1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Marekani kuihakikishia msaada zaidi Ukraine

Lilian Mtono
23 Februari 2024

Kiongozi wa Baraza la Seneti nchini Marekani Chuck Schumer anazuru Ukraine kwa lengo la kumuhakikishia Rais Volodymyr Zelensky kwamba mamlaka hiyo kamwe haitaitelekeza Ukraine.

https://p.dw.com/p/4cn3x
McConnell, Zelensky na Schumer kwenye jengo la Capitol 2023 | Mahusiano ya Kimataifa
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiongozana na Mitch McConnell(L) ambaye ni kiongozi wa walio wachache bungeni na Chuck Schumer(R) ambaye ni kiongozi wa walio wengi, wakati Zelensky alipohudhuria kikao kwenye Bunge la MarekaniPicha: Julia Nikhinson/UPI/picture alliance

Schumer anafanya ziara nchini Ukraine Ijumaa hii ambapo anatarajiwa kumuhakikishia Rais Volodymyr Zelensky na wengine kwamba Bunge la nchi hiyo litapeleka awamu nyingine ya misaada katika wakati ambapo uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ukikaribia kuingia mwaka wa tatu. 

Ziara ya Schumer inafanyika wakati msaada wa dola bilioni 60 kwa ajili ya Ukraine ukiwa bado umekwama katika Baraza la Wawakilishi katika wakati ambapo Ukraine inahitaji mno misaada. Rais Zelensky amesema ucheleweshwaji huo kutoka Washington na washirika wa Magharibi umeisaidia Urusi kusonga mbele katika uwanja wa vita, wakati wanajeshi wa Ukraine wakiripotiwa kupungukiwa pakubwa na silaha pamoja na makombora.

Wabunge kutoka vyama vyote vya Republican na Democrat walikwenda Ulaya wiki iliyopita na kuahidi kwamba Marekani kamwe haitaitelekeza Ukraine na washirika wake wengine wa Ulaya. Schumer alisisitizia hilo alipozungumza na shirika la habari la AP.

Soma pia:Bundestag yapiga kura ya kupinga kuipatia Ukraine makombora ya masafa marefu

Mbali na ziara hii, Washington yenyewe, inaandaa vikwazo vipya dhidi ya makampuni 50 yanayojihusika na vita vya Urusi nchini Ukraine, maafisa wamesema. Vikwazo hivyo vinatarajiwa wakati vita hivyo vikielekea mwaka wa tatu na kwa upande mwingine kifo cha mpinzani mkubwa wa Rais Vladimir Putin, Alexei Navalny akiwa gerezani.

Marekani | Jengo la Bunge
Bendera ya Ukraine ikipepea mbele ya jengo la Bunge la nchini Marekani ambako mjadala bado ungalipo juu ya msaada mpya wa kijeshi nchini UkrainePicha: Roberto Schmidt/Getty Images

Kirby: Hivi ni vikwazo vikubwa zaidi tangu 2022

Mapema, Mkurugenzi wa mawasiliano wa masuala ya Usalama wa Taifa katika Ikulu ya White House, John Kirby alisema Marekani imeandaa rundo la vikwazo dhidi ya Moscow vyenye lengo la kuidhoofisha kabisa kijeshi. Wizara ya Fedha imevitaja vikwazo hivyo kuwa vikubwa zaidi tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka 2022.

Marekani tayari imeiwekea Urusi msururu wa vikwazo vilivyosababisha kuwekwa kwa ukomo wa bei ya mafuta ya Urusi ili kupunguza mapato yatokanayo na bidhaa za mafuta nchini humo.

Huku hayo yakiendelea huko nchini Urusi, Rais Putin ameendelea kuwamwagia sifa wanajeshi wake kwa kuendelea kulipambania taifa hilo na kuwaita ni mashujaa wa kweli ambao taifa hilo lina imani nao kubwa. Akasema ingawa ni ngumu, lakini watafanya kila linalowezekana ili kuwawezesha kumaliza kazi waliyopewa na kikubwa kuliimarisha zaidi jeshi hilo. Putin alisema hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Ijumaa hii.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na Waziri wa ulinzi Sergei Shoigu
Rais Vladimir Putin akiwa na Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu walipokutana katika Ikulu ya kremlin mjini Moscow, Februari 20, 2024Picha: ALEXANDER KAZAKOV/AFP

"Kwa kuzingatia uzoefu wa kupigana, tutaendelea kuimarisha Vikosi vya jeshi kwa kila inavyowezekana na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kiufundi na kuvifanya vya kisasa zaidi" alisema Putin.

Watatu wafa kwa shambulizi la droni, Odessa

Taarifa kutoka Kyiv zinasema Urusi imewauwa takriban watu watatu kwa kutumia droni katika mji wa Odessa nchini Ukraine. Mamlaka za eneo hilo zimesema droni hiyo iliangukia jengo moja la kampuni katika eneo hilo la pwani. Zoezi la kuwatafuta watu waliofukiwa chini ya kifusi linaendelea.

Na huko nchini Brazil, Rais Inacio Lula da Silva amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov anayeyashutumu mataifa ya Magharibi kwa kuungana dhidi ya Urusi kuelekea vita vya Ukraine. Hata hivyo viongozi hao hawakusema hadharani kile walichojadiliana. Mapema, Rais Lula alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na kujadiliana naye kuhusiana na vita hivyo, pembezoni mwa mkutano wa kundi la Mataifa yaliyoendelea na yanayoinukia kiuchumi, G20 huko Rio De Jeneiro.

Lula anapinga shinikizo linaloongozwa na Marekani la kuitenga na kuiadhibu Urusi kwa uvamizi wake dhidi ya Ukraine.