwa na mkanganyiko na machafuko."

Utawala wa kijeshi ulipiga marufuku shughuli za muungano mpya wa upinzani mwezi Machi, ukitaja "vitisho vya kuvuruga utulivu wa umma". HRW:Wanajeshi Mali,Wagner wamefanya mauaji ya raia kiholelaMuungano huo ulikosoa sana utawala wa kijeshi na kupendekeza "njia mpya" kwa raia wa Mali ambao tangu mwaka 2012 wameshuhudia nchi hiyo ikiharibiwa na makundi yenye mafungamano na Al-Qaeda na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS.

Umoja wa Mataifa ulisema mwezi uliopita kwamba angalau mashirika manne yalivunjwa nchini Mali tangu Desemba 2023, yakiwemo makundi yanayohusiana na utawala bora, uchaguzi na upinzani.Umoja wa Mataifa wakabidhi moja ya kambi za mwisho kwa Mali

Tangu kunyakua mamlaka mnamo 2020, serikali ya kijeshi imefuta mashirikiano kadhaa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya na mkoloni wake wa zamani Ufaransa, na badala yake kuimarisha uhusiano wa karibu na Urusi.