1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa azikwa

Veronica Natalis
17 Februari 2024

Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Ngoyai Lowassa, umezikwa leo Jumamosi katika kijiji alikozaliwa kaskazini mwa taifa hilo wiki moja baada ya kuaga dunia akiwa na umri wa miaka 70.

https://p.dw.com/p/4cWeF
Tanzania, Monduli | Samia akiongoza mazishi ya Lowassa
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, akiweka udongo kwenye kaburi la Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Lowassa aliyezikwa kwenye kijiji alichozaliwa kaskazini mwa taifa hilo. Picha: Tanzania State House/Presidency

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ndiye aliwaongoza maelfu ya waombolezaji kwenye mazishi hayo ya Lowassa yaliyofanyika katika kijiji cha Ngarash kilichopo wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.

Katika hotuba yake mbele ya waombolezaji kabla ya mazishi, Rais Samia amemuelezea hayati Edward Lowassa, kuwa mwanasiasa aliyetumia nusu ya maisha yake kulitumikia taifa  hilo la Afrika Mashariki, na ameacha alama kubwa kutokana na utumishi wake aliosema "umetukuka."

Rais Samia pia ameeleza kwamba Lowassa alikuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za nchi hiyo, hali iliyomuwezesha kupata kura nyingi za urais kuliko mgombea mwingine yeyote wa chama cha upinzani tangu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi nchini Tanzania. 

Lowassa, kada wa siku nyingi wa chama tawala nchini Tanzania, CCM, alikihama chama hicho mwaka 2015 na kugombea kiti cha urais kupitia upinzani. Alipata asilimia 40 ya kura katika uchaguzi ambao John Magufuli, aliyewania kupitia CCM alishinda kiti cha urais kwa asilimia 58 ya kura.

Kiongozi wa upinzani ahoji historia ya Lowassa upinzani kufutwa kwenye wasifu

Akitoa salamu zake za rambi rambi, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha CHADEMA, Freeman Mbowe Mbowe, alionesha kusikitishwa na historia ya hayati Lowassa iliyosomwa Monduli, kutotaja kama mwanasiasa huyo aliwahi kugombea urais kupitia chama hicho cha upinzani.

 Freeman Mbowe na Edward Lowassa| Daressalam
Kiongozi wa chama cha upinzani Tanzania, CHADEMA, Freeman Mbowe akiwa na Edward Lowassa wakati mwanasiasa huyo na waziri mkuu wa zamani wa Tanzania alipojiunga na upinzani mwaka 2015.Picha: DW/Hawa Bihoga

Mbowe amesema  Lowassa alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA kwa miaka minne na mgombea urais na alileta kasi ya ukuaji wa demokrasia katika chama cha hicho kwa kuongeza idadi ya wabunge na madiwani akisema kuwa historia hiyo haipaswi kupuuzwa.

Ikumbukwe kuwa Lowassa alihamia CHADEMA siku chache baada ya jina lake kuenguliwa kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM mwaka 2015. 

Wakati huo alikuwa mwanasiasa aliyekuwa na jina na aliiamini angeweza kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho tawala kwenye uchaguzi huo uliokuja baadae kuwa wa ushindani mkubwa. 

Miaka minne baadaye mnamo mwaka 2019 alirejea CCM.

Lowassa, mwanasiasa anayeacha urathi wenye pande mbili za sarafu 

Lowassa alifariki dunia Februari 10, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar Es Salaam, kutokana na tatizo la kujikunja utumbo, tatizo la mapafu na shinikizo la damu.

Ibada ya taifa ya kuuaga mwili wa Edward Lowassa.
Mwili wa Edward Lowassa ulipoagwa Dar es Salaam, Tanzania kabla ya kusafirishwa kwa mazishi mkoani Arusha. Picha: Eric Boniface/DW

Ameacha mke mmoja Regina Lowassa na watoto wa watano, na pia anakumbukwa na jamii yake ya kifugaji ya maasai kwa mchango mkubwa wa maendeleo.

Anaacha nyuma urathi wenye taswira mbili, ya mwanasiasa kigogo na nyingine ya mtu aliyelitia doa jina lake mwenyewe. 

Miaka ya mwanzo ya kuingia kwake kwenye siasa alisifika kama mtumishi wa umma asiye mwoga, aliyechukia uzembe na mchapakazi hodari. Hadhi hiyo aliibeba hata baada ya kuteuliwa na rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Disemba 2005.

Kiasi miaka miwili baadaye alilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa kubwa ya rushwa. 

Kashfa ya Richmond na anguko la Lowassa

John Magufuli na  Edward Lowassa
Edward Lowassa (kulia) na aliyekuwa rais wa Tanzania hayati John Pombe MagufuliPicha: DW/S. Khamis

Kashfa ya Richmond ilisadifu kuwa kihunzi kirefu kwa Lowassa. Alituhumiwa kutumia nafasi yake kurefusha mkataba wa kampuni hewa ya Richmond iliyopewa kandarasi ya kufua umeme.  

Kamati ya bunge iliyofanya uchunguzi wa kasfha ya Richmond, ilisema Lowassa alipuuza ushauri wa kampuni ya taifa ya kufua umeme, TANESCO na kushinikiza kurefushwa mkataba wa Richmond.  

Uamuzi huo uliligharimu taifa mabilioni ya shilingi. Kamati hiyo iliyoongozwa na mbunge wa jimbo la Kyela, Harrison Mwakyembe ilisema kampuni hewa Richmond ilikuwa ikipokea dola 100,000 za marekani kila siku bila kuzalisha hata wati moja ya umeme.  

Ilikuwa dhahiri kuwa waziri mkuu aliyeingia madarakani kwa ahadi ya mageuzi asingeweza kusalimika. Hatimaye Februari 7 2008 Edward Lowassa alisalimu amri.  

Mwanasiasa huyo hakuwahi kufikishwa mahakamani wala kupata nafasi rasmi ya kujitetea kuhusu uhusika wake kwenye kashfa ya Richmond.  

Mwenyewe tangu wakati huo hadi kifo chake aliendelea kukanusha kuhusika na kashfa hiyo.